KOCHA mkuu wa Cesiaa FC, Sultan Juma amesema timu hiyo bado haijawa salama kwenye mbio za kusalia Ligi Kuu ya Wanawake na italazimika kupambana katika mechi mbili zilizobaki ili kujihakikishia nafasi ya kuendelea kucheza ligi hiyo msimu ujao.

Juma amesema kikosi hicho kina kibarua kigumu cha kusaka pointi sita zilizobaki kutokana na ushindani mkubwa uliopo mkiani na timu kadhaa bado zinapigania hatma yao.

Kocha huyo alikiri Cesiaa ilianza msimu kwa kiwango kizuri kilichowapa matumaini ya kufanya vizuri, lakini mambo yamekuwa tofauti mwishoni baada ya timu kuanza kupoteza mwelekeo na kushindwa kupata matokeo waliyokuwa wakiyatarajia.

“Tulianza vizuri na tulikuwa tunapata matokeo ambayo yalitupa matumaini makubwa, lakini katika kipindi cha mwisho tumekuwa tukisuasua. Hiyo imetuweka kwenye mazingira ambayo yanatulazimisha kupambana zaidi katika mechi zilizobaki,” amesema Sultan.

“Tunafahamu umuhimu wa mechi hizi mbili za mwisho. Kila mchezaji anatambua kilichopo mbele yetu na lengo ni kuhakikisha tunapambana hadi dakika ya mwisho ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kubaki ligi,” amesema.

Ceasiaa iko nafasi ya 10 ikiwa na pointi 15 baada ya kucheza mechi 19, ikishinda nne, sare tatu na kupoteza mechi 12.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *