KOCHA mkuu wa Tausi FC, Martin Hammel amesema bado ana matumaini makubwa ya timu hiyo kubaki kwenye Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu licha ya changamoto walizokutana nazo tangu mwanzoni mwa msimu.

Hammel amesema kikosi hicho kimeanza kuonyesha mabadiliko katika mechi za hivi karibuni na anaamini kiwango hicho kinaweza kuwasaidia kuvuna matokeo mazuri katika mechi miwili iliyosalia kabla ya msimu kumalizika.

Kocha huyo alikiri Tausi FC haikuwa na mwanzo mzuri baada ya kupanda daraja, jambo lililowafanya kujikuta katika mazingira magumu kwenye msimamo wa ligi, lakini kwa sasa anaona timu imeanza kupata mwelekeo sahihi.

HUMM 01

“Hatukuanza ligi vizuri, lakini taratibu timu imeanza kujipata. Wachezaji wameongeza kujiamini na tunaonyesha ushindani mkubwa zaidi kuliko mwanzo wa msimu. Bado tuna mechi mbili muhimu na tunapambana kuhakikisha tunapata pointi sita zilizobaki,” amesema Hammel.

Aliongeza lengo kubwa kwa sasa ni kuhakikisha Tausi FC inamaliza msimu katika nafasi nzuri itakayowaruhusu kuendelea kushiriki Ligi Kuu msimu ujao.

Tausi ni miongoni mwa timu zilizopanda daraja msimu huu baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza kabla ya kubadili jina na awali ilikuwa ikiitwa Ukerewe Queens.

HUMM 02

Mbali na Tausi FC iliyopo nafasi ya sita ikiendelea kupambana kujinasua kwenye mtego wa kushuka daraja, timu za Geita Queens, Ruangwa Queens na Bilo Queens zimekuwa zikihangaika katika mapambano ya kusalia ligi.

Timu hizo zilipata nafasi ya kucheza Ligi Kuu baada ya kumaliza katika nafasi nne za juu kwenye mashindano ya ligi ya Daraja la kwanza yaliyofanyika jijini Mwanza, lakini zimejikuta zikikumbana na ushindani mkubwa wa ligi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *