
Ikiwa ni katika muendelezo wa ukiukaji wa makubaliano ya usitishaji vita na mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya miji na vijiji vya kusini mwa Lebanon yaliyotekelezwa zaidi ya mara 36 mchana na Jumapili usiku, watu 12 wameuawa shahidi na wengine 35 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya jinai.
Watu wanne wameuawa shahidi katika hujuma ya anga ya utawala wa Israel katika mji wa “Abassiyah” katika mji wa Sour au Tyre kwa Kiingereza, kusini mwa Lebanon. Pia, katika mashambulizi sita ya anga ya Israel kwenye kitongoji cha Deir al-Zahrani, watu wanane wameuawa shahidi na wengine 16, wakiwemo watoto watano na wanawake sita kujeruhiwa, ambapo majengo ya makazi yameharibiwa vibaya.
Pia inaripotiwa kuwa watu watatu, wakiwemo watoto wawili, wamejeruhiwa katika shambulio la anga katika eneo la Jadid Ansar. Huko Adousia, pikipiki moja pia imeshambuliwa kinyama katika shambulio la anga la Israel, na kupelekea watu watatu kujeruhiwa.
Ndege hizo za kivita za Israel pia zimelenga eneo lililo karibu na hospitali ya Hiram mjini Sour, na kuwajeruhi wafanyakazi 13 wa hospitali hiyo wakiwemo wauguzi.
Wakati huo huo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Qatar imelaani katika taarifa mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel dhidi ya Lebanon, upanuzi wa uvamizi wa nchi kavu wa utawala huo katika eneo la kusini mwa Lebanon, na kuwalenga raia, ikitaja vitendo hivyo kuwa uchochezi hatari wa vita, ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya Lebanon, pamoja na ukanyagaji wa wazi wa sheria za kimataifa za kibinadamu. Imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuulazimisha utawala vamizi wa Israel usitishe mara moja mashambulizi yao ya mara kwa mara dhidi ya Lebanon.
Hamish Falconer, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza pia ameonya kwamba kuendelea kuongezeka mivutano nchini Lebanon kunadhoofisha juhudi za kidiplomasia na kuna taathira zisizokubalika kwa raia.
Johann Wadful, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani ameeleza kusikitishwa kwake na kupanuka kwa mashambulizi ya nchi kavu ya utawala ghasibu wa Israel huko kusini mwa Lebanon na kuonya kwamba kushadidi mapigano ya kijeshi kunahatarisha hali mbaya ya sasa kuwa mbaya zaidi katika siku zijazo.