
Rais wa Kenya, William Ruto, amemwagiza waziri wa elimu kushirikisha wadau wote husika na kuanzisha mashauriano kuhusu ujumuishaji rasmi wa shule za Kiislamu nchini, zinazojulikana kama Duksi au Madrasa, katika mfumo wa elimu wa Kenya.
Akizungumza Jumatatu wakati wa maadhimisho ya miaka 63 ya Madaraka yaliyofanyika katika Kaunti ya Wajir, Ruto amesema hatua hiyo itahakikisha kuwa kila mtoto anapata njia inayotambuliwa rasmi ya kuingia katika elimu, bila kujali mazingira yake au asili yake.
Amekiri kuwa baadhi ya wanafunzi katika maeneo yaliyotengwa bado wako nje ya mfumo rasmi wa elimu kutokana na ukosefu wa njia mbadala za kujifunza zinazotambuliwa, hususan mifumo ya Duksi, Madrasa na elimu ya jamii za wafugaji.
Rais Ruto amesema kila mtoto anastahili kufunguliwa mlango wa elimu, na kwamba ni wajibu wa serikali kuhakikisha hakuna mlango wa maarifa unaobaki umefungwa.
Akiweka mambo katika muktadha mpana wa kitaifa, Rais Ruto amelinganisha mwelekeo wa sasa wa maendeleo ya Kenya na kipindi cha mwanzo wa uhuru, akisema kuwa mustakabali wa ukombozi wa taifa sasa utaamuliwa zaidi katika taasisi za elimu kuliko katika medani za mapambano ya kivita.
Akihutubia maadhimisho ya kwanza kabisa ya Madaraka kufanyika Kaskazini mwa Kenya tangu kupatikana kwa uhuru, alitolea mifano mataifa yaliyoendelea kupitia uwekezaji wa kudumu katika elimu, yakiwemo Korea Kusini, Malaysia, Singapore na Finland.
Aidha, amesema zaidi ya walimu 100,000 wameajiriwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, huku walimu wengine 20,000 wakitarajiwa kuajiriwa mwaka huu.
Kuhusu Kaskazini mwa Kenya, Rais alisema serikali imechukua hatua maalumu ili kukabili upungufu wa walimu, kwa kutoa mafunzo na kuajiri walimu wa maeneo husika.
Alisema vyuo vya mafunzo ya walimu vya Wajir, Kotulo na Mandera vimeanza kufanya kazi kikamilifu, sambamba na Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Garissa.
Vilevile, amesema zaidi ya vijana 850,000 wamejiandikisha katika taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Kitaaluma, wakipata stadi za kusaidia maendeleo ya taifa.
Katika upande wa ulinzi wa kijamii, amesema programu za lishe mashuleni sasa zinawanufaisha wanafunzi milioni 2.4 katika maeneo kame na nusu-kame, pamoja na upanuzi wa usambazaji wa walimu na huduma za muunganisho wa kidijitali.
Rais Ruto pia ameahidi kuanzisha chuo kikuu mjini Wajir, akisema ujenzi utaanza ndani ya mwaka huu kama sehemu ya juhudi za kupanua upatikanaji wa elimu ya juu katika eneo hilo ambalo limepuuzwa kimaendeleo tokea uhuru wa Kenya miaka 63 iliyopita.