Hanang. Wananchi wa Kijiji cha Masakta, Kata ya Masakta wilayani Hanang, mkoani Manyara, wameiomba Serikali kupandisha hadhi Zahanati ya Masakta na kuiboresha kwa kuongeza watumishi pamoja na huduma muhimu za matibabu ili kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa eneo hilo.
Ombi hilo liliwasilishwa leo, Juni 1, 2026, na Mwenyekiti wa Shina Namba Moja, Tawi la Masakta, Dismas Gwasima, mbele ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, aliyekuwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Manyara.
Kihongosi ameanza ziara ya mikoa ya Kanda ya Kaskazini katika Mkoa wa Manyara akitokea Mkoa wa Kilimanjaro.
Akisoma taarifa ya shina hilo, Gwasima amesema Zahanati ya Masakta imekuwa ikitoa huduma kwa wananchi kwa zaidi ya miaka 20, lakini bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa huduma bora za afya.
Amesema wananchi wanaomba zahanati hiyo ipandishwe hadhi na kuongezewa madaktari na watumishi wa afya, pamoja na huduma za mama na mtoto, huduma za upasuaji na nyumba za watumishi wa afya ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
“Wanawake wajawazito na watoto wanapata changamoto kubwa kutokana na ukosefu wa baadhi ya huduma muhimu. Tunaomba Serikali iangalie uwezekano wa kuboresha zahanati yetu ili iweze kukidhi mahitaji ya wananchi,” amesema Gwasima.
Mbali na sekta ya afya, Gwasima amesema wanachama wa shina hilo wanaendelea kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za Chama cha Mapinduzi kupitia mfumo wa uanachama wa kielektroniki, huku wakishirikiana katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii.
Amesema shina hilo pia limeunda Kamati ya Ulinzi na Usalama inayoshirikiana na viongozi wa kijiji na vitongoji kufuatilia usalama wa wananchi na kukabiliana na matukio ya uhalifu, ikiwemo wizi na uporaji.
Wanachama wa CCM katika Shina namba moja tawi la Masakta, wilayani Hanang’ mkoa wa Manyara.
Aidha, wanachama hao wamempongeza Rais, Samia Suluhu Hassan kwa kutekeleza Ilani ya CCM na kuendelea kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta mbalimbali.
Akijibu ombi hilo, Kihongosi amesema suala la kupandishwa hadhi kwa zahanati hiyo linapaswa kuzingatia vigezo vilivyowekwa na Serikali, lakini amewahakikishia wananchi kuwa CCM itaendelea kulifuatilia ili lipatiwe ufumbuzi.
“Jambo kubwa lililojitokeza katika taarifa yenu ni ombi la zahanati kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya. Kama vigezo vitakuwa vimekidhiwa, niwahakikishie kuwa chama kitaendelea kusimamia jambo hili kwa asilimia 100. Mkuu wa Mkoa, viongozi wa wilaya na mbunge wenu wamelisikia, hivyo kwa pamoja tutafuatilia ili wananchi wapate huduma wanazozihitaji,” amesema Kihongosi.
Amesema moja ya malengo ya ziara hiyo ni kusikiliza changamoto za wananchi na kuzifikisha katika mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati.
“CCM ndiyo chama kinachounda Serikali, hivyo msingi wake mkubwa ni kuwasikiliza wananchi, kutatua shida zao na kuhakikisha changamoto zinazohitaji ngazi za juu zinafikishwa katika mamlaka husika ili zipatiwe ufumbuzi,” amesema.