
Arusha. Siku za hivi karibuni kumekuwa na matukio mbalimbali ya kushangaza yanayohusisha vijana, ikiwemo vitendo vya uhalifu pamoja na mauaji ambayo yameelezwa chanzo chake ni matumizi ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia jijini Arusha.
Baadhi ya matukio, yamekuwa yakihusisha madereva bodaboda kujichukulia sheria mikononi kwa kuwaadhibu watu na kusababisha vifo au uharibifu wa mali.
Yapo matukio kadhaa ambayo yameendelea katika jiji hilo ikiwepo kuteketezwa kwa daladala baada ya kumgonga bodaboda na kusababisha kifo cha dereva aliyekuwa anavuka barabara eneo la Morombo.
Usiku wa kuamkia Mei 18, 2026 mkazi wa Sinoni, Emmanuel Thomas aliuawa kwa kuchomwa kisu sehemu mbalimbali za mwili wake na chanzo kikielezwa alitoa salamu kwa kuonyesha ishara ya tano kwa baadhi ya watu na kuwaacha wawili.
Inadaiwa vijana hao walikasirishwa na kitendo hicho na kumtaka awasalimie kwa nguvu, hali iliyosababisha mabishano na baadaye ugomvi.
Mbali na matukio hayo wapo wageni wanaopewa tahadhari ya kuwa makini katika maeneo wanayotembelea ikiwepo katika barabara ya kuelekea Tengeru.
“Nimekuja Arusha kutembea na kufikia kwa mwenyeji wangu lakini amenipa tahadhari ya kuwa makini ninaporudi nyumbani kwa sababu hakutabiriki vijana hujiamulia mambo yao hata wanaweza kukuibia na mambo hayo hufanyika kuanzia saa moja jioni,” anasema Samira Idd.
Mmoja wa wazazi kutoka eneo la Muriet, Mariana Japhet anasema tatizo wazazi wengi wameacha jukumu lao la msingi la malezi na kuacha kwa wasaidizi wao wa majumbani.
“Siku hizi malezi wazazi wameacha kwa wasaidizi wao majumbani badala ya kukaa kwenye nafasi zao, hili linachangia mmomonyoko wa maadili kwa vijana,” anasema.
Thomas Lairumbe anasema vitendo hivyo vinachangiwa na baadhi ya wazazi na walezi wenyewe kukosa maadili jambo linalochangia watoto wao kuiga kutoka kwao.
Mmoja wa vijana, Ashraf Mohamed anasema suala hilo linachangiwa na kampani mbaya kutoka kwa wenzao.
“Vijana wengine wanajikuta wanaingia kwenye mkumbo kutokana na marafiki zao. Nadhani ni muhimu jamii ikahimiza malezi bora na kufungua fursa za ajira zaidi kwa vijana ili wasikae kwenye magenge yanayowashawishi kufanya vitendo viovu,”anasema
Takwimu zinaeleza
Katika taarifa ya Hali ya Dawa za Kulevya ya Mwaka 2025 iliyowasilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi, Mei 29, 2026 imeonyesha matumizi ya dawa za kulevya kwenye vyakula yameibua changamoto mpya inayohitaji uangalizi mkubwa wa jamii na vyombo vya dola.
Profesa Kabudi alisema operesheni zilizofanyika mwaka 2025 zinaonyesha mamlaka zilikamata tani 3.2 za bangi aina ya skanka, ikiwemo kilogramu 9.82 zilizokuwa zimechanganywa kwenye biskuti na keki ambapo watuhumiwa 137 walikamatwa kuhusiana na biashara hiyo wakiwemo wanaume 116 na wanawake 21.
Profesa Kabudi alitaja mikakati ya kukabiliana na tatizo la dawa za kulevya ni kupunguza uhitaji wa matumizi, kupunguza madhara kwa waraibu pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kitaifa na kimataifa.
Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja, watu 85,425 wenye uraibu walipatiwa matibabu bure lengo ni kurudisha nguvu kazi ya Taifa ambayo ingeweza kupotea kutokana na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema Tanzania imemaliza tatizo la dawa za kulevya aina ya heroini na imetajwa kuwa ni mfano wa dunia katika udhibiti huo ingawa akasema haipaswi kulewa sifa.
Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo aliutaja Mkoa wa Morogoro unaongoza kwa kilimo cha bangi ukifuatiwa na Mara, Tabora na Arusha.
Tatizo malezi
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mkude, anasema mmomonyoko wa maadili na ongezeko la vitendo vya kihalifu miongoni mwa vijana vinachangiwa zaidi na malezi duni pamoja na ukosefu wa usimamizi wa wazazi.
Anasema uhuru mkubwa wa watoto bila uangalizi huwafanya kujiingiza katika matumizi ya pombe na dawa za kulevya, hali inayochochea vitendo vya uhalifu na kuporomoka kwa maadili.
Anafafanua kuwa baadhi ya vijana wamekuwa wakionesha kutokuwa na hofu wala kujali thamani ya maisha kutokana na athari za matumizi ya dawa za kulevya pamoja na mmomonyoko wa maadili unaoendelea katika jamii.
“Wakati mwingine unaona vijana wanafanya mambo kana kwamba maisha hayana thamani tena hali hii ni hatari kwa mustakabali wa taifa letu,”anasema.
Katika wilaya hiyo, anasema aliunda timu maalumu ya kufuatilia changamoto za mmomonyoko wa maadili katika shule za msingi na sekondari wilayani humo, huku taarifa mbalimbali zikiwa zimeanza kupatikana kuhusu maeneo yenye changamoto kubwa zaidi.
“Tumewaambia walimu wawe waangalizi wa karibu wa watoto, sehemu wanazoenda na muda wanaokaa huko unatakiwa kufuatiliwa maana tabia zinaweza kuanzia nyumbani zikahamia shuleni kama hakuna usimamizi,” anasema.
Mkude anasema katika jitihada za kurejesha maadili, Serikali pia imeanza kuhamasisha vikao vya kijamii vitakavyowahusisha wazee wa mila, viongozi wa kata na maofisa maendeleo ya jamii ili kujadili namna ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Anasema lengo ni kuhakikisha jamii inashiriki moja kwa moja katika kurejesha maadili kwa vijana badala ya kuiachia Serikali pekee jukumu hilo.
“Nilifanya mkutano Moshono nikitarajia wananchi wengi wajitokeze kuchangia mawazo kuhusu namna ya kurejesha maadili, lakini waliojitokeza walikuwa wachache. Hata hivyo tulikubaliana kuwa wazee wa mila na viongozi wa jamii waanze kukaa pamoja kujadili chanzo cha matatizo haya,” anasema
Anasema jamii inapaswa kuacha tabia ya kufumbia macho vitendo viovu vinavyoanza kwa watoto tangu wakiwa wadogo.
“Mimi nimeanza kampeni binafsi ya kuzungumza kwenye misiba na mikusanyiko mbalimbali nikisisitiza wazazi wasiwe waoga kukemea tabia yoyote ovu mapema. Usipomrekebisha mtoto mapema, baadaye tunapata kizazi cha namna hii.”
Mkude anasema hata baadhi ya vijana wanaoendesha bodaboda wamekuwa wakieleza kuwa kuna watu wanaotumia mwamvuli wa bodaboda kufanya vitendo vya kihalifu kwa kutumia pikipiki zisizo zao au zilizoibwa.
Kwa upande wake, wakili wa kujitegemea na mdau wa haki za binadamu, Peter Madeleka anasema matumizi ya dawa za kulevya ni tatizo mtambuka ambalo haliwezi kujadiliwa bila kuangalia suala la malezi ndani ya jamii.
Madeleka anasema wazazi wengi wamekuwa wakishindwa kufuatilia mienendo ya watoto wao, jambo linalowafanya vijana kuingia kwenye makundi mabaya na kuanza kutumia dawa za kulevya.
“Unapoona matumizi ya dawa za kulevya yanaongezeka kwa vijana maana yake jamii imetelekeza wajibu wake wa msingi wa malezi bora. Wazazi wengi hawafuatilii watoto wao ipasavyo,” anasema
Kuhusu nafasi za viongozi wa dini, anasema wanapaswa kuongeza juhudi katika kufundisha maadili kwani vijana wengi wanaoingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya hupoteza mwelekeo wa maisha na kuingia kwenye vitendo vya kihalifu.
“Matumizi ya dawa za kulevya yanamfanya kijana awe mbali na Mungu na baadaye anajiingiza kwenye mauaji, wizi na uvunjifu mwingine wa sheria,” anasema Madeleka.
Madeleka anasema pamoja na uwepo wa sheria kali dhidi ya dawa za kulevya, bado usimamizi wake unapaswa kuongezwa nguvu ili kudhibiti uzalishaji, usafirishaji na matumizi ya dawa hizo.
“Sheria zipo nzuri lakini utekelezaji wake wakati mwingine unakuwa dhaifu. Watu wakiona hakuna usimamizi madhubuti wanaendelea kufanya vitendo hivyo bila hofu,”anasema.
Viongozi wa dini wanena
Imamu Mkuu wa Msikiti wa Unga Ltd, jijini Arusha, Sheikh Ayubu Hussein anasema wazazi na walezi wana wajibu wa kusimamia wajibu wa pamoja na kufuatilia mienendo ya vijana.
“Sasa hivi mfano biashara za maduka kawaida unakuta viti nje, vijana wanakaa hapo kunywa pombe nadhani likidhibitiwa hili itasaidia kupunguza matumizi ya dawa za kulevya na pombe kwa kundi la vijana.”
“Tatizo hakuna ajira kwa vijana, Serikali iangalie ile mikopo ya halmashauri kwa vijana iendelee kutoa naamini vijana wengi wakiwa na ajira itapunguza matumizi ya dawa za kulevya.”
Anasema kuwa viongozi wa dini wanajitahidi kusisitiza maadili, hivyo akaomba wazazi wafuatilie mienendo ya watoto wao sio sawa vijana wanatoka wazazi hawajui wanaenda wapi na wanarudi saa ngapi.
Mratibu wa Vijana wa KKKT nchini, Mchungaji Frank Mng’ong’o, anasema malezi duni yanachangia vitendo hivyo na kuwa elimu ya makuzi ni muhimu kwa vijana.
“Hali ya uchumi Imekua changamoto kwa wengi, makundi rika wanajikuta wanafanya vitu hivyo, kutokumwelewa Mungu ni sababu pia inayochangia kujiingiza kwenye matukio hayo.
“Kwa upande wa malezi hata nyumbani wazazi wengine wanachangia mzazi anakunywa pombe mbele ya watoto huyo kijana hana ujasiri wa kutokunywa inachangia vijana kuingia kwenye vitendo hivyo, wazazi na walezi wajitahidi kuwa mfano kwa watoto wao ili kuwasaidia kuanzia nyumbani ili wawe na maadili, elimu ya makuzi iwekewe nguvu,” anasema.