Dar es Salaam. Aliyekuwa mgombea urais kupitia ACT Wazalendo, Luhaga Mpina amesema Tume ya kuchunguza jinai katika mauaji ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, haitatatua tatizo la msingi bali ni kupoteza muda, matumizi mabaya ya fedha za umma na kutaka kufunika ukweli.
Mpina ameyasema hayo leo Juni Mosi, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na vyombo vya habari, akitoa maoni yake kuhusu ripoti ya Tume ya uchunguzi wa matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo.
Novemba 18, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume hiyo chini ya mwenyekiti wake, Jaji mstaafu, Mohamed Chande. Tume hiyo ilitumia siku 153 ikikutana na mashahidi mbalimbali wanaoeleza wanachokijua kuhusu matukio hayo.
Aprili 23, 2026, Jaji Chande alikabidhi ripoti yake kwa Rais Samia, ikiwa na mapendekezo mbalimbali ikiwemo kuitaka Serikali iunde tume ya uchunguzi wa kijinai kufuatia matukio hayo.
Katika utekelezaji wa pendekezo la tume, Mei 18, 2026, Rais Samia aliunda Tume hiyo huku akimteua Jaji Shaban Lila kuwa Kamishna na Mwenyekiti wake.
Akizungumzia Tume hizo, Mpina amesema Tume ya Jaji Chande haikufanya kazi yake kikamilifu kwani imeacha maswali mengi vichwani mwa wananchi ikiwamo watu 245 ambao hawajaonekana tangu vurugu za siku ya uchaguzi.
Aliyekuwa mgombea urais kupitia ACT Wazalendo, Luhaga Mpina wakati akizungumza na vyombo vya habari leo Juni Mosi, 2026 jijini Dar es Salaam.
Mpina ambaye hakuteuliwa kugombea urais baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kumwekea pingamizi, amesema bado Watanzania wana uchungu mioyoni mwao kwa sababu Tume ya Jaji Chande haijatatua matatizo ya msingi yaliyosababisha watu kuandamana siku ya uchaguzi.
“Pendekezo la kuundwa Tume nyingine halikubaliki na hatuwezi kuwa na Tume juu ya Tume tena zinazoundwa na mamlaka ile ile, leo Rais ameteua tena tume ya mrengo mmoja anayoiita ‘Tume ya Uchunguzi wa Kijinai wa Matukio ya Ghasia ya wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025’.
“Tume ya uchunguzi wa kijinai imechelewa na haiwezi kupewa nafasi tena. Mwanadiplomasia mashuhuri nchini Profesa Anna Tibaijuka alishauri mapema kupitia andiko lake Novemba 15, 2025 katika mtandao wa X akisisitiza kuundwa kwa Tume ya Kijaji (Judicial Enquiry) lakini ushauri wake ulipuuzwa. Leo Serikali inarejea mawazo yake kwa kuchelewa, haitasaidia. Watanzania na jumuiya za kimataifa haziwezi kusubiri tena,” amesema.
Mpina ambaye ni mbunge wa zamani wa Kisesa kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), amesema haiwezekani jambo moja likaundiwa Tume mbili akidai huo ni mkakati wa kukwepa uwajibikaji na kutaka kuwabebesha watu wengine mzigo huo.
Ameongeza kwamba kabla ya kuundwa kwa Tume ya kuchunguza jinai inayoongozwa na Jaji Lila, Watanzania wanataka majibu ya namna watakavyolipwa fidia kwa kuwapoteza wapendwa wao ambao ni miongoni mwa watu 518 waliouawa wakati wa uchaguzi.
“Familia nyingi zimepoteza watu waliokuwa wanawategemea, wapo waliopoteza waume zao, wapi waliopoteza baba zao, wengine wamepoteza mama zao, kaka na dada. Lakini hakuna utaratibu wowote wa kuzifidia familia hizo ili maisha yaendelee.”
“Mimi nimechunga ng’ombe, ukienda kuchunga ng’ombe hata 100, ukampoteza mmoja, hurudi nyumbani hadi apatikane. Huyo ni ng’ombe tu, itakuwaje kwa binadamu? Lakini Serikali yetu imepoteza watu 518, haitangazi hata maombolezo wala bendera kupepea nusu mlingoti,” amehoji Mpina.
Mpina amedai kuwa hivi karibuni Serikali imekuwa na uhusiano mbaya na viongozi wa kisiasa, wa dini, wazee, wanaharakati, wanahabari hasa wakosoaji ambao wamekuwa wakitungiwa kesi za kubambikwa mara kwa mara ikiwemo ugaidi na uhaini na wengine kuzuiwa kugombea kwa nguvu.
“Serikali ilishauriwa kikamilifu kabla ya uchaguzi ili isije kusababisha vurugu lakini mfumo mzima wa Serikali ulikaidi na kuendelea na shughuli hiyo,” amedai Mpina.