Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Nchini Ufaransa, moto umeharibu zaidi ya nyumba 100 katika mji wa Le Porge ulioko karibu na eneo la mapumziko la Cap Ferret, nyumba nyingi zimeteketea kabisa huku zingine zikibaki na kuta zilizochomeka, na maeneo yaliyokuwa yamefunikwa na miti sasa yamegeuka majivu.
Moto huo pia unaendelea kutishia jiji la Bordeaux, mojawapo ya vituo vikuu vya usafiri na eneo linalojulikana kwa mashamba ya mizabibu.
Hadi sasa, zaidi ya watu 220,000 wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao kutokana na kuenea kwa moto huo uliochochewa na wimbi kali la joto linaloikumba Ulaya.
Wakati huo huo nchini Uhispania, vikosi vya zimamoto, wanajeshi na wakazi wa kujitolea wanaendelea kupambana na moto mkubwa unaowaka katika maeneo ya Madrid na Avila.
Moto huo umeunguza zaidi ya hekta 50,000 za ardhi na umetajwa kuwa miongoni mwa moto mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Zaidi ya watu 75,000 wamehamishwa makazi yao nchini Uhispania, huku wengine 30,000 wakitakiwa kubaki ndani ya nyumba zao kwa usalama wakati juhudi za kuudhibiti moto huo zikiendelea.