Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma imeamuru wajumbe wa Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, waitwe mahakamani hapo kwa kutangazwa kupitia Gazeti la Mwananchi.

Uamuzi huo umetolewa jana Jumatatu, Juni Mosi, 2026 na  Jaji Agustine Rwizile, anayesikiliza shauri linaloikabili tume, kutokana na kutofika mahakamani hapo wao wenyewe au wawakilishi wao wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya usikilizwaji.

Tume hiyo maarufu kama Tume ya Jaji Lila, inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Shaban Lila imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, na mwenyekiti na wajumbe wake walitangazwa rasmi Mei 18, 2026.

Mbali na mwenyekiti, wajumbe wa Tume hiyo ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.

Rais Samia aliunda Tume hiyo kufuatia ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Hata hivyo, siku chache tu baada ya kutangazwa kwa Tume hiyo na wajumbe wake, mwanaharakati Buberwa Buberwa na mwenzake Joseph Mabugo, wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, walikwenda mahakamani kuhoji uhalali wake.

Buberwa na Mabugo wamefungua shauri dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), na mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Lila na wajumbe wake hao watatu, Mjemmas, Bawazir na Sumari (mjibu maombi wa pili mpaka wa tano mtawalia).

Katika shauri hilo waombaji hao wanaomba ruhusa ya kufungua shauri la mapitio ya Mahakama, kuiomba Mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa Rais Samia kuunda tume hiyo na uteuzi wa wajumbe wake, pamoja na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.

Mei 27, 2026, Mahakama hiyo ilikaa bila wadaawa wote kuwepo, kwa ajili ya kutoa amri maalumu, ambapo iliwapa wajibu maombi siku moja kuwasilisha viapo kinzani na ikapanga kusikiliza shauri hilo leo, huku ikimwelekeza naibu msajili kuwafikishia wadaawa pande zote wito.

Hata hivyo ni mjibu maombi mmoja tu AG, ndiye alifika mahakamani ambaye amewakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Stanley Kalokola. Kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, lakini wajumbe wa tume hiyo hawakufika kwa kuwa naibu msajili hakuweza kuwapata.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa waombaji, Mpale Mpoki aliieleza Mahakama tayari walishawapatia wajibu maombi nyaraka za shauri hilo na hata za wajumbe wa tume hiyo waliziwasilisha ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Wakili Kalokola alikiri kupokea nyaraka hizo na tayari mjibu maombi wa kwanza ambaye anamwakilisha (AG) ameshawasilisha majibu yake kupitia kiapo kinzani.

Hata hivyo, aliieleza Mahakama hawawakilishi wajibu maombi wa pili mpaka wa tano (wajumbe wa tume hiyo) kwa kuwa hajapata maelezo ya kuwawakilisha kutoka Ofisi ya AG.

Kutokana na hali hiyo, wakili Mpoki aliiomba Mahakama ielekeze itumie njia mbadala ya kuwafikishia wito wa kufika mahakamani wajibu maombi hao (wajumbe wa tume) kwa tangazo la gazetini katika gazeti linalosambazwa zaidi nchini na hususan Mwananchi.

Jaji Rwizile aliridhia maombi hayo ya upande wa waombaji na akauelekeza upande wa waombaji kutoa tangazo hilo la wito wa wajumbe hao kufika mahakamani, akielekeza hatua hiyo ifanyike kabla au kufikia Juni 4, 2026 akapanga kusikiliza shauri hilo Juni 8, 2026.

Shauri hilo lilifunguliwa chini ya hati ya dharura sana na mawakili Mpoki na Mwasipu wakidai kama shauri hilo halitasikilizwa haraka wajibu maombi hasa mwenyekiti na wajumbe wa tume wataendelea na mchakato wa uchunguzi huo, wakati hawana mamlaka hayo kikatiba na kisheria.

Kwa mujibu wa nyaraka za shauri hilo za waombaji, kufuatia matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo, Jeshi la Polisi liliwakamata watu kadhaa maeneo mbalimbali nchini na kuwafungua kesi mbalimbali.

Wakati kesi hizo zinaendelea Rais (Samia Suluhu Hassan) aliagiza baadhi ya watuhumiwa waachiwe kutokana na uzito wa ushahidi uliokuwepo.

Kisha aliunda tume ya kuchunguza matukio hayo aliyoyaita ya uvunjifu wa amani (Tume ya Jaji Chande) ambayo iliwasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026.

Pamoja na mambo mengine katika hotuba ya kukabidhi ripoti hiyo mwenyekiti alibainisha kuwa watu 518 waliuawa na wengine kujeruhiwa huku ikitahadharisha kuwa idadi hiyo inaweza kuwa zaidi.

Rais Samia akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo pamoja na mambo mengine alitangaza kuunda tume nyingine ya kuchunguza vitendo vya kijinai wakati wa katika matukio hayo.

Hata hivyo, waombaji wanadai kuwa kitendo cha Rais kuunda tume kuchunguza kitu ambacho aliamuru watuhumiwa waachiwe bila mahakama kutoa uamuzi wowote kuhusu uhusika wao, inakosa mantiki kisheria na ni kitendo cha kibaguzi kinachopingana na ibara ya 13 (1) ya Katiba ya nchi.

Katika hati ya maelezo na kiapo chao cha pamoja waombaji hao wanadai kuwa   kwa Mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchunguzi sura ya 32(R:E 2023) Rais hana Mamlaka ya kuunda Tume nyingine baada ya Tume ya Jaji Chande kutoa ripoti yake.

Wanabainisha kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 21(1)  (a) na (b) Rais kama ataona kuna haja ya kuchunguza zaidi baada ya kusoma ripoti ya Jaji Chande anatakiwa kumuagiza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuliagiza Jeshi la Polisi kupeleleza zaidi.

Pia wanadai mujibu wa kifungu hicho kama ripoti inajitosheleza waliotajwa wachukuliwe hatua za kisheria.

Vilevile wanadai kuwa Rais hana mamlaka ya kuunda tume ya kuchunguza matukio ya kijinai kwa sababu DPP ndiye mtu pekee mwenye jukumu hilo kikatiba na kisheria.

Wamesisitiza kuwa Sheria ya Huduma Mashtaka Sura ya 430 ( Marejeo ya mwaka 2023) inampa DPP mamlaka ya kipekee kufanya jukumu hilo bila kujali sheria nyingine zozote za nchi hii.

Pia wanaeleza kuwa DPP amepewa majukumu ya kikatiba na kisheria kuratibu na kusimamia upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai kasoro makosa yanayohusu mahakama ya kijeshi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *