
Idadi kubwa ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameonyesha kutokuridhishwa kwao na kuongezeka kwa mashambulizi ya kijeshi ya Israel dhidi ya Lebanon. Wakati hayo yakijiri, Marekani imepuuza kuukosoa utawala wa Israel, badala yake ikielekeza lawama zake zote kwa harakati ya Muqawama ya Hizbullah na nchi ya Iran.
Jerome Bonnafont, Balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, alieleza Jumatatu jioni kuwa waliomba kikao cha dharura “ili kushughulikia ongezeko kubwa la uhasama linaloshuhudiwa sasa na kushadidi kwa operesheni za kijeshi za Israel nchini Lebanon, licha ya kuwepo kwa makubaliano ya kusitisha mapambano yaliyoanza Aprili 17.”
Bonnafont ameonya kuwa uvamizi mpya utachochea zaidi mzozo huo, akisema: “Badala ya kuleta usalama kwa Israel na watu wake, uvamizi mpya una uwezekano wa kuongeza ukosefu wa utulivu, kwani kila kijiji kinachopigwa mabomu na kila raia anayeuawa kunadhoofisha mamlaka ya serikali ya Lebanon.”
Mwakilishi wa Russia katika Umoja wa Mataifa, Vassily Nebenzia, amelinganisha operesheni za kijeshi za Israel nchini Lebanon na zile zinazotokea katika Ukanda wa Gaza. Amesema Lebanon inashuhudia “marudio yaliyo karibu kufanana kabisa na mkakati wa kufuta maeneo ya Gaza kupitia kuanzisha udhibiti mkubwa wa kikoloni na kuwahamisha raia kwa lazima.”
Nebenzia ametoa wito wa kuondolewa mara moja kwa wanajeshi wa Israel, akionya kuwa bila hatua hiyo, “itakuwa muhali kufikia usitishaji vita wa kweli.” Pia amehusisha mgogoro wa Lebanon na masuala mapana ya kikanda, akisisitiza kuwa “kuzorota kwa hali nchini Lebanon ni matokeo ya moja kwa moja ya vita haramu vya Marekani na Israel dhidi ya Iran.”
Naye Balozi wa China katika Umoja wa Mataifa, Fu Cong, amesema kuwa Israel “imevuka Mto Litani na kuteka Ngome ya Belfort .” Ameitaja hatua hiyo kama “uvamizi mkubwa zaidi wa kijeshi wa Israel nchini Lebanon katika kipindi cha zaidi ya miaka 20,” akisisitiza kuwa nia ya Israel ya kuongeza mashambulizi ya nchi kavu “inatia wasiwasi mkubwa jumuiya ya kimataifa.”
Naye James Kariuki, Kaimu Balozi wa Uingereza, amekosoa kile alichokiita “ongezeko la kiholela na lisilo na uwiano la mashambulizi ya kijeshi ya Israel,” akibainisha kuwa hatua hiyo “imeongeza madhara katika mazingira ambayo tayari ni ya kikatili kwa raia wa Lebanon.”
Hata hivyo, mjumbe wa Marekani, Mike Waltz, aliwasilisha mtazamo tofauti kabisa, akisifu uongozi wa moja kwa moja wa Rais Donald Trump huku akitupia lawama zote kwa Hizbullah na Iran, bila kukiri ukiukaji wowote uliofanywa na Israel.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Lebanon, tangu tarehe 2 Machi, zaidi ya watu 3,400 wamepoteza maisha kutokana na mashambulizi ya Israel nchini kote.