
Waziri wa Vita wa Marekani amesema katika mkutano wa Shangri-La huko Singapore kwamba Washington inatarajia washirika wake wa Asia waongeze matumizi yao ya kijeshi na ulinzi hadi asilimia 3.5 ya Pato lao la Taifa.
Ikiwa ni wiki chache tu zimepita tangu kufanyika mkutano wa marais wa Marekani na China mjini Beijing, Waziri wa Vita wa Marekani amewataka washirika wa nchi hiyo wa bara Asia kuongeza matumizi yao ya ulinzi katika mkutano wa Singapore.
Siku ya Jumamosi, Mei 30, katika mkutano wa usalama wa Shangri-La nchini Singapore, Pete Hegseth Waziri wa Vita wa Marekani alidai kuwa kuna wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la kihistoria la China katika nguvu za kijeshi na kupanuka shughuli zake za kijeshi katika eneo hilo na kwingineko. Aliongeza kuwa udhibiti na ongezeko la nguvu yoyote katika Bahari ya Pasifiki utavuruga uwiano wa nguvu katika eneo. Hegseth pia alikariri msimamo wa Rais Donald Trump wa Marekani kuwa nchi hiyo haiko tayari kugharamia ulinzi wa nchi tajiri peke yake, na kusisitiza kuwa Marekani inataka mshirika, na sio mtu aliye chini ya himaya yake.
Matamshi haya yanaweza kukosolewa kwa pande kadhaa. Kwanza, licha ya pongezi za kidiplomasia za maafisa wakuu wa Marekani kwa wenzao wa China, hasa wakati wa ziara ya Rais Trump mjini Beijing na mkutano na Rais Xi Jinping wa China, Marekani bado inajaribu kuimarisha msimamo wake wa kichochezi katika eneo la Asia-Pacific kwa kuituhumu China kuwa ni tishio. Kwa mtazamo wa Wamarekani, kadiri nchi za eneo zinavyotishika kuhusu China, ndivyo zitakavyotoa pesa nyingi kwa Wamarekani ili kudhamini usalama wao. Kwa sababu hiyo, Marekani bado haiioni China kama mshirika wake wa kimkakati, bali ni tishio la hivi sasa kwa maslahi ya Marekani na washirika wake, ambapo washirika hao wanatakiwa kuongeza bajeti zao za ulinzi kadiri inavyowezekana.
Kwa kutilia maanani mtazamo huu, unafuata ukosolewaji wa pili kuhusu matamshi ya Waziri wa Vita wa Marekani, nao ni kwamba nchi hii inadai kuwa inataka kuzuia uundwaji wa nguvu ya kibabe katika eneo la Asia-Pacifiki, wakati yenyewe imekuwa na nafasi na msimamo huo huo kwa miongo kadhaa. Kwa maneno mengine, Marekani haina tatizo na suala la uwepo wa nguvu kubwa katika kanda hiyo, bali wasiwasi wake ni kudhihiri nguvu mpya itakayotoa changamoto kwa nafasi yake ya kibabe katika eneo hilo muhimu duniani.
Marekani, kinyume na madai ya waziri wake wa sasa wa vita, inataka nchi za eneo hilo ziendelee kuwa chini ya himaya yake, tofauti ya pekee mara hii ikiwa ni kwamba nchi hizo zinatakiwa kugharamia ulinzi wao zenyewe, na sio walipa kodi wa Marekani. Kwa sababu hii, Washington inajaribu kwa nguvu zake zote kuzuia serikali huru za eneo hilo kupata nguvu na kuunda miungano ya kikanda isiyoongozwa na Washington.
Kwa mujibu wa wataalamu wa mikakati wa Marekani, tofauti pekee iliyopo kati ya hali ya zamani na ya hivi sasa ni kwamba washirika wa Marekani wanapaswa kulipia gharama ya kudumishwa nguvu za Marekani katika ngazi ya kimataifa kwa sababu uchumi wa nchi hiyo hauwezi tena kubeba mzigo wa kuendelezwa himaya ya kimataifa ya Marekani. Kwa hivyo, iwe ni katika Asia Mashariki, Asia Magharibi, au Ulaya ya Mashariki na ya Magharibi, nchi tajiri zinazofungamana na Marekani sasa zitalazimika kutia mikono mifukoni na kulipia utashi na mipango ya kijeshi ya Marekani kwa madhara ya ustawi wa raia wao.
Kwa maneno mengine, nchi ambayo ina deni la karibu dola trilioni arubaini na baadhi ya mipango yake ya ustawi na kijamii imevurugika kutokana na ukosefu wa rasilimali za kifedha, inazikodolea macho fedha na utajiri wa nchi nyingine ili kuzinyang’anya fedha na mali zao kwa kisingizio cha hatari bandia ya China, Russia au Iran.
Ni kwa sababu hiyo, ndio maana kwa upande mmoja, Marekani inaendelea kubuni maadui bandia katika kila pembe ya dunia, na kwa upande mwingine, kuwashinikiza washirika wake waongeze bajeti zao za kijeshi kadiri inavyowezekana. Bajeti ambazo iwapo zitaongezwa, zitaibua mafuriko ya madai ya ulinzi na usalama kutoka kwa makampuni ya Marekani, ambapo faida za madai hayo hatimaye zitaishia kwenye mifuko ya makampuni na uchumi wa Marekani.