Zikiwa zimebaki siku tisa kabla ya Fainali za Kombe la Dunia 2026 zitakazofanyika Marekani, Canada na Mexico, kwa mara ya kwanza itashuhudiwa mabadiliko kadhaa katika mashindano hayo makubwa duniani, ikiwemo mpira utakaotumika kutakiwa kuchajiwa kabla ya mechi kutokana na kuwa na kifaa maalumu cha kielektroniki kinachofanya kazi muda wote wa mchezo.
Mpira huo umepewa jina la TRIONDA linalotokana na maneno mawili, ‘Tri’ ikimaanisha tatu na ‘Onda’, neno la Kihispania linalomaanisha mawimbi ambapo kwa pamoja jina hilo lina maana ya ‘Mawimbi Matatu’ yaani ushirikiano wa Mataifa matatu ambayo ni Marekani, Canada na Mexico yanayoandaa mashindano hayo mwaka huu , ikiwa ni mara ya kwanza kwa mashindano hayo kuandaliwa na nchi tatu kwa pamoja.
Mpira huo umepambwa kwa rangi nyekundu, bluu na kijani pamoja na alama maalumu zinazowakilisha nchi hizo tatu, zikiwamo jani la maple kwa Canada, tai kwa Mexico na nyota kwa Marekani.
Kinachoufanya mpira wa TRIONDA kuwa wa kipekee zaidi ni uwepo wa sensa maalumu yenye uzito wa gramu 14 iliyowekwa ndani.
Sensa hiyo ina uwezo wa kurekodi kila mguso wa mchezaji, kasi ya mpira, mzunguko wake na mwelekeo wake kwa usahihi.
Taarifa hizo hutumwa na kuunganishwa na mfumo wa VAR ili kufanya maamuzi ya haraka na sahihi zaidi katika matukio ya kuotea, mipira ya kushika, mipira iliyovuka mstari wa goli pamoja na matukio mengine yenye utata.
Mpira huo uliotengenezwa na kampuni ya vifaa vya michezo ya Adidas hutumia betri ndogo inayoweza kuchajiwa upya.
Hivyo, kabla ya kila mechi, waandaaji hulazimika kuuchaji kikamilifu ili kuhakikisha teknolojia yake inafanya kazi bila hitilafu.
Kwa mujibu wa FIFA, betri ya mpira huo inaweza kudumu kwa takribani saa sita baada ya kuchajiwa, muda unaotosha kumaliza dakika 90 za kawaida, muda wa ziada na hata mikwaju ya penalti endapo mechi itafikia hatua hiyo.
Teknolojia hiyo imeufanya mpira wa TRIONDA kuwa miongoni mwa mipira ghali zaidi kuwahi kutengenezwa kwa ajili ya Kombe la Dunia.
Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa mpira mmoja unauzwa kwa Dola 175 (Sh446,249).