
Dar es Salaam. Utafiti mpya wa kisayansi umeibua mjadala kuhusu usalama wa matumizi ya sigara za kielektroniki (vaping), baada ya kubaini matumizi ya kawaida ya vifaa hivyo yanaweza kusababisha mabadiliko katika zaidi ya vinasaba 3,000 vinavyohusishwa na magonjwa hatarishi kama saratani, magonjwa ya moyo na matatizo ya mapafu.
Kwa mujibu wa gazeti la Dailymail la nchini Uingereza, utafiti huo uliochapishwa katika jarida la kisayansi la Frontiers in Oncology, umefanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Southern California, ambapo walilinganisha sampuli za watu 83 wakiwemo wavutaji sigara, watumiaji wa vape na wasiovuta kabisa.
Matokeo yanaonyesha watu wanaotumia sigara hizo walionekana kuwa na mabadiliko ya utendaji wa katika vinasaba 3,124 hali inayomaanisha kuwa baadhi ya jeni zilikuwa zikifanya kazi kwa namna inayoweza kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali.
Watafiti wanasema mabadiliko haya hayathibitishi moja kwa moja kuwa sigara za kielektroniki husababisha magonjwa, lakini ni ishara ya awali ya mabadiliko ya kibaiolojia yanayoweza kuleta madhara ya muda mrefu.
Mmoja wa watafiti wakuu, Profesa Ahmad Besaratinia amesema bado haijajulikana kama athari hizo zinatokana na uvutaji wenyewe au aina ya vifaa na viambato vinavyotumika.
Wakati utafiti huo ukitolewa, nchini Tanzania matumizi ya sigara za kielektroniki yanazidi kuenea miongoni mwa vijana, huku wataalamu wa afya wakionya kuwa tabia hiyo itaongeza mzigo wa saratani na magonjwa mengine yasiyoambukiza ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Hospitali ya Aga Khan, Dk Harrison Chuwa amesema matumizi ya tumbaku yanaendelea kuwa miongoni mwa visababishi vikuu vya saratani, huku takribani asilimia 30 magonjwa ya saratani yakihusishwa moja kwa moja na matumizi ya bidhaa za tumbaku.
“Karibu saratani zote zina uhusiano kwa namna moja au nyingine na matumizi ya tumbaku, lakini saratani za kichwa na shingo ndizo zinazoonekana zaidi kuhusishwa na uvutaji sigara,” amesema Dk Chuwa.
Takwimu zilizotolewa leo na Shirika la Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha takribani vijana milioni 15 wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 15 duniani tayari wanatumia sigara za kielektroniki (e-cigarettes), huku vijana milioni 40 wa kundi hilo la umri wakitumia bidhaa za tumbaku.
Ladha na vifaa vya kisasa
Utafiti huo umebaini kuwa karibu theluthi mbili ya mabadiliko hayo ya vinasaba yalihusiana na aina ya ladha na kifaa kinachotumika, si tu kiwango cha matumizi.
Ladha za matunda zilionekana kuhusishwa zaidi na mabadiliko hayo, zikihusika na takriban asilimia 31 ya mabadiliko yaliyochunguzwa. Watumiaji wanaochanganya ladha mbalimbali walionekana kuathiriwa zaidi, hadi kufikia asilimia 64.3 ya mabadiliko.
Kwa upande mwingine, ladha tamu zilihusishwa na asilimia 2.9 huku menthol au mint zikiwa na athari ndogo zaidi ya asilimia 0.9.
Aidha, vifaa vya kisasa vinavyojulikana kama “mods” ambavyo huruhusu mtumiaji kubadilisha nguvu na joto la mvuke, vilionekana kuhusishwa na mabadiliko makubwa zaidi ya kinasaba.
Uchambuzi zaidi wa watafiti umeonesha kuwa mabadiliko hayo ya vinasaba yanahusishwa zaidi na njia za kibaiolojia zinazohusiana na saratani, kisha magonjwa ya mfumo wa homoni, mfumo wa mmeng’enyo wa chakula na hata magonjwa ya neva.
Watafiti wanasema seli zilizochukuliwa kutoka ndani ya mashavu ya washiriki zilionyesha tofauti kubwa za utendaji wa vinasaba kati ya watumiaji wa vape na wasiotumia, ikionyesha uwezekano wa athari zisizotabirika za kiafya.
Wataalamu waonya
Ingawa tafiti nyingi zinaonyesha kuwa sigara za kielektroniki zinaweza kuwa na madhara kidogo ukilinganisha na uvutaji wa sigara za kawaida, wataalamu wanasisitiza kuwa si salama.
Sigara za kielektroniki zina kemikali kama ‘formaldehyde’ ambazo zinaweza kusababisha uvimbe na mabadiliko ya seli zinazoweza kuchangia magonjwa ya muda mrefu.
Hata hivyo, watafiti wanasema utafiti huu bado ni wa kiwango cha awali na hauwezi kutumika kuthibitisha moja kwa moja uhusiano wa kisababishi kati ya sigara za kielektroniki na magonjwa hayo.
Wito kwa wadhibiti na watengenezaji
Watafiti hao wameitaka mamlaka za udhibiti wa bidhaa za tumbaku kuzingatia kwa makini aina za ladha na viambato vinavyotumika kwenye bidhaa hizo, kwa kuwa baadhi zinaonekana kuwa na athari kubwa zaidi za kibailojia kuliko nyingine.
“Lengo ni kutambua kemikali zinazohusika ili ziweze kupunguzwa au kuondolewa kabisa,” amesema Profesa Besaratinia.
Wakati mjadala huo ukiendelea, wataalamu wa afya wanasema uvutaji wa sigara za kawaida bado unaongoza kwa kusababisha vifo vinavyoweza kuzuilika, lakini wanaonya kuwa sigara za kielektroniki pia inaweza kuwa na mchango katika mzigo wa magonjwa ya muda mrefu iwapo haitadhibitiwa ipasavyo.