Dar es Salaam. Wakazi wawili jijini Dar es Salaam wenye uhusiano wa kifamilia, wamehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroini huku mama mzazi wa mmoja wa washitakiwa akiachiwa huru.

Hata hivyo, Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala ya Dar es Salaam chini ya Jaji Sedekia Kisanya, imeamuru Sh873,000 alizokamatwa nazo mshitakiwa namba 2 na 3 warejeshewe.

Aliyekuwa mshitakiwa wa pili, Sharifa Seleman Bakari ambaye aliachiwa huru na mahakama kwa kukosekana ushahidi dhidi yake ni mama mzazi wa mshitakiwa wa tatu, Farid Said na shangazi wa mshitakiwa wa kwanza, Suleiman Ngulangwa.

Sh375,000 alikutwa nazo mshitakiwa wa pili na Sh500,000 alikutwa nazo mshitakiwa wa tatu ambaye alikuwa ni mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) akisomea stashahada ya uhandisi wa umeme na mawasiliano.

Katika hukumu yake aliyoitoa jana Jumatatu Juni 1,2026 na nakala ya hukumu yake kuwekwa katika tovuti ya Mahakama leo Jumanne, Juni 2,2026, Jaji Kisanya alisema hakuna ushahidi mahususi uliotolewa, kuthibitisha kuwa fedha hizo ni zao la uhalifu.

Awali, wote watatu walidaiwa kuwa mnano Novemba 30,2022, huko maeneo ya Shule ya Sekondari Charambe, Wilaya ya Temeke Mkoa wa Dar es Salaam, walikamatwa na dawa za kulevya aina ya heroini yenye uzito wa kilo 15.19.

Washitakiwa walikanusha mashitaka hayo na kuufanya upande wa mashitaka kuita mashahidi saba na kuwasilisha vielelezo tisa lakini mwisho wa shauri hilo, Jaji Kisanya aliwatia hatiani mshitakiwa wa kwanza na wa tatu na kumwachia huru Sharifa.

Namna walivyokamatwa

Ushahidi wa Jamhuri unaeleza Novemba 27,2022 saa 2:00 usiku, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Hassan Msangi aliyekuwa shahidi wa tano, alipokea taarifa fiche kuna mtu anafanya biashara ya dawa za kulevya katika mgahawa wa Utamu.

Mgahawa huo upo barabara ya Ufipa Wilaya ya Kinondoni, na baada ya kupokea taarifa hiyo, ASP Msangi alimjulisha mkuu wake wa kazi ambaye alimwagiza moja kwa moja katika eneo hilo na kumkamata mshukiwa huyo wa dawa za kulevya.

Aliwakusanya makachero wenzake na kuelekea eneo waliloelekezwa ambapo walikutana na mtoa taarifa wao ambaye aliwaelekeza maofisa hao kwa kunyoosha kidole eneo alipo mshukiwa ambaye ni mshitakiwa wa kwanza, Ngulangwa.

Walifanikiwa kumkamata mshitakiwa na kumtaka asogee pembeni ili waweze kufanya mahojiano ya awali ingawa alitii amri hiyo, lakini ghafla alijaribu kuwatoroka maofisa,  alikamatwa na kurejeshwa eneo hilo.

ASP Msangi akatafuta shahidi huru (independent witness), Mohamed Maalim ambaye ni meneja wa mgahawa wa Utamu na katika upekuzi walimkuta na vitu mbalimbali ikiwamo Sh5 milioni, kadi ya gari, gari na simu mbili za kiganjani.

Upekuzi wa awali ulifanyika na upekuzi makini ulifanyika ofisi za DCEA (Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya).

Novemba 29,2022, Inspekta Wamba Msafiri aliyekuwa shahidi namba mbili, alikabidhiwa jukumu la kumsindikiza mshitakiwa wa kwanza katika nyumba iliyopo karibu na Shule ya Sekondari ya Charambe ambayo alikiri ndipo alipotunza dawa hizo.

Baada ya kufika katika nyumba hiyo akiwa na maofisa wengine kutoka DCEA,  walifanya upekuzi katika nyumba hiyo na kupata mfuko wa sulphate ukiwa na pakti 16 zilizodhaniwa ni dawa za kulevya.

Katika upekuzi huo walifanikiwa pia kupata Sh500,000 katika chumba cha mshitakiwa wa tatu, huku vifungashio viwili vikikutwa na unga uliodhaniwa ni dawa za kulevya na Sh373,000 zilipatikana katika chumba cha mshitakiwa wa pili.

Baadaye Novemba 30,2022, pakti zile 16 na vifungashio vingine viwili vilipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kuthibitika zilikuwa ni dawa aina ya heroini.

Walivyojitetea kortini

Katika utetezi wake, mshitakiwa wa kwanza, alijitetea kuwa yeye ni wakala (broker) wa kuuza magari na kukanusha kufanya biashara ya dawa za kulevya.

Alieleza kuwa alikamatwa Novemba 27,2022 katika mgahawa wa Utamu huko Kinondoni kwa kushukiwa kuwa mwizi wa gari na katika upekuzi mbele ya shahidi huru, alipatikana na fedha taslimu, gari pamoja na vitu mbalimbali.

Aliendelea kueleza kuwa ukaguzi haukufanyikia katika ofisi za DCEA kama mashahidi wa Jamhuri walivyodai bali ni katika eneo alilokamatiwa na baada ya kusaini kielelezo D3, alizibwa uso na kupelekwa mahabusu hadi Desemba 17,2022.

Mshitakiwa alikanusha kwenda pamoja na shahidi namba mbili hadi eneo la Mbagala Novemba 29 au 30,2022 na pia akakanusha kujihusisha au kufahamu lolote kuhusiana na dawa za kulevya aina ya heroini zinazodaiwa kupatikana.

Kwa upande wake, mshitakiwa wa pili, Sharifa,aliiambia mahakama kuwa yeye ni mfanyabiashara mdogo akiuza juice, halua, keki, maandazi na maji na kwamba kuanzia Novemba 9 hadi 29,2022 alikuwa akimuuguza mama yake huko Mbande.

Mshitakiwa huyo alieleza kuwa alirudi nyumbani Mbagala Maji Matitu saa 4:30 usiku wa Novemba 29,2022 na kukuta hakuna umeme na baada ya kuoga alikwenda kulala chumbani kwake ambacho hakuna mlango bali pazia pekee.

Alieleza kuwa wakati amelala, aliamshwa na kundi la maofisa wa Polisi walioingia katika chumba chake na alishtuka akidhani walikuwa ni wahalifu.

Maofisa hao walimwamrisha avae nguo na kwenda kwenye kibaraza (corridor) ambako aliona mfuko na beseni vikiwa tayari chini ya usimamizi wa maofisa hao na alimuona pia mshitakiwa wa kwanza, kiongozi wa Serikali ya mtaa.

Alieleza kuwa anakumbuka kuweka dole gumba kwenye nyaraka akiwa pale kibarazani lakini hakufahamu maudhui yake wala kujua nani aliisaini.

Utetezi wa mwanafunzi DIT

Kwa upande wake, mshitakiwa wa tatu, Farid Said, alisema yeye ni mwanafunzi wa Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) akisomea stashahada ya uhandisi wa umeme na mawasiliano na alijiunga na chuo hicho mwaka 2018.

Alieleza alikuwa akiishi katika hosteli za DIT hususan Block 3 chumba namba 108 na alikuwa akifadhiliwa masomo yake hayo na Serikali na alitoa fomu ya maombi ya hosteli kuthibitisha madai yake kuwa alikuwa akiishi hosteli za DIT.

Ni utetezi wake kuwa siku nzima ya Novemba 29,2022  alikuwa katika hosteli hizo za DIT akiwa na rafiki yake aitwaye Yahaya na waliachana saa 9 au 10 alasiri na baadaye alienda nyumbani kwao Mbagala Maji Matitu na kufika saa 2 au 3 usiku.

Alidai usiku, walifika polisi na kufanya upekuzi na yeye aliamshwa kutoka usingizini na kuwakuta maofisa hao wakiwa kibarazani ambapo walimuonyesha beseni na mfuko, vitu ambavyo alikana kuwa na ufahamu navyo.

Katika upekuzi ndani ya chumba alichokuwa amelala, polisi walikuta nyaraka za chuo, vitambulisho na Sh500,000 na kukana kufahamu juu ya dawa za kulevya na kusisitiza yeye ni mwanafunzi na mchana wote alikuwa hosteli za DIT.

Hukumu ya Jaji ilivyokuwa

Katika hukumu yake aliyoitoa Juni 1,2026, Jaji Kisanya alisema anakubaliana na wakili wa Serikali kwamba upande wa mashitaka umeweza kuthibitisha kuwa kielelezo PE3 ni dawa za kulevya aina ya heroini zenye uzito wa kilo 15.19.

Baada ya kuthibitisha hivyo, Jaji alisema swali lililohitaji majibu ni kama washitakiwa ndio waliopatikanana kielelezo hicho ama la hasa ikizingatiwa kuwa kukutwa na dawa hizo ni moja ya makosa ya kusafirisha dawa za kulevya.

Jaji alisema shahidi namba mbili aliiambia mahakama ni mshitakiwa wa kwanza ndiye aliyewapeleka Charambe ambako dawa hizo zilipatikana.

Shahidi huyo aliendelea kueleza walipomgongea mshitakiwa wa tatu na kumuuliza kama aliwahi kumuona mshitakiwa wa kwanza akiwa na mfuko wa suplhate, aliwaeleza kuwa amewahi kumuona akiwa amebeba mfuko huo.

Baada ya mfuko huo kutolewa ukiwa katika beseni na mshitakiwa wa tatu kuulizwa nini kilikuwepo ndani ya mfuko huo, mshitakiwa huyo wa tatu aliwaambia kuwa kuna pakti 16 za heroini zilizoletwa na mshitakiwa namba moja.

Kwa kuegemea ushahidi huo na ushahidi mwingine kwa ujumla wake, kwamba pakti hizo zilipatikana katika mfuko huo wa sulphate, nanashawishika kuwa mshitakiwa namba moja na tatu walikuwa na ufahamu juu ya dawa hizo za kulevya.

Kuhusiana na mshitakiwa wa pili, Sharifa Bakari, Jaji alisema hakuona ushahidi unaomuunganisha kuwa alifahamu uwepo wa kielelezo PE3 wala hakuna ushahidi wowote kuonyesha kuwa kilipelekwa nyumbani hapo kwa maelekezo yake.

“Kwa kuhitimisha, suala dogo la pili la iwapo washtakiwa walikutwa na kielelezo PE3 linajibiwa kwa uthibitisho (affirmative) dhidi ya mshitakiwa wa kwanza na wa tatu, na kwa upande hasi (negative) kwa mshitakiwa wa pili,”alisema Jaji.

Jaji alisema pamoja na maombolezo ya washitakiwa namba moja na tatu baada ya kutiwa hatiani, mahakama hii inafungwa mikono na sheria ambayo imeweka adhabu ya kifungo cha maisha kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya.”alisema.

Baada ya hukumu hiyo, Jaji aliamuru pia dawa hizo zitekelezwe kwa mujibu wa sheria huku akiutaka upande wa Jamhuri kufuata sheria ya kutaifisha mali zinazothibitika ni zao la uhalifu, na wakishindwa basi zirejeshwe kwa washitakiwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *