Dar es Salaam. Benki ya Absa Tanzania imepongeza mafanikio makubwa ya mashindano ya Tanzania Pickleball Open 2026 yaliyovunja rekodi ya ushiriki wa wachezaji wa kimataifa, huku yakichangia kuimarisha azma ya Tanzania ya kuwa kitovu cha michezo na utalii wa michezo katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Mashindano hayo ya siku tano yaliyofanyika katika viwanja vya Gymkhana Club jijini Dar es Salaam, yamewakutanisha wachezaji kutoka zaidi ya nchi saba, zikiwamo Kenya, Uganda, Rwanda, Afrika Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), India, Uturuki na Falme za Kiarabu.
Michuano hiyo, iliyoandaliwa kwa ushirikiano kati ya Chama cha Pickleball Tanzania (TPA) na East Africa Racket Sports Club (EARSC), imehusisha zawadi na vifaa vya michezo vyenye thamani ya dola za Marekani 15,000, jambo lililovutia washiriki wa kimataifa na mashabiki wengi wa mchezo huo.
Kama mdhamini mkuu wa mashindano hayo, Benki ya Absa Tanzania imesema ushiriki wake unaendana na dhamira yake ya kuendeleza vijana, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kukuza michezo inayoibukia nchini.
Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa wa Benki ya Absa Tanzania, Christopher Mgani (kushoto), akikabidhi zawadi kwa baadhi ya washindi wa Tanzania Pickleball Open 2026 wakati wa hafla ya ufungaji rasmi wa mashindano hayo yaliyodumu kwa siku tano na kudhaminiwa na benki hiyo katika Viwanja vya Klabu ya Gymkhana, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mashindano hayo, Meneja wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Beda Biswalo amesema mafanikio ya michuano hiyo yanaonesha uwezo mkubwa wa mchezo wa pickleball katika kuunganisha jamii na kufungua fursa mbalimbali kwa vijana.
“Tumevutiwa na kiwango cha ushindani, nidhamu na vipaji vilivyooneshwa na washiriki kutoka mataifa mbalimbali. Ushirikiano wetu unalenga kusaidia ukuaji wa mchezo huu pamoja na kuwapatia vijana fursa za maendeleo kupitia michezo,” amesema Biswalo.
Amewahimiza Watanzania, hususan vijana kuupokea mchezo huo kutokana na manufaa yake katika afya, burudani na maendeleo ya kitaaluma.
Kwa mujibu wa wadau wa michezo, ukuaji wa kasi wa pickleball unaendelea kufungua fursa mpya kwa wanamichezo kupitia mashindano ya kimataifa, ufadhili wa masomo na ushiriki katika ligi mbalimbali za kitaalamu duniani.
Aidha, urahisi wa kuucheza pamoja na gharama nafuu umechangia kuongezeka kwa umaarufu wake miongoni mwa watu wa rika tofauti.
Mafanikio ya Tanzania Pickleball Open 2026 yanaendana na juhudi za Tanzania za kuimarisha sekta ya michezo kama nyenzo ya kukuza uchumi na utalii.
Kupitia ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, Tanzania imeendelea kuwa mwenyeji wa mashindano ya kikanda na kimataifa yanayochangia kuitangaza nchi kimataifa.
Biswalo amesema uwekezaji wa Absa katika mashindano hayo unaunga mkono juhudi za Serikali za kuendeleza miundombinu ya michezo, kukuza vipaji vya ndani na kuifanya michezo kuwa kichocheo cha shughuli za kiuchumi.
“Mpango huu pia unaendana na jitihada za Baraza la Michezo la Taifa (BMT) za kupanua fursa kwa wanamichezo na mashirika ya michezo nchini,” amesema.
Benki hiyo imetoa shukrani kwa Serikali ya Tanzania, wadhamini wenza wa mashindano hayo, waandaaji, washirika wa teknolojia na mashabiki kwa mchango wao uliofanikisha kufanyika kwa michuano hiyo.
Baada ya mafanikio ya mwaka huu, Absa Tanzania imeahidi kuendelea kuunga mkono maendeleo ya mchezo wa pickleball nchini kwa lengo la kuvutia ushiriki mkubwa zaidi wa kimataifa, kukuza vipaji vya vijana wa Kitanzania na kuimarisha hadhi ya Tanzania katika medani za michezo duniani.
Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Tanzania Pickleball na Mkurugenzi wa East Africa Racket Sports Club, Kartik Kapor amesema mafanikio ya Tanzania Pickleball Open 2026 yanaashiria hatua muhimu katika safari ya kuifanya Tanzania kuwa moja ya mataifa yanayoongoza katika mchezo huo duniani.
Katika matokeo ya mashindano hayo, Rakshika na Agni wametwaa ubingwa wa wanawake wawili wawili, huku Sally na Rinaaz wakishika nafasi ya pili na Edna pamoja na Ester wakimaliza katika nafasi ya tatu.
Kwa upande wa wanaume wawili wawili, Yuvraj na Purvansh wameshika nafasi ya kwanza wakifuatiwa na Fifi na Shane katika nafasi ya pili, huku Kartik na Dev wakimaliza katika nafasi ya tatu.
Katika mashindano ya wanaume mmoja mmoja, Purvansh ametwaa ubingwa, akifuatiwa na Fifi katika nafasi ya pili na Dev katika nafasi ya tatu.
Kwa upande wa mchanganyiko wa kimataifa, Shaheed na Deandra wameshinda taji hilo, huku Ahmad na Zainab wakishika nafasi ya pili na Lisa pamoja na Zuber wakimaliza wa tatu.
Kwa upande wa wanawake mmoja mmoja, Agni ametwaa ubingwa, Tamara akishika nafasi ya pili na Sally nafasi ya tatu.
Nayo michuano ya mchanganyiko imeshuhudia Rakshika na Dev wakimaliza katika nafasi ya kwanza, wakifuatiwa na Alikhan na Sally, huku Yuvraj na Agni wakishika nafasi ya tatu.