Arusha. Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rebecca Kadaga amewasilisha katika Bunge la Afrika Mashariki (Eala) mapendekezo ya bajeti ya jumuiya hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27, ambayo ni jumla ya Dola za Marekani 110.9 milioni (Sh291 bilioni).

Kikao hicho kilichofanyika Juni Mosi, 2026 kwa njia ya mtandao, kilipitisha makadirio ya bajeti yaliyopendekezwa ya mwaka wa fedha 2026/27 na kuyawasilisha kwa kamati maalumu ya Bunge ili yakaguliwe.

Makadirio hayo ya bajeti yalithibitishwa katika mkutano maalumu wa 60 wa Baraza la Mawaziri uliofanyika kuanzia Mei 18 hadi 22, 2026 ambapo walipitisha jumla ya bajeti ya dola 110.9 milioni pamoja na bajeti ya nyongeza ya dola 4.8 milioni (Sh12.5 bilioni) kwa mwaka wa fedha wa 2025/26.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Ofisa Habari Mwandamizi wa Eala, Nicodemus Bior, mapendekezo ya bajeti ya EAC ya mwaka wa fedha 2026/27 yanaonyesha dhamira thabiti ya kuendeleza utendaji na programu za mihimili pamoja na taasisi za jumuiya hiyo.

Bajeti inayopendekezwa kwa mwaka wa fedha 2026/27 imetengwa kwa mihimili na taasisi zake kwa mgawanyo wake ambao sekretarieti ya EAC imetengewa dola 59.7 milioni (Sh156 bilioni).

Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki imetengewa dola 5 milioni (13.1 bilioni) huku Bunge la Afrika Mashariki (Eala) dola 19.2 milioni (Sh50.3 bilioni).

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Stephen Mbundi akihutubia kikao maalumu cha Bunge la Afrika Mashariki kilichofanyika jijini Arusha jana.

Kuhusu mgawanyo kwenye taasisi za EAC ambazo zipo kwenye nchi wanachama Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (IUCEA), imetengewa dola 9.3 milioni (Sh24.4 milioni), Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria dola 7 milioni (Sh18.3 milioni), Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki kiasi cha dola 2.7 milioni (Sh7 bilioni).

Pia taasisi nyingine ni Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria dola 2.2 milioni (Sh5.7 bilioni), Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yenye makao yake visiwani Zanzibar dola 1.6 milioni (Sh4.1 bilioni) na Kamisheni ya Utafiti wa Afya ya Afrika Mashariki iliyopo nchini Burundi dola 2.3 milioni (Sh6 bilioni).

Taarifa hiyo imebainisha kwamba vyanzo vya bajeti hiyo utatokana hasa na michango kutoka nchi wanachama inayofikia dola 62.77 milioni (Sh177.7 bilioni) huku dola 46 milioni (Sh120 bilioni) kitachangiwa na washirika wa maendeleo na mapato mengine yanatarajiwa kutoka kwenye akiba za kitaasisi na vyanzo vingine vya mapato.

“Mbali na bajeti kuu, Baraza lilipitisha bajeti ya nyongeza ya mwaka wa fedha 2025/26 ya dola 4.79 milioni (Sh12.3 bilioni) ili kushughulikia vipaumbele vinavyoibuka na mapengo ya kifedha ambayo yasingeweza kuahirishwa. Mgawo huu wa nyongeza unaongezeka juu ya bajeti ya mwaka 2025/26 iliyopitishwa awali ya takribani dola 109 milioni (Sh286 bilioni) na unalenga kuhakikisha uendelevu na ufanisi katika utekelezaji wa programu na miradi muhimu,” imeeleza taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Eala, fedha hizo za nyongeza zimetengwa kwa ajili ya taasisi zilizoteuliwa ambapo sekretarieti ya EAC itapokea fungu la dola 2.31 milioni (Sh6 bilioni) ikifuatiwa na Shirika la Uvuvi la Ziwa Victoria, Kamisheni ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika Mashariki na Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria.

“Fedha hizi zitatolewa kwa kiasi kikubwa kutoka kwenye ruzuku za washirika wa maendeleo, akiba za kitaasisi, na michango maalumu ikionyesha mfumo rahisi wa kifedha ulioundwa ili kuitikia mahitaji ya haraka na changamoto zinazoibuka,” imeeleza taarifa hiyo.

Bajeti hiyo imetoa vipaumbele vya afua zenye athari kubwa kwamba zitaungwa mkono chini ya bajeti ya nyongeza. Afua hizo ni pamoja na mipango inayolenga kuimarisha kujiandaa na majanga ya milipuko, kuendeleza programu za afya ya uzazi, kuimarisha uwezo wa utawala bora na ujenzi wa amani na kuboresha miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ndani ya taasisi za EAC.

Kiasi kingine cha fedha kitaenda kwenye miradi ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika Bonde la Ziwa Victoria, usimamizi wa uvuvi na programu za usalama wa chakula, pamoja na mipango ya kukuza uvumbuzi haswa miongoni mwa wanawake na vijana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *