Tanga. Katibu Mkuu wa Chama cha National League for Democracy (NLD), Doyo Hassan Doyo, amewataka wanasiasa kuendelea kuelekeza nguvu zao katika kushughulikia changamoto za wananchi na kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, badala ya kuanza mijadala ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2030 mapema.

Doyo alitoa kauli hiyo jana Juni 2,2026 jijini Tanga alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuhitimisha ziara yake ya kichama mkoani humo.

Akizungumza katika mkutano huo, Doyo, ambaye pia aliwahi kugombea urais kupitia NLD katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, alisema baadhi ya kauli zinazotolewa na wanasiasa katika majukwaa mbalimbali zimeibua mjadala kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2030.

Alisema Katiba na sheria za nchi zinatoa fursa kwa kila Mtanzania mwenye sifa kugombea nafasi za uongozi, lakini kwa sasa kipaumbele kinapaswa kuwa utekelezaji wa ajenda za maendeleo na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

“Kikatiba na kisheria kila mwenye sifa ana haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi. Hata hivyo, tunaamini kipindi hiki ni muhimu zaidi kuelekeza nguvu katika maendeleo na ustawi wa wananchi,” alisema Doyo.

Aliongeza kuwa wabunge na viongozi wengine wa kisiasa wanayo nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo kupitia mijadala ya bungeni, usimamizi wa miradi na ushauri kwa serikali katika masuala yanayogusa maisha ya wananchi.

Doyo alisema ushirikiano wa kisiasa na umakini katika utekelezaji wa majukumu ya maendeleo ni muhimu ili kuharakisha utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.

Aidha, alisema kauli mbalimbali zinazojadili mustakabali wa uongozi wa nchi zinaonyesha umuhimu wa viongozi kuendelea kuweka mbele masilahi ya Taifa na maendeleo ya wananchi.

“Kwa sasa ni wakati wa kushughulikia kero za wananchi, kuboresha huduma za jamii na kusukuma mbele ajenda ya maendeleo. Muda wa siasa za uchaguzi ukifika, kila mwenye nia na sifa atapata nafasi ya kujitokeza,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa NLD Wilaya ya Tanga, Abdul Karney, alisema bado kuna changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tanga, ikiwamo upatikanaji wa maji safi na salama pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya barabara.

Karney alisema wakati wa ziara ya chama hicho walipata fursa ya kujionea hali ya huduma hizo katika baadhi ya wilaya za mkoa huo.

Alitaja maeneo ya Maramba, Mashewa, Korogwe, Mwakijembe na Lushoto kuwa miongoni mwa yanayohitaji maboresho zaidi ya miundombinu ili kurahisisha shughuli za wananchi na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

“Tulijionea hali ya miundombinu na changamoto za upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo. Ni muhimu juhudi ziendelee kufanyika ili wananchi wapate huduma bora zaidi,” alisema.

Alisisitiza kuwa Serikali, vyama vya siasa na wadau mbalimbali wanapaswa kuendelea kushirikiana katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi na kuharakisha maendeleo kwa manufaa ya Watanzania wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *