Dar es Salaam. Mwongozaji wa tamthilia ya Kombolela, Abdul Juma ‘Abdul Writer’, amesema ilimchukua takribani mwezi mmoja hadi miwili kumshawishi Msemaji wa Timu Za Taifa, Diwani wa Kata ya Kariakoo  na mtangazaji, Haji Manara kukubali kuingia kwenye ulimwengu wa filamu.

Abdul amesema tangu mwanzo alikuwa akihitaji mtu mwenye ushawishi mkubwa kwa jamii. Anayekubalika kwenye mijadala na mwenye uwezo wa kubeba tabia ya mhusika aliyekuwa amemkusudia kwenye simulizi la Kombolela.

“Kumpata Haji Manara haikuwa rahisi kwa sababu hajawahi kuwa mwigizaji hapo awali. Nilimtafuta kwa karibu miezi miwili nikimbembeleza. Mara nyingi alikuwa akiniambia anapenda kazi ninayofanya na yupo tayari kunisapoti, ila si kwa kuigiza,” amesema Abdul.

Amesema wakati akiendelea kumshawishi, tayari alikuwa ameandaa nafasi ya fundi cherehani katika simulizi hilo. Uhusika ambao ungehusisha maisha ya nyumbani kwa Mzee Kikala.

Kwa mujibu wa Abdul, alikuwa akitafuta mtu mwenye uwezo wa kuishi na kuonyesha maisha ya Upwani kupitia mavazi, lafudhi na mwenendo wake wa maisha. Jambo lililomfanya aamini Haji ndiye alikuwa chaguo sahihi.

“Nikafikiri Haji anafiti zaidi kwenye nafasi hiyo. Niliona pamoja na ubora wake kwenye sekta ya michezo, anaweza pia kufanya vizuri kwenye uigizaji,” amesema.

Mwongozaji huyo amesema baada ya majaribio kadhaa ya kumshawishi kushindikana, siku moja alikutana na Haji Mlimani City hapo ndipo walipata nafasi ya kumuelezea kwa kina mhusika ambaye angecheza na namna simulizi hiyo ilivyokuwa umeandaliwa.

Amesema hapo ndipo Haji alianza kuona upekee wa nafasi hiyo na hatimaye kukubali kushiriki kwenye tamthilia hiyo.

“Hapo awali sikuwahi kumueleza kwa undani ataenda kuigizaje. Nilipomuelezea majukumu yake na aina ya mhusika atakayekuwa, akaona inaweza kuwa nafasi tofauti kwake na ndipo akakubali,” amesema.

Abdul amesema licha ya kuwa mgeni kwenye uigizaji, Haji Manara ameonyesha kiwango kizuri cha utendaji na kumshangaza yeye pamoja na wadau wengine waliokuwa wakifuatilia kazi hiyo.

Picha ya Abdul mwongozaji wa tamthilia ya Kombolela

“Performance yake ni nzuri sana ukilinganisha na ugeni wake. Wapo waigizaji wanaokuja mara ya kwanza wakapata shida, lakini yeye ameweza. Mimi naona ana kipaji kikubwa cha muda mrefu, sema tu hakupata mtu wa kumwambia asonge mbele,” amesema.

Ameongeza kuwa hakukutana na changamoto yoyote kubwa, alipokuwa akifanya kazi na Haji. Akieleza kuwa amekuwa miongoni mwa watu waliotekeleza maelekezo kwa haraka na kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa.

Kuhusu mapokezi ya mashabiki, Abdul amesema ujio wa Haji Manara kwenye Kombolela umevutia makundi mapya ya watazamaji, hususan kutoka kwenye sekta ya michezo ambao hapo awali hawakuwa karibu sana na tamthilia hiyo.

“Tumeona hata watu wa michezo wameanza kutoa maoni kuhusu Kombolela kwa sababu kuna mtu wao ndani ya kazi hii. Hilo pekee linaonyesha tumefanikiwa kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Akizungumzia mtazamo wa baadhi ya watu wanaodai watu maarufu huingia kwenye uigizaji kwa ajili ya kutafuta umaarufu zaidi. Abdul amesema hana tatizo na jambo hilo ikiwa linaweza kusaidia kukuza kazi na kuwafikia watu wengi zaidi.

“Hakuna ubaya kama mtu maarufu akiingia kwenye uigizaji. Kikubwa ni kuongeza wigo wa watazamaji na kuwafikia watu wengi zaidi,” amesema.

Abdul amewataka mashabiki wa Kombolela kuendelea kuifuatilia tamthilia hiyo, akiahidi kuwa kuna sura nyingine maarufu zitaonekana hivi karibuni. Ikiwemo uwezekano wa kuonekana kwa waigizaji wakubwa kutoka nje ya Tanzania.

Amehitimisha kwa kuwashukuru mashabiki kwa kuendelea kuipokea Kombolela. Akisema mchango wao ndiyo unaoifanya kazi hiyo kuendelea kukua siku hadi siku

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *