Dar es Salaam. Ulimwengu wa muziki umeingia katika majonzi kufuatia kifo cha mwanamuziki mkongwe wa Marekani, Peabo Bryson, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 75. Huku akiacha urithi mkubwa wa nyimbo zake za mapenzi na sauti iliyogusa mioyo ya mamilioni ya watu duniani.
Bryson, ambaye kwa miongo kadhaa alitambulika kama mmoja wa waimbaji bora wa muziki wa R&B na Soul, alifariki Juni 2, 2026 baada ya kuugua kiharusi kama ilivyoeleza familia yake.
Ingawa alitamba kupitia nyimbo nyingi za mapenzi. Bryson atakumbukwa zaidi kusikika katika nyimbo mbili zilizobeba historia kubwa katika ulimwengu wa filamu za Disney, Beauty and the Beast alioimba na Celine Dion pamoja na A Whole New World alioshirikiana kuimba na Regina Belle.
Nyimbo hizo zitaendelea kuwa sehemu ya kumbukumbu za maisha ya mamilioni ya watu duniani. Wengi wamekua wakizisikiliza, wengine wakizitumia katika sherehe za harusi na wengine wakizihusisha na nyakati muhimu za maisha yao.
Mwaka 1992, Beauty and the Beast ilimletea tuzo ya Grammy na kumtambulisha kwa kizazi kipya cha mashabiki wa muziki duniani. Mwaka mmoja baadaye, A Whole New World iliandika historia kuwa wimbo wa kwanza kutoka filamu ya katuni ya Disney kufika nafasi ya kwanza katika chati ya Billboard Hot 100 nchini Marekani.
Zaidi ya tuzo na mafanikio, Bryson alikuwa mfano wa msanii aliyedumu katika tasnia kwa zaidi ya miaka 50 huku akiendelea kuheshimika kwa kipaji chake. Alitoa albamu zaidi ya 20 na kushirikiana na baadhi ya majina makubwa katika muziki kimataifa.
Kifo chake kimeacha pengo kubwa kwa familia, marafiki na mashabiki wake duniani kote. Hata hivyo, sauti yake itaendelea kuishi kupitia nyimbo alizoacha, ambazo zimekuwa sehemu ya historia ya muziki na kumbukumbu za maisha ya watu wengi.