
Vijana wawili, wote wanasheria kitaaluma, wakapita chuo kimoja kwa nyakati tofauti kusoma masuala ya kodi. Wote wakawa wakaguzi wa kodi.
Walikutana kazini wakiwa wataalamu wa kodi. Uhusiano wao ulianzia kazini, wakauhamishia kwenye siasa. Walianzisha chama pamoja, wakafanya siasa za upinzani kwa upacha wa hali ya juu. Walipofanikiwa kushinda dola, kila kitu kikabadilika.
Bassirou Diomaye Faye na Ousmane Sonko, ndiyo wahusika wa muktadha. Mapito yao, ushindi wao, kutengana kwao ni darasa kuwa dunia haijabadilika sana, kutoka utatu wa Julius Caesar, Pompey the Great na Marcus Crassus, ulivyovunjika na kuiacha Roma ikiwa magofu, miongo mitano Kabla ya Kristo.
Ni shule kwamba dunia ni ileile ya utatu (troika) wa Joseph Stalin, Grigory Zinoviev na Lev Kamenev, Urusi (Soviet). Baada ya Stalin kushika madaraka, hatima ya troika ilikuwa Zinoviev na Kamenev, kuuawa kwa kupigwa risasi, tena kwa amri ya Stalin.
Jibu ni moja tu; madaraka huwa hayachangiwi. Ndoa za kisiasa (political marriages), siyo taasisi ya moyo na imani. Huvunjika haraka kwa sababu za kimasilahi.
Katika kitabu changu “Kikwete Lowassa; Urafiki, Ndoa Yao ya Kisiasa, Uadui,” niliandika yafuatayo:
“Mamlaka yana wivu kupindukia na hayana kawaida ya kushindwa vita ya mapenzi. Wenye kuyaendea ndivyo sivyo, hao ndiyo hushindwa, huumia au hata kuangamia.
“Ukifunga ndoa ya kisiasa baada ya kuingia madarakani, mamlaka huchanua wivu wake, ama uchague mwenzi wako au uyape yenyewe thamani yake. Mamlaka hayatambui ndoa za mitaala. Watu wawili hawawezi kutawala kwa pamoja. Moto utawaka. Mamlaka yakija kwako, yaheshimu, yanyenyekee, yakumbatie na uyatimizie mahitaji yake. Utafaulu.” Mwisho wa kunukuu.
Kuyaingiza Mamlaka kwenye ndoa za mitaala, ni sababu ya Tony Blair na Gordon Brown, kuvurugana, UK. Thabo Mbeki na Jacob Zuma walining’inizana, Afrika Kusini.
Uhuru Kenyatta na William Ruto, ndoa ilivunjika vipande vipande, Kenya. Jakaya Kikwete na Edward Lowassa, hata vyombo vya ndani hawakupata wasaa wa kugawana, Tanzania. Diomaye na Sonko, ni vita pevu Senegal.
Tuzame Senegal
Mwanamuziki Hamis Mwinjuma “MwanaFA”, katika wimbo “Asanteni kwa Kuja”, ubeti wa tatu, anarap “Ilikuwa poa tu, ilikuwa love tu, ilikuwa safi kabla mkwanja haujaleta makuu. Ilikuwa shega tu, ilikuwa peace tu, ilikuwa mzuka ghafla mkwanja ukaleta upuuzi.”
MwanaFA ambaye kwa sasa ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, tafsiri ya mistari yake hiyo ni kuwa mambo yalikuwa mazuri, amani na upendo, lakini fedha ilipoingia kati, kila kitu kilibadilika.
Fedha na mamlaka ni harabu ya upendo na uhusiano. Ilikuwa mshikamano wenye upendo mkubwa baina ya Diomaye na Sonko, kabla mamlaka hayajawavuruga.
Rudi miaka 12 iliyopita. Ilikuwa Januari 2014. Sonko, aliyekuwa na umri wa miaka 39, alikuwa ameshafukuzwa kwenye utumishi wa umma kwa sababu ya kujihusisha na siasa, akaamua kuanzisha chama. Sonko alimfanya Diomaye kuwa mshirika wake muhimu. Diomaye, aliyekuwa na umri wa miaka 33, alikuwa sehemu ya timu iliyojenga maono, sera na falsafa za chama. Pastef ndiyo jina la chama.
Pastef, kifupi cha maneno ya Kifaransa, Patriotes Africains du Sénégal pour le Travail, l’Ethique et la Fraternité, yakiwa na maana ya chama cha Wazalendo wa Kiafrika wa Senegal kwa ajili ya Kazi, Maadili na Undugu. Sonko akawa kiongozi wa Pastef.
Katika uchaguzi wa urais Senegal, uliofanyika Februari 24, 2019, Sonko akiwa na umri wa miaka 44, alishika nafasi ya tatu nyuma ya mshindi, Rais Mack Sall, na Idrissa Seck, aliyetoka wa pili.
Miaka mitatu baadaye, yaani mwaka 2022, Diomaye alikuwa Katibu Mkuu wa Pastef. Tazama upacha huu; Sonko mkuu wa chama, Diomaye, mtendaji mkuu. Ni kipindi ambacho Sonko alikuwa juu kabisa ya kilele cha siasa Senegal na pembeni yake alionekana Diomaye, pacha wake.
Ulikuwa wakati ambao Pastef ilibeba sauti kubwa ya upinzani Senegal. Aprili 2023, Sonko na Diomaye walifungwa jela kwa makosa ya kufanya siasa za uchochezi.
Walikaa jela kwa miezi 11. Kuelekea Uchaguzi wa Rais Senegal 2026, Sonko alizuiwa kushiriki kutokana na hatia alizokutwa nazo mahakamani, ikiwamo kutoa rushwa na kumchafua kwa uongo aliyekuwa Waziri wa Utalii, Mame Mbaye Niang.
Yalikuwa mapito magumu ya kisiasa na kisheria ya Sonko. Mwaka 2021, Sonko alishitakiwa kwa kumbaka mara kwa mara mfanyakazi wa kituo cha “masaji”. Mwaka 2023, mahakama ilitoa hukumu kuwa Sonko hakuwa na hatia katika kesi ya ubakaji, lakini ilimtia hatiani kwa kumpa rushwa mfanyakazi wa “masaji”, hivyo ilimhukumu kwenda jela miaka miwili.
Sonko baada ya kuzuiwa kushiriki uchaguzi, alimpendekeza Diomaye kuwa mbeba tiketi ya Pastef. Jina kuu ni Sonko, kwa kutambua hilo, kauli mbiu iliandikwa “Diomaye Mooy Sonko”, ikiwa na maana “Diomaye Ndiye Sonko.” Mipango na michakato yote ya Diomaye kugombea urais, ilifanywa akiwa jela na Sonko.
Nusura uchaguzi ufanyike Diomaye akiwa jela. Awali, uchaguzi ulikuwa ufanyike Februari 25, 2024. Ukasogezwa mbele hadi Machi 24, 2024, hivyo kusababisha vurugu kubwa. Mapema Machi, Bunge la Senegal lilipitisha sheria ya msamaha (Senegal’s Amnesty Law), ambayo iliwafutia makosa watu wote waliokutwa na hatia katika ghasia za kisiasa nchini humo kati ya Februari Mosi, 2021 na Februari 25, 2024. Sheria hiyo iliwaweka huru Diomaye na Sonko.
Wasenegali hawataisahau ile siku. Ilikuwa Machi 14, 2025. Barabara za jiji la Dar zilifurika watu. Yalikuwa maandamano ya mapokezi ya Diomaye na Sonko. Mabango makubwa yalibeba ujumbe “Diomaye Mooy Sonko”. Hiyo ilikuwa siku 10 kabla ya uchaguzi. Kampeni zilianza rasmi Machi 9, 2024.
Siku ikafika. Wasenegali milioni 4.5, ambao ni asilimia 61.3 ya waliojiandikisha kupiga kura, walijitokeza siku ya uchaguzi. Kisha, Wasenegali 2,434,751, ambao ni sawa na asilimia 54.28 ya waliopiga kura, walimchagua Diomaye. Kilikuwa kishindo. Historia ikaandikwa. Diomaye akiwa na umri wa miaka 44, akaweka rekodi ya kuwa Rais mwenye umri mdogo zaidi kupata kuiongoza Senegal.
Kwa uaminifu mkubwa, Diomaye alimteua Sonko kuwa Waziri Mkuu. Mpaka hapo, ilitakiwa Sonko atambue kwamba kibao kilishageuka.
Ni kweli umaarufu wake, na nguvu yake kubwa ya ushawishi, ndivyo vilimpa urais Diomaye. Ni kweli pia, yeye (Sonko), ndiye kiongozi wa chama, Pastef. Hata hivyo, Diomaye alishakuwa Rais. Raia namba moja katika nchi.
“Never outshine your master,” – “Kamwe usimfunike bosi wako” Ni sheria namba moja kati ya 48, kama zilivyoandikwa na mwandishi Robert Greene, katika kitabu chake “The 48 Laws of Power” – “Sheria 48 za Mamlaka.” Sonko alipitwa na ujumbe huu. Alitaka kuendelea kuwa mkubwa mbele ya Diomaye.
Dalili zilikuwa wazi kwamba ndoa ya kisiasa baina ya Diomaye na Sonko isingekuwa na maisha marefu. Diomaye alikuwa mdogo kabla ya urais. Hivyo, ilikuwa sawa kwake kufanya kazi chini ya Sonko. Baada ya kuwa Rais, ndani ya Pastef kukawa na mafahari wawili. Diomaye Rais wa nchi, Sonko kiongozi wa chama. Mafahari wawili hawakai zizi moja, abadan!
Deni la Taifa Senegal ni kubwa. Limefikia asilimia 132 ya Pato la Ndani la Taifa (GDP). Hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Hali hiyo imesababisha presha kubwa. Presha hiyo ikawa sababu ya hitimisho la uhusiano wa kikazi baina ya Diomaye na Sonko.
Mei 26, 2026 (Jumanne), Sonko alitoa msimamo wake bungeni, uliokinzana na ule wa Diomaye, kuhusu namna ya kushughulikia deni la taifa.
Kitendo cha waziri mkuu kukinzana na rais waziwazi, ni kipimo cha juu kwamba uhusiano wa kikazi umefika mwisho.
Bila kuchelewa, Diomaye alimfuta kazi Sonko. Kisha, kwa kuwa Sonko ndiye kiongozi wa Pastef, chama ambacho kina wabunge wengi, alicheza karata zake vema.
Ilimchukua Sonko muda wa chini ya saa 72, kupindua meza na kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Senegal.
Fikra za wengi ni kuwa Sonko kwa nafasi yake ya spika wa bunge, ataliongoza bunge kuibana serikali, ili kumkomoa Diomaye.
Hata hivyo, mtindo wa kisiasa wa Sonko ni kuyaelekea yale ambayo wananchi wanapenda kuyasikia, hata kama hayana uhalisia. Ni kwa sababu hiyo hoja yoyote ambayo itakuwa inaibana Serikali na ina mvuto kwa umma, matarajio ni kwamba Sonko ataibebea bango bungeni.
Mathalan, deni la taifa Diomaye alilikuta. Mtazamo Diomaye ni kukubaliana na mapendekezo ya IMF ya kufanya majadiliano na wadeni wa kimataifa na kukubaliana mpango wa malipo, wakati Sonko anataka Serikali isiwasikilize IMF, badala yake deni lilipwe kwa kufanya mabadiliko ya mikataba ya nishati na kubana matumizi.
Jambo la kushika
Ndoa za kisiasa hazifungwi na kasisi wala shehe. Jina la Mungu huwa halitajwi. Hazina kiapo wala mkataba. Hufungwa kwa kuaminiana kulingana na mahitaji ya nyakati. Washenga huitenda kazi kwa masilahi. Nyakati za machafuko ya ndoa, badala ya kusimama kama wapatanishi, huegemea upande wenye masilahi yao.
Hadithi za makubaliano huwa maneno ambayo hayamfungi mtu. Rahisi kuyakana. Kwamba Jakaya alikuwa na ahadi ya kumwachia Edward urais, vivyo hivyo Uhuru kwa Ruto, Mbeki na Zuma, au Blair kumwachia kijiti swahiba wake Brown. Hakuna mkataba, washenga, wala nyaraka za kiapo kuthibitisha maneno hayo.
Mara nyingi lawama humwelekea mwenye mamlaka. Ukweli ni kuwa unyenyekevu dhidi ya aliye na mamlaka hulinda uhusiano.
Shida kubwa watu wengi hudhani historia za nyuma zinaweza kuwalinda mbele ya wenye mamlaka. Husahau kwamba baada ya kula kiapo na kushika madaraka, mtu hubadilika. Mamlaka humlazimisha kubadilika.
Sonko alipaswa kutambua kuwa ni kweli Diomaye alikuwa kijana wake kisiasa. Alimwongoza tangu wakiwa wakaguzi wa kodi. Baadaye kwenye chama cha mawakala wa kodi Senegal (SAID), kabla ya kumshawishi kujiunga na siasa kupitia Pastef. Yote hayo Sonko alipaswa kuyameza baada ya Diomaye kuwa Rais.
Hivi sasa Sonko anaendelea kuwa Kiongozi wa Pastef. Diomaye hana chama. Hadithi kama Bakili Muluzi na Bingu wa Mutharika Malawi. Yajayo Senegal ni kizungumkuti. Ni somo lilelile kuwa ndoa za kisiasa mwisho wake huwa si mwema. Dunia ya Jakaya Kikwete na Edward Lowassa, haijabadilika, haitabadilika.