
Dar es Salaam. Benki ya Stanbic Tanzania imepata ufadhili wa Sh70 bilioni utakaotumika kuongeza mikopo kwa biashara ndogo na za kati (SMEs), hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa mitaji kwa wafanyabiashara na kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi.
Ufadhili huo umetolewa kwa awamu mbili, ambapo Sh50 bilioni zilipatikana na kuanza kutumika mwaka 2025, huku Sh20 bilioni zimepatikana mwaka 2026.
Fedha hizo zimepatikana kupitia ushirikiano kati ya Stanbic Bank Tanzania, Finance in Motion na eco.business Fund ukilenga kusaidia biashara zinazojihusisha na kilimo endelevu, minyororo ya thamani ya kilimo, pamoja na sekta nyingine zinazochangia ukuaji wa uchumi na ajira.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutia saini makubaliano hayo iliyofanyika Dar es Salaam, Ofisa Mkuu wa Fedha wa Stanbic Bank Tanzania, Derick Lugamala amesema ufadhili huo unaonesha dhamira ya benki ya kuwezesha biashara kwa mitaji inayochochea ukuaji na kuimarisha uwajibikaji wa kifedha.
“Biashara ndogo na za kati zina nafasi kubwa katika mustakabali wa uchumi wa Tanzania. Zinatoa ajira, zinaimarisha minyororo ya thamani na kusaidia maendeleo ya biashara za ndani. Kupitia ufadhili huu tunaongeza upatikanaji wa mikopo inayowezesha wafanyabiashara kuwekeza, kukua na kujenga ustahimilivu wa muda mrefu,” amesema Lugamala.
Amesema ushirikiano kati ya Stanbic, Finance in Motion na eco.business Fund unatoa fursa ya kusaidia biashara zinazohitaji mtaji huku zikitekeleza mifumo endelevu ya uzalishaji na uendeshaji.
Kwa mujibu wa Stanbic, fedha hizo zitatolewa kwa Shilingi za Kitanzania, jambo litakalowasaidia wafanyabiashara kupunguza athari za mabadiliko ya viwango vya fedha za kigeni na kuwawezesha kupanga kwa uhakika zaidi shughuli zao za muda mrefu.
Ufadhili huo pia unaendana na mkakati wa Stanbic wa kusaidia maendeleo endelevu kwa kuchangia ukuaji wa uchumi, kuimarisha ujumuishaji wa kifedha, kusaidia miundombinu inayostahimili mabadiliko ya tabianchi na kusimamia vihatarishi vya mazingira, jamii na utawala bora.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa eco.business Fund, Michael Evers, amesema taasisi hiyo inaendelea kuelekeza mitaji katika biashara zinazochangia maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.
“Tunafurahi kuendelea kufanya kazi na Stanbic Bank Tanzania katika kuongeza upatikanaji wa mikopo kwa biashara zinazofanya kazi katika kilimo endelevu na minyororo ya thamani ya kilimo. Sekta hizi ni muhimu kwa uchumi wa ndani na mikopo inayofaa inaweza kuongeza tija, kuimarisha minyororo ya ugavi na kuendeleza uzalishaji endelevu,” amesema Evers.
Amesema eco.business Fund inalenga kusaidia biashara zinazochangia uhifadhi wa bioanuai, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi na matumizi bora ya rasilimali.
Naye Mkuu wa Idara ya Biashara wa Stanbic Bank Tanzania, Fredrick Max amesema ufadhili huo utawezesha benki hiyo kuwafikia wafanyabiashara wengi zaidi na kusaidia sekta mbalimbali za uchumi.