Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya mchezo wa Kuogelea Baharini, imeahidi kurejea na medali katika mashindano ya kanda Afrika yatakayofanyika Mauritius Juni 6 na Juni 7 mwaka huu.

Akizungumza leo Juni 3, 2026 wakati wa hafla ya kuiaga na kuikabidhi bendera timu hiyo, mwakilishi wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Afisa Michezo Mwandamizi, Ingridy Kimario alisema Serikali ina imani kubwa na timu hiyo na inatarajia kuona wanamichezo hao wakirejea na medali.

“Tunawapongeza kwa hatua mliyofikia. Mnapokwenda si kwenda kushiriki tu, bali kwenda kutuletea ushindi na medali. Baraza la Michezo la Taifa liko pamoja nanyi na lina imani kubwa kuwa mtaiwakilisha vyema Tanzania,” amesema Kimario.

Amewataka wanamichezo hao kwenda kupambana kwa uzalendo na kushirikiana kama timu moja ili kupeperusha vyema bendera ya Taifa.

“Kuogelea baharini kuna changamoto zake tofauti na kuogelea kwenye bwawa, lakini ninaamini mmejiandaa vizuri na mko tayari kufanya vizuri katika mashindano hayo,” amesema.

Pia, amezungumzia changamoto ya ushiriki wa wanawake katika michezo, akisema bado jamii inahitaji kupewa elimu zaidi ili kubadili mitazamo inayowazuia watoto wa kike kushiriki kikamilifu katika michezo.

“Mtoto wa kike anaweza kufanya vizuri katika michezo kama mtoto wa kiume na tunapaswa kuendelea kutoa elimu kwa wazazi na jamii ili kuongeza ushiriki wa wanawake na wasichana katika michezo mbalimbali,” amesema Kimario.

Mratibu wa Kamati ya mchezo wa Kuogelea Baharini chini ya Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA), Ramadhani Mkoveka amesema ushiriki wa Tanzania katika mashindano hayo ni sehemu ya juhudi za kukuza mchezo wa kuogelea nchini na kuwapa wanamichezo nafasi ya kupata uzoefu wa kimataifa.

Nahodha wa timu hiyo, Adil Abdurahman Husein amesema  wanamichezo wote wamejipanga kufanya vizuri na kuhakikisha wanailetea Tanzania heshima.

“Tunaenda kuiwakilisha Tanzania na kufanya kila linalowezekana ili kupata matokeo mazuri, lengo letu ni kufanya vizuri, kutengeneza muda mzuri na kupambana kwa ajili ya ushindi,” amesema Hussein.

Kwa upande wake, Kocha wa timu hiyo, Khalid Rushaka amesema maandalizi ya timu yamekuwa mazuri kutokana na ushiriki wa wanamichezo katika mashindano mbalimbali yaliyowapa uzoefu wa kutosha.

Amesema baadhi ya waogeleaji walishiriki mashindano ya Taifa yaliyofanyika Kigamboni mwaka jana, mashindano ya kuogelea baharini yaliyofanyika Mombasa nchini Kenya pamoja na mashindano ya kimataifa yaliyofanyika Algeria.

“Wachezaji wetu wako katika hali nzuri na wana uwezo wa kufanya vizuri, tunatarajia kuona matokeo chanya yatakayowasaidia kufuzu mashindano makubwa zaidi siku zijazo. Tumejenga mshikamano mzuri ndani ya timu na tunaenda kama timu moja ya Tanzania,” amesema Rushaka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *