Serikali ya Mali imezindua kifurushi kisicho cha kawaida cha hatua za usalama, kikijumuisha zawadi kubwa za kifedha na hatua kali, kama sehemu ya kuzidisha mapambano dhidi ya makundi ya waasi yenye silaha ambayo yamezidisha mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni, haswa baada ya shambulio la umwagaji damu la Aprili 25 lililomuua Waziri wa Ulinzi wa Mali.

Katika hatua inayoakisi ukubwa wa changamoto za kiusalama zinazoikabili nchi hiyo, serikali ya Mali imetangaza zawadi za fedha ya hadi faranga za CFA bilioni 7.5 (karibu dola milioni 12.4) kwa taarifa zitakazopelekea kukamatwa au kuuawa viongozi saba mashuhuri wa makundi ya waasi yenye silaha nchini humo.

Orodha hiyo imeongozwa na Iyad Ag Ghali, kiongozi wa kundi linaloshirikiana na Al-Qaeda “Jama’at Nusrat al-Islam Walmuslimin” (JNIM), ambaye serikali imetoa zawadi ya karibu dola milioni 3.3 kwa taarifa zitakazopelekea kukamatwa au kuuawa kwake.

Iyad Ag Ghali, mwanadiplomasia wa zamani wa Mali na mmoja wa viongozi mashuhuri wa waasi wa Tuareg, ni miongoni mwa watu wanaotafutwa sana katika eneo la Sahel. Amewekwa kwenye orodha ya ugaidi ya Marekani na anatafutwa chini ya hati iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.

Serikali pia imetenga zawadi ya faranga za CFA bilioni 1.5 (karibu dola milioni 2.48) kwa taarifa zitakazopelekea kukamatwa au kuuawa Amadou Koufa, kiongozi wa kundi la Macina, naibu wa Iyad Ag Ghali huko katikati mwa Mali, na mmoja wa viongozi mashuhuri wa makundi yenye silaha nchini humo.

Orodha hiyo pia inamjumuisha Abdoulaye Mamadou Diallo, anayejulikana kama “Joulibib,” huku mamlaka zikitoa zawadi sawa kwa taarifa yoyote itayopelekea kukamatwa kwake.

Kama sehemu ya msako mkali dhidi ya makundi ya waasi yenye silaha, serikali ya Mali pia imeamua kusimamisha usafirishaji wa pikipiki zenye uwezo wa sentimita za ujazo 125 au zaidi nje ya miji mikubwa, huku ikisimamisha uagizaji, uuzaji na usambazaji wa pikipiki hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Uamuzi huo unahusu sehemu kubwa ya nchi, isipokuwa mji mkuu wa Mali, Bamako na baadhi ya vituo vikubwa vya mijini.

Serikali inatarajia hatua hii itapunguza uwezo wa makundi yenye silaha kusonga mbele haraka na kuvuka vituo vya ukaguzi, hasa katika maeneo ya vijijini na barabara mbaya ambapo makundi ya waasi hutegemea sana pikipiki katika shughuli zao za kijeshi na upelelezi.

Licha ya malengo ya usalama ya uamuzi huo, lakini unaibua wasiwasi mkubwa kuhusu athari zake kwa raia wa kawaida, kwani pikipiki zinatambuliwa kuwa njia kuu ya usafiri kwa mamilioni ya Wamali, haswa katika maeneo ya vijijini yenye zaidi ya nusu ya idadi ya watu nchini, ambapo hutumika kwa usafiri wa kwenda na kurudi, kusafirisha wagonjwa na bidhaa, na kwenda kwenye masoko na huduma za msingi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *