Wakulima wa zao la miwa katika wilaya za Mvomero na Kilosa mkoani Morogoro wamehimizwa kutumia viuatilifu kwa usahihi na kufuata taratibu za usalama ili kujikinga na madhara yanayoweza kuathiri afya zao pamoja na mazingira.
Rai hiyo imetolewa na Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Kituo cha Kibaha, Ngabo Vicent Pamba wakati wa mafunzo maalumu yaliyofanyika eneo la Mtibwa wilayani Mvomero, yakihusisha wakulima wa miwa, maafisa ugani, wauzaji wa pembejeo za kilimo pamoja na maafisa wa mazingira.
Ngabo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo wadau mbalimbali wa mnyororo wa thamani wa zao la miwa kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu na namna salama ya kuhifadhi na kutupa vifungashio vya viuatilifu baada ya matumizi.
“Tuko hapa Mtibwa kutoa mafunzo mahususi kwa wakulima, maafisa ugani, wauzaji wa pembejeo na maafisa wa mazingira kuhusu matumizi sahihi ya viuatilifu pamoja na uhifadhi salama wa vifungashio vyake. Lengo ni kuiepusha jamii ya wakulima na madhara yanayoweza kujitokeza kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya viuatilifu,” amesema Ngabo.
Ameeleza kuwa TARI Kibaha imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za kuboresha kilimo cha miwa nchini na kwamba mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha wakulima wanalima kwa tija huku wakilinda afya zao na mazingira.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fedha za kutosha kusaidia utekelezaji wa programu zinazolenga kuimarisha usalama wa wakulima na kuongeza tija katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wake, Afisa Mwandamizi kutoka Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Raphael Mwezi, amesema mamlaka hiyo imeungana na TARI katika kutoa elimu kwa wakulima ili kuhakikisha matumizi ya viuatilifu yanafanyika kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
Amesema kupitia mafunzo hayo, wakulima wamefundishwa namna ya kujikinga dhidi ya madhara ya viuatilifu kwa kutumia vifaa kinga wakati wa kunyunyizia sumu za viuatilifu
(Feed generated with FetchRSS)