Shambulio la ndege zisizo na rubani sokoni katika jimbo la Kordofan Kaskazini nchini Sudan limeua takriban raia 11 na kujeruhi makumi ya wengine.

Shirika la Haki za Binadamu la Sudan limearifu kuwa ndege isiyo na rubani ilishambulia soko katika eneo la Abu Zaeima huko Hamrat Al Sheikh Kordofan Kaskazini.  

Shambulio hilo liliua raia 11 na kujeruhi makumi ya wengine, kulingana na idadi ya awali.

Shirika la Haki za Binadamu la Sudan limeeleza kuwa shambuli hilo limejiri masaa 24 baada ya mashambulizi kama hayo ya ndege zisizo na rubani kulenga vijiji na gari la raia katika eneo hilo hilo.

Shirika hilo limelaani hujuma hiyo ya ndege zisizo narubani katika soko huko Kordofan Kaskazini na kusema kuwa, vitendo vya mara kwa mara vya kuwalenga mara raia, vijiji na vyombo vya usafiri wa raia vinadhihirisha kupuuzwa wazi maisha ya binadamu na kanuni za msingi za sheria ya kimataifa ya kibinadamu.

Aidha limesema kuwa kuendelea kuuliwa raia hakupaswi kuchukuliwa kama jambo la kawaida na kutaka kukomeshwa hujuma kama hizo na kuadhibiwa wahusika wa jinai hizo.

Mapema siku ya Jumamosi, Shirika la Haki za Binadamu la Sudan liliarifu kuwa watu wanne wameuawa na sita kujeruhiwa kufuatia mashambulizi ya droni katika vijiji viwili sikuhuko Kordofan Kaskazini juzi Ijumaa.

Umoja wa Mataifa mwezi Mei ulitahadharisha kuhusu kuongezeka mashambulizi ya ndege zisizo na rubani katika jimbo la Kordofan, ukisema mashambulizi hayo yameuwa takriban raia 880 kati ya Januari na Aprili 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *