Kwa mujibu wa jarida la Foreign Affairs la nchini Marekani, vita na Iran vinaweza kutoa changamoto kubwa kwa jeshi la Marekani na hasa kuhusu hatari ya kushambuliwa kambi zake za kijeshi katika siku zijazo.

Vituo vya kijeshi vya Marekani katika Nchi za Kiarabu za eneo hili la Mashariki ya Kati, zikiwemo Qatar, Imarati, Bahrain, Saudi Arabia, Kuwait na Jordan, zilishambuliwa moja kwa moja na Iran wakati wa vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kutokana na kuwa wenyeji wa kambi za Marekani na kuruhusu vituo hivyo kutumika dhidi ya Iran.

Sasa wasiwasi umeibuka katika nchi za Asia Mashariki kwamba hatima kama hiyo ya nchi za Kiarabu za Asia Magharibi huenda ikazikumba katika siku zijazo ikiwa hazitachukua tahadhari ya kutosha katika uwanja huo. Nchi kama vile Japan, Korea Kusini, Australia na Ufilipino huenda zikaiwekea Marekani vikwazo zaidi katika kutumia kambi zake za kijeshi zilizopo katika ardhi zao, ikiwa kutatokea mzozo kati ya Marekani na China, zikihofia mashambulizi ya kulipiza kisasi kutoka kwa Beijing.

 

Kwa kupungua uwezo wa Marekani wa kufikia na kunufaika na kambi zake zilizopo katika nchi za nje, uwezo wa Washington kuanzisha chokochoko na kuingilia kijeshi sehemu mbalimbali za dunia utapungua pakubwa.

Hali hii ilionekana wazi katika vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa kibaguzi wa Israel dhidi ya Iran ambapo Iran ilifanikiwa pakubwa katika kuzima na kulemaza mashambulio ya pande mbili hizo zenye silaha za nyuklia. Katika vita hivyo vya siku 40 Iran iliweza kupambana kishujaa na wavamizi hao wenye silaha za kisasa na kuvishambulia vikali kambi za kijeshi za adui zilizoko katika nchi za Kiarabu za eneo na hivyo kufanya kambi hizo kutokuwa na umuhimu mkubwa wa kijeshi kwa Marekani. Uharibifu mkubwa ulifanyika katika vituo hivyo vya kijeshi kiasi cha kuwalazimu askari wa Marekani kukimbilia usalama wao katika maeneo ya kiraia, jambo ambalo ni kinyume na sheria za kimataifa za vita kwa sababu linahatarisha maisha ya raia wa kawaida.

Ni wazi kuwa iwapo vita vitaibuka tena katika eneo huenda uharibifu mkubwa zaidi ukafanyika dhidi ya askari wa kigeni katika eneo. Jambo hili lilisisitizwa wazi na Meja Jenerali Muhsin Rezaei, kamanda wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mahojiano na televisheni ya CNN ambapo alisema ikiwa vita vitaibuliwa tena na maadu katika eneo, vitakuwa na madhara makubwa kwa Marekani.

Kamanda huyo wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Vita vya Kujitetea Kutakatifu vya miaka minane vya Iraq dhidi ya Iran alisema katika mahojiano hayo kwamba Lango Bahari la Hormuz ni mali ya Iran na Oman, hivyo usimamizi wake unapasa kufanywa kwa ushirikiano wa nchi mbili hizi.

Amesema hali ya Lango Bahari la Hormuz si hatari kwa biashara, bali ni hatari kwa vurugu na operesheni za kijeshi, na kuwa ni Marekani ndiyo inavuruga usalama na utulivu wa eneo hili. Amesisitiza kuwa ikiwa Marekani itaendelea na tabia hii, itapata mapigo makali ya Iran katika siku zijazo.

Meja Jenerali Rezaei pia ameonya, akijibu swali la mwandishi wa CNN aliyesema “kwa kuzingatia tishio la Trump dhidi ya miundombinu ya Iran kuwa vita hivi vitakuwa na uharibifu mkubwa kwa Iran,” kwamba, ikiwa vita vitaendelea na mzingiro kutoondolewa, tutapanua zaidi vita nje ya eneo, kutoka Bahari ya Hindi hadi Bahari ya Shamu na Lango Bahari la Bab al-Mandab na Bahari ya Mediterania, na hili bila shaka litakuwa na matokeo mabaya sana kwa Marekani.

Ni kwa kutilia maanani maonyo na tahadhari hizi ndipo, nchi nyingine zilizo na kambi za kijeshi za Marekani katika maeneo mengine ya dunia zikapata funzo muhimu kutoka kwa Iran na kutaka hatua za lazima zichukuliwe ili kuepuka kukabiliwa na hatima kama ile iliyozifika nchi za Kiarabu za Asia Magharibi katika vita vya karibuni vya Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *