#HABARI: Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa ufafanuzi kuhusu lalamiko la mwanamke aitwaye Filomena Richard Mataris, Miaka 36, Mkazi wa Gongo la mboto, Dar es Salaam, kuhusu kubadilishiwa mtoto baada ya
kujifungua katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo.

Limesema Juni 05, 2026 Filomena Richard Mataris akiwa na mume wake Caros
Kapata walifika kituo cha Polisi Bagamoyo wakilalamika kubadilishiwa mtoto Hospitali ya Bagamoyo.

Walieleza kuwa Aprili 14, 2026 Filomena Richard alihama kutoka Gongo la Mboto Dar es Salaam kwenda Kerege, wilayani Bagamoyo kwa mtoto wa dada yake aitwaye Avetha Mabadiliko kwa ajili ya uangalizi wa karibu.

Mei 17, 2026 majira ya saa 3:00 asubuhi alipata uchungu wa kujifungua hivyo aliongozana na ndugu yake huyo Avetha Mabadiliko kwenda Hospitali ya Kerege kwa ajili ya kujifungua.

Baada ya kufika hospitalini hapo na kufanyiwa vipimo daktari alibaini Filomena ana dalili ya uzazi pingamizi hivyo alielekeza apelekwe Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo kwa ajlili ya kufanyiwa upasuaji.

Ilipofika Mei 18, 2026 majira ya saa 8:00 usiku Filomena alihamishiwa Hospitali yaWilaya ya Bagamoyo ambapo saa 8:30 usiku alijifungua mtoto wa kiume kwa njia ya upasuaji na alieleza kuwa alimuona mtoto wake na kumbeba akiwa mzima wa afya.

Filomena Richard alieleza kuwa baada ya kupewa huduma na kwenda wodini alioneshwa picha za mtoto kwenye simu ya daktari na kuambiwa ndiye mtoto wake na ameshafariki.

Mtoto aliyeoneshwa kwenye picha
alikuwa na changamoto kama vile kichwa kubonyea na kuwa na uvimbe kifuani tofauti na mtoto wake aliyembeba baada ya kujifungua.

Baada ya kuoneshwa picha hizo aliambiwa na daktari kuwa mwili umekabidhiwa kwa ndugu zake ambao ni Avetha Mabadiliko na shangazi
yake aitwaye Adora Mathias kwa ajili ya mazishi.

Mtoto huyo alizikwa bila uwepo wa Filomena Richard ambaye ni mama wa mtoto wala baba wa mtoto hakufahamishwa kuhusu mazishi hayo.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linaendelea na uchunguzi zaidi wa kitaalamu na kisayansi ili kubaini ukweli wa taarifa hiyo.

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *