NAHODHA wa Simba, Shomari Kapombe ameweka wazi mikakati waliyonayo katika mechi tano zilizosalia, zilizobeba maamuzi ya kuchukua ama kudondosha ubingwa waliyoukosa kwa misimu minne mfululizo.
Simba imebakiza mechi dhidi ya Pamba Jiji, Mbeya City, Mtibwa Sugar, Singida Black Stars na KMC, jambo ambalo Kapombe alikiri siyo rahisi lakini wamejipanga kuhakikisha hawadondoshi pointi na kila mechi kwao ni muhimu kuiwekea umakini wa hali ya juu.
“Hatutaki yajirudie ya msimu uliyopita, ambapo tulikosa ubingwa mechi ya mwisho dhidi ya Yanga, hilo lilimuumiza kila mtu na natambua mashabiki wanatamani kicheko na wamechoka kutaniwa na watani wao, ninaloweza kuwaambia wajitokeze kila mechi ili pointi 15 zilizopo nje tuzivune kwa pamoja,” amesema Kapombe na kuongeza;
“Natambua tumezidiwa pointi mbili na Yanga, hilo haliwezi kutupa presha tunachotakiwa kukifanya nikuendelea na mapambano ya kazi ngumu iliyopo mbele yetu, tukishinda mechi zote hilo litaondoa presha bila kujali wapinzani wetu watafanya kitu gani.”
Msimu uliyopita Simba ilikosa ubingwa baada ya kufungwa na Yanga mabao 2-0 waliyofunga mabao hayo walikuwa ni Pacome Zouzoua kwa penati na Clement Mzize, Wanajangwani walimaliza na alama 82 na Wanamsimbazi walimaliza na pointi 78.
Amesema Simba ya msimu huu ina mabadiliko kutokana na ongezeko la wachezaji kama Libasse Gueye ambaye ana mabao sita,Anicet Oura mabao manne hao ni baadhi, wameongeza nguvu ya timu kuwa ya ushindani zaidi.
Kapombe aliporejea Simba Simba Julai Mosi, 2017 akitokea Azam FC, alikuwa kati ya wachezaji ambao waliisaidia timu hiyo kunyakua mataji mara nne mfululizo msimu wa 2017/18 2018/19, 2019/20 na 2020/21, jambo analolitamani litokee katika msimu huu, jambo ambalo amesema:
”Kuna wachezaji hawajachukua ubingwa wanatamani sana kuona wanaandika rekodi hiyo”.
Kwa mara ya kwanza Kapombe kucheza Simba ilikuwa 2011-2013 kisha akatimkia Ufaransa kwenda kujiunga na Cannes, kisha akarejea tena nchini na kutua Azam kuanzia msimu wa 2014-2017.
Imeandaliwa na Olipa Assa, Nevumba Abubakar na Daudi Elibahati.