Dar es Salaam. Mwaka 1961, Tanganyika ilikuwa tajiri kuliko Singapore. Pato lake la Taifa (GDP) lilikuwa takriban dola bilioni 2.82 (zaidi ya Sh7.3 trilioni), huku pato la mtu mmoja likiwa karibu dola 285 za Marekani (zaidi ya Sh741,000).
Singapore, ambayo kwa wakati huo ilikuwa sehemu ya Shirikisho la Malaysia, ilikuwa na GDP ya takribani dola milioni 765 (zaidi ya Sh1.9 trilioni), ingawa uchumi wake tayari ulianza kukua kwa kasi ya wastani wa asilimia 8.1 kwa mwaka.
Hata hivyo, ndani ya miaka michache, mwenendo wa uchumi wa Tanganyika ambayo baadaye iliungana na Zanzibar na kuwa Tanzania ulianza kuwa chini ya Singapore, hasa baada ya Taifa hilo la Asia, kupata uhuru wake mwaka 1965.
Leo hii, Singapore ni miongoni mwa miamba ya uchumi wa viwanda duniani, ikiwa na GDP inayokadiriwa kufikia takribani dola bilioni 659.5, huku pato la mtu mmoja likizidi dola 107,000 (zaidi ya Sh278.9 milioni).
Kwa upande wa Tanzania, uchumi wake kwa sasa unakadiriwa kufikia takribani dola bilioni 90, huku pato la mtu mmoja ni karibu dola 1,300 (zaidi ya Sh3.38 milioni), ikipitwa mbali na Singapore.
Mapinduzi hayo ya uchumi kwa Singapore, ndiyo yaliyochochea kufanyika kwa mhadhara ambao Rais wa Taifa hilo, Tharman Shanmugaratnam, aliwahutubia wasomi, wanafunzi na Watanzania kwa ujumla katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) jana Jumanne, Juni 9, 2026.
Katika hotuba yake hiyo, iliyojikita kuonyesha vikwazo na njia za utatuzi wa maendeleo ya Afrika, Rais Shanmugaratnam amesema nchi za bara hilo zina nafasi ya kujinasua kiuchumi iwapo zitaimarisha uwezo wa kukabiliana na changamoto za ajira, elimu, nishati, biashara na utawala bora.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Juni 9, 2026 kwa ziara ya Kitaifa.
Vinavyoikwaza Afrika
Rais Shanmugaratnam, aliyewasili nchini kwa ziara ya siku tatu jioni ya Jumatatu, Juni 8, 2026, amesema Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa ya idadi ya vijana wanaoingia kwenye soko la ajira.
“Benki ya Dunia inakadiria kuwa vijana milioni 500 wa Afrika wataingia kwenye nguvu kazi katika miaka 10 ijayo, lakini ni milioni 165 pekee wanaotarajiwa kupata ajira. Pengo la watu milioni 335 halijawahi kushuhudiwa katika historia ya dunia,” amesema.
Amesema hali hiyo inaweza kusababisha kupotea kwa matumaini kwa mamilioni ya vijana na kuathiri uchumi pamoja na utulivu wa jamii.
Mkuu huyo wa nchi, amesema ajira bora zinapaswa kuwa kipimo cha mafanikio ya maendeleo ya nchi.
“Ajira lazima ziwe kipimo cha kama ukuaji wa uchumi una maana kwa wananchi au la. Serikali na jamii zinapaswa kuelekeza nguvu zake katika kuzalisha ajira,” amesema.
Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan akiwa na mgeni wake Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam kwenye mkutano na waandishi wa habari leo Juni 9, 2026, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Mabadiliko ya ulimwengu
Rais Shanmugaratnam, amesema mazingira ya kimataifa yamekuwa magumu zaidi kwa Afrika ikilinganishwa na yale yaliyokuwepo wakati nchi za Asia Mashariki zilipoanza safari ya viwanda.
Amesema mabadiliko ya kanuni za biashara ya kimataifa, teknolojia ya akili unde (AI) na mabadiliko ya tabianchi ni baadhi ya vikwazo vipya vinavyoikabili Afrika.
“Kanuni za biashara na uwekezaji wa kimataifa zimebadilika na kuwa mbaya zaidi kuliko ilivyokuwa wakati Asia Mashariki inaanza safari ya uchumi wa viwanda. AI pia itabadilisha karibu kila sekta; itafuta baadhi ya ajira na kuunda nyingine mpya,” amesema.
Hata hivyo, amesema changamoto hizo zinaweza kubadilishwa kuwa fursa kupitia mageuzi ya elimu, uwekezaji na sera za maendeleo.
Amesema Afrika imepata nafasi ya kujenga mfumo wa elimu unaozingatia zaidi stadi za vitendo na mahitaji ya soko la ajira.
“Afrika inaweza kujenga mfumo wa elimu ya juu unaolenga uwezo na ujuzi badala ya vyeti. Inaweza kuwekeza katika vyuo vya ufundi na taasisi za mafunzo ya kiufundi zenye ubora,” amesema.
Pia, amesema Waafrika milioni 600 hawana umeme, lakini hali hiyo inaweza kuwa fursa ya kuwekeza katika nishati jadidifu.
“Waafrika milioni 600 hawana umeme. Hilo ni tatizo, lakini pia ni fursa ya kufikia usalama wa nishati kupitia mchanganyiko wa nishati jadidifu. Uwekezaji katika nishati jadidifu unaweza kuwa chanzo cha ajira,” amesema.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mazungumzo na ujumbe wa Singapore uliongozwa na Rais Tharman Shanmugaratnam.
Mgawanyiko wa masoko
Rais Shanmugaratnam, amesema ukuaji wa uchumi wa Afrika unakwamishwa na masoko madogo na yaliyogawanyika ambayo hayatoi fursa ya kuongeza uzalishaji na tija.
Amesema utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) unapaswa kuharakishwa ili kuunda soko kubwa la uzalishaji na uwekezaji.
“Masoko ya Afrika ni madogo mno na yamegawanyika. Hayatoi ukubwa unaohitajika kukuza uzalishaji na kuongeza tija. Utekelezaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika unapaswa kuharakishwa,” amesema.
Umuhimu wa utawala bora
Pamoja na hayo, amesema mafanikio ya Afrika yatategemea ubora wa utawala, sheria na taasisi zake.
Akirejea utafiti wa Shirika la Fedha Duniani (IMF), amesema nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara zikipunguza kwa nusu pengo la viwango vya utawala bora kati yake na mataifa mengine yanayoibukia kiuchumi, pato la uchumi linaweza kuongezeka kwa asilimia 20 ndani ya miaka mitano hadi 10.
“Utawala bora, uthabiti wa sera, uwazi wa taasisi na utawala wa sheria ndiyo msingi wa mageuzi ya muda mrefu ya uchumi. Haya yanawapa wawekezaji uhakika, yanahamasisha uzalishaji wa ajira na kujenga imani kwa wananchi,” amesema.
Amesema mafanikio ya Afrika hayatategemea wingi wa rasilimali zake bali uwezo wa kugeuza changamoto kuwa fursa kupitia uwekezaji katika watu, ujuzi, nishati, biashara ya kikanda na taasisi imara.
Afrika itumie rasilimali zake
Akijibu swali kuhusu namna taasisi za fedha za Singapore zinavyoweza kusaidia kuziba pengo la mitaji kwa wafanyabiashara wa Tanzania, Shanmugaratnam amesema Afrika inapaswa kuongeza ukusanyaji wa rasilimali za ndani na kudhibiti upotevu wa mapato.
“Dunia imebadilika. Tuko katika hali ambayo kiwango cha misaada kitakuwa kidogo kuliko ilivyokuwa zamani. Afrika ina nafasi ya kuongeza rasilimali zake za ndani na kudhibiti upotevu wa mapato,” amesema.
Amesema serikali zinapaswa kuelekeza fedha katika elimu, afya na miundombinu huku sekta binafsi ikipewa nafasi kubwa ya kuwekeza.
“Sekta ya umma inapaswa kutoa huduma za umma, si kufanya yale ambayo sekta binafsi inaweza kufanya. Rasilimali nyingi za kukuza uchumi lazima zitokane na sekta binafsi,” amesema.
Hata hivyo, amesema Afrika pia inakabiliwa na mfumo wa kifedha wa dunia unaofanya nchi zake kukopa kwa gharama kubwa.
“Afrika inakabiliwa na gharama kubwa mno za ukopaji na viwango vya juu vya riba. Hata ukilinganisha na hatari halisi zilizopo, viwango hivyo haviwezi kuelezwa kwa misingi ya ufanisi wa soko pekee,” amesema.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Singapore, Tharman Shanmugaratnam mara baada ya kuwasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Jumanne Juni 9, 2026 kwa ziara ya Kitaifa.
Kuhusu PPP
Akijibu swali kuhusu uzoefu wa Singapore katika ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), amesema mafanikio yake huanza kwa serikali kujikita katika majukumu yake ya msingi na kuunda mazingira yanayovutia uwekezaji.
Amesema serikali zinapaswa kuelekeza rasilimali katika elimu, afya, utafiti na miundombinu huku sekta binafsi ikiendesha uwekezaji unaochochea ukuaji wa uchumi.
“Rasilimali nyingi zinazohitajika kukuza uchumi lazima zitokane na sekta binafsi. Ili hilo litokee, unahitaji kanuni zinazotabirika, utawala unaotabirika na mtazamo wa muda mrefu,” amesema.
Amesema mazingira yenye uhakika wa sera na utawala bora huwapa wawekezaji ujasiri wa kuwekeza mitaji yao katika miradi ya maendeleo.
“Tunapaswa kutoa mazingira yanayoruhusu sekta binafsi kuwekeza na kuwezesha uchumi kukua. Huo ndio msingi wa kuvutia mitaji ya muda mrefu kwa maendeleo,” amesema.
Tanzania yajifunza Singapore
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema Tanzania inaitazama Singapore kama mfano wa mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana kupitia maono ya muda mrefu, uwekezaji katika watu na matumizi ya teknolojia.
Amesema pato la mtu mmoja nchini Singapore limefikia zaidi ya dola 100,000 kwa mwaka, huku Tanzania kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ikilenga kufikisha pato hilo hadi dola 7,000 ifikapo mwaka 2050.
Balozi Kombo, amesema uzoefu wa Singapore katika sayansi na teknolojia, mageuzi ya kidijitali, utafiti na usimamizi wa uchumi ni muhimu kwa Tanzania.
“Tanzania inatarajia kujifunza kutoka Singapore namna ilivyofanikiwa kutumia sera, taasisi imara na ushirikiano na sekta binafsi kujenga uchumi unaoshindana kimataifa,” amesema.