Unguja. Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar imekiri kuwapo kwa mapungufu katika awamu ya kwanza ya ugawaji wa boti za uvuvi (fiberglass), ikieleza kuwa maoni na mahitaji ya wavuvi hayakuzingatiwa kikamilifu wakati wa maandalizi ya mradi huo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Juni 10, 2026, na Naibu Waziri wa Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Mboja Ramadhan Mshenga, wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Chumbuni (CCM), Makame Mohamed Sufiani, katika kikao cha Baraza la Wawakilishi.

Katika swali lake, Makame amesema matayarisho ya boti zilizogawiwa kwa wavuvi katika awamu ya kwanza hayakushirikisha maoni ya watumiaji wakuu wa vyombo hivyo, hali iliyosababisha baadhi ya boti hizo kutokidhi mahitaji halisi ya shughuli za uvuvi.

Kutokana na hali hiyo, amehoji Serikali imejipangaje kuhakikisha wavuvi wanashirikishwa katika awamu zijazo ili kuepusha changamoto zilizojitokeza hapo awali.

Akijibu, Mshenga amesema Serikali inatambua changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo na imejifunza kutokana na uzoefu huo.

“Ni kweli kulijitokeza changamoto katika zoezi la awali la ugawaji wa boti hizo katika awamu ya kwanza. Serikali imezipokea changamoto hizo na itachukua hatua za makusudi kuhakikisha wavuvi wanashirikishwa moja kwa moja katika hatua zote za maandalizi na utekelezaji wa miradi kama hii,” amesema.

Amefafanua kuwa katika awamu inayofuata, Serikali imepanga kusambaza boti zenye urefu wa mita 14 katika maeneo ya Chwaka, Ukongoroni na maeneo jirani, huku mafunzo kwa wanufaika wa mradi huo yakianza kutolewa.

Aidha, Naibu Waziri huyo amempongeza Mwakilishi wa Chumbuni kwa ushirikiano wake na wananchi, hususan wavuvi, katika kufuatilia na kuibua changamoto zinazowakabili ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Amesema ushirikishwaji wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha miradi ya maendeleo inaleta matokeo yaliyokusudiwa na kukidhi mahitaji ya wananchi wanaolengwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *