
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) likishirikiana na Jeshi la Kitaifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (Artesh), limetangaza mfululizo wa operesheni za kijeshi za kulipiza kisasi zilizoratibiwa vyema dhidi ya kambi za kijeshi za Marekani katika eneo la Asia Magharibi.
Katika taarifa zilizotolewa mapema Alhamisi, operesheni hizo zimeelezwa kuwa ni jibu dhidi ya uchokozi wa Marekani uliolenga maeneo mbalimbali hasa kusini mwa Iran. IRGC imesema kuwa Kikosi chake cha Anga na kile cha Wanamaji vilitekeleza operesheni hiyo ya kulipiza kisasi kwa mawimbi mawili tofauti, ikiwa ni jibu kwa mashambulizi dhidi ya vituo vya ulinzi wa pwani vya IRGC, vitengo vya huduma, vituo vya usalama, na eneo la uwanja wa ndege wa Bandar Abbas. Taarifa hiyo ilieleza kuwa: “Malengo muhimu kumi na nane ya jeshi la kihalifu la Marekani yamepigwa na kuharibiwa katika kambi za anga za Ali al-Salem na Ahmad al-Jaber nchini Kuwait, pamoja na kambi ya anga ya Sheikh Isa nchini Bahrain,”
Wakati huo huo, Ofisi ya Uhusiano wa Umma ya Jeshi la Iran imeripoti operesheni ya droni iliyolenga makao makuu ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji wa Marekani (US Fifth Fleet) nchini Bahrain.
Aidha, IRGC imesema imerusha makombora 12 ya balistiki katika kambi ya jeshi la anga ya al-Azraq nchini Jordan inayotumiwa na Marekani, ikiwa ni jibu kwa mashambulizi ya makombora yaliyofanywa na Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Katika taarifa nyingine siku ya Alhamisi, IRGC imesema kuwa Kikosi chake cha Anga kimelenga eneo la kuegeshea ndege za kivita za Marekani aina ya F-35, F-15, na F-16 pamoja na miundombinu muhimu ya “jeshi la kigaidi la Marekani” iliyopo katika kambi hiyo na kituo cha amri na uratibu. Shambulio hilo la makombora limeharibu vifaa vya kambi hiyo na idadi kubwa ya ndege za kivita. IRGC imeonya kuwa operesheni hizo zitaendelea iwapo adui ataendeleza uchokozi wake. Operesheni hizo za kijeshi za Iran za kulipiza kisasi zimekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuamuru duru mpya ya uchokozi dhidi ya Iran usiku wa kuamkia leo, ikiwa ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutumika tarehe 8 Aprili. Trump aliiambia Fox News kuwa vikosi vya Marekani vimerusha makombora 49 ya Tomahawk katika mashambulizi hayo ya hivi karibuni.