
Afrika itaandika historia katika Kombe la Dunia la FIFA 2026 kwa kuwakilishwa na timu 10, ikiwa ni idadi kubwa zaidi kuwahi kufikiwa na bara hilo katika mashindano hayo.
Mashindano hayo yanaanza Alhamisi nchini Amerika Kaskazini, ambapo Afrika Kusini itakutana na wenyeji wenza Mexico katika mechi ya ufunguzi. Kwa mara ya kwanza, Afrika itakuwa na uwakilishi wa timu za tarakimu mbili katika jukwaa kubwa zaidi la soka duniani.
Timu zitakazopeperusha bendera ya bara hilo katika mashindano yaliyopanuliwa hadi timu 48 nchini Canada, Mexico na Marekani ni: Algeria, Cape Verde, Côte d’Ivoire, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Misri, Ghana, Morocco, Senegal, Afrika Kusini na Tunisia.
Huu ni wakati wa kihistoria kwa soka la Afrika, ukija miaka minne baada ya Morocco kuwa timu ya kwanza kutoka Afrika kufika nusu fainali ya Kombe la Dunia katika Qatar 2022.
Kuongezeka kwa uwakilishi huu kunalipa bara hilo fursa pana zaidi ya kujenga juu ya mafanikio hayo na kusonga mbele zaidi katika mashindano kuliko ilivyowahi kushuhudiwa hapo awali.
Sasa Afrika ina fursa nyingine ya kuonyesha kwamba nafasi yake katika Kombe la Dunia haikui kwa idadi pekee, bali pia kwa kiwango cha matarajio na azma.
Hata hivyo, ushiriki wa Afrika umekumbwa na utata baada ya mwamuzi wa Kisomali, Omar Abdulkadir Artan, kukosa fursa ya kuchezesha katika Kombe hili la Dunia baada ya Marekani kumzuia kuingia nchini humo.
Artan, ambaye ni miongoni mwa waamuzi bora wa Afrika na yumo katika orodha ya waamuzi 52 wa Kombe la Dunia ya FIFA, “alibainika kutoruhusiwa kuingia kutokana na masuala ya uhakiki wa kiusalama na hivyo akanyimwa ruhusa ya kuingia.” Rais Trump wa Marekani amekuwa akitoa matamshi ya kibaguzi na chuki dhidi ya Somalia na Wasomalia na hiyo imetajwa kuwa sababu kuu ya kuzuiwa refa hiyo maarufu barani Afrika
Marekani pia imekabiliwa na lawama kwa kuidalilisha timu za Senegal katika ukaguzi wa kiusalama wakati timu hiyo ilipowasilia katika uwanja wa ndege.
Zaidi ya robo ya nchi zinazoshiriki katika Kombe la Dunia, nyingi zikiwa ni za Afrika, zinaathiriwa na vizuizi vya kusafiri na pia zinakabiliwa na viwango vya juu vya kukataliwa kwa visa za maafisa na mashabiki.
Aidha Kutokana na changamoto za visa na mvutano wa kisiasa unaoendelea, timu ya taifa ya Iran imelazimika kuweka kambi nchini Mexico.
Mechi zote tatu za Iran katika hatua ya makundi zitachezwa nchini Marekani, lakini kwa hali isiyo ya kawaida, wachezaji na maafisa wa timu hiyo watalazimika kuingia na kutoka nchini humo siku hiyohiyo ya kila mechi kutokana na vizuizui vilivyowekwa na utawala wa Trump.