
Kundi la wadukuzi wanaopinga uvamizi wa kivita wa Marekani limetangaza kwamba limedukua vituo vya maji vya California kama kulipiza kisasi cha moja kwa moja kwa shambulio la anga la Marekani lililoharibu maghala ya maji ya kunywa kusini mwa Iran.
Kundi hilo linalojulikana kama Handala, limesema kwamba limelenga miundombinu ya maji ya California baada ya vikosi vya jeshi la Marekani kushambulia maghala mawili ya kuhifadhia maji huko Sirik, mji ulioko katika jimbo la Hormozgan, na kukatisha upatikanaji wa maji ya kunywa kwa zaidi ya wakazi 20,000.
“Siku mbili tu zilizopita, [Trump] aliharibu vyanzo vya maji vya watu wa Sirik kwa makombora ya mamilioni ya dola, na kusababisha ukosefu wa maji na mateso katika joto la nyuzi joto 50,” Handala imesema katika taarifa yake na kuongeza: “Leo, adhabu imefika kwenye moyo wa Marekani.”
Kundi hilo limesema limejizuia kukata maji kwa miji ya Marekani — uwezo ambao limesema linao — likitaja kanuni tofauti za maadili kuliko hasimu wake, (Marekani).
“Tungeweza kukata maji kwa urahisi kwenye miji ya Marekani kama alivyofanya rais wenu mpumbavu, lakini njia yetu na maadili yetu ni tofauti,” imeongeza taarifa ya Handala.
Kundi hilo la wadukuzi limesema hatua hiyo ilikuwa onyo kwa Ikulu ya White House.
“Huu si mwaka wa 2010, ambapo ungeweza kushambulia kwa Stuxnet na usipate madhara yoyote. Leo, kila shambulio litakabiliwa na shambulio na pigo kubwa zaidi kwa miundombinu yako mwenyewe ndani ya saa chache,” imesisitiza taarifa hiyo.
Shambulizi la Marekani dhidi ya mifumo ya usambazaji maji huko Sirik, kusini mwa Iran, limekabiliwa na lawama na ukosoaji mkubwa na kuchochea hatua za kisheria.
Mojtaba Qahramani, mkuu wa mahakama ya mkoa wa Hormozgan, ametangaza kwamba shambulio hilo limesajiliwa rasmi kama kesi ya uhalifu wa kivita, akinukuu Vifungu vya 52 na 54 vya Itifaki ya Kwanza ya Nyongeza ya 1977 ya Mikataba ya Geneva, ambayo inakataza kuharibu miundombinu muhimu kwa maisha ya raia – ikiwa ni pamoja na mifumo ya maji.
Wakati huo huo, gazeti mashuhuri la The New York Times limesema kuwa mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya miundombinu ya maji kusini mwa Iran yanaweza kuhesabika kama uhalifu wa kivita, kwani kulenga miundombinu ya kiraia ni kinyume kabisa na sheria za kimataifa.
Uchambuzi uliofanywa na gazeti la The New York Times kupitia picha za satalaiti na video zilizotolewa na mamlaka za mkoa umehitimisha kuwa kitendo cha Marekani kulenga miundombinu hiyo ya maji kinaweza kuhesabiwa kuwa ni uhalifu wa kivita.