Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud leo amelaani hatua ya Israel ya kuitambua rasmi Somaliland, na kuituhumu Tel Aviv kuwa inatumia mzozo kati ya Mogadishu na eneo hilo lililojitenga na Somalia kwa maslahi yake.

Amesema, hatua ya Israel ya kuitambua Somaliland inaashiria moja ya siku za giza zaidi katika historia ya Somalia.

“Tel Aviv inatumia vibaya fursa ya mzozo wa muda mrefu kati ya Mogadishu na Hargeisa,” amesema Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alipohojiwa na Dawan TV, kituo cha habari cha ndani chenye makao yake mjini Mogadishu.

Amesema Mogadishu imezingatia njia mbili zinazowezekana kushughulikia suala la eneo hilo lililojitenga na kwamba imeechagua kufanya mazungumzo na kutafuta njia za ufumbuzi badala ya kutumia nguvu.

Rais Sheikh Mohamud amesema kuwa Somalia haijawahi kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na Israel, na kwamba anaihesabu Israel kama dola vamizi dhidi ya wananchi wa Palestina.

Disemba mwaka jana Israel ililitambua eneo lililojitenga la Somaliland la kaskazini mwa Somalia kama taifa huru.

Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 kufuatia vita vikali vya wenyewe kwa wenyewe. Jamhuri hiyo iliyotangaza kujitenga na Somalia imeanzisha sarafu yake, bendera na bunge, ingawa maeneo yake ya mashariki yameathiriwa na mzozo.

Serikali ya Somalia inautaja uamuzi wa Israel wa kuitambua Somaliland kuwa ni uvunjaji wa mamlaka na umoja wa ardhi ya nchi hiyo.

Nchi mbalimbali za kikanda na kimatafa zilitoa radiamali na mijibizo yao kufuatia hatua ya Israel ya kuitambua rasmi Somaliland huku nchi nyingi zikiitaja hatua hiyo kuwa kinyume na sharia za kimataifa na ni tishio kwa uthabiti wa kikanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *