Dar/Iringa. Wakati aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa amewaomba radhi wananchi kwenye mkutano wa hadhara, ujumbe wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu umewekwa wazi, akitaka mikutano ya hadhara ya Dar es Salaam aachiwe yeye ili aihutubie atakapotoka gerezani.

Msigwa ameomba msamaha huo leo Jumamosi Juni 13, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa, ukiudhuriwa pia na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche.

Msigwa aliyesema wananchi hao ndio waliomweka katika ramani za siasa, amesema alikimbia vita katikati ya matatizo na hakupaswa kukifanya alichokifanya, bali alitakiwa kuangalia mambo kwa picha kubwa ya kutetea haki za wanyonge.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Hech akizungumza na wananchi leo Jumamosi Juni 13, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa.

Baada ya kudumu CCM kwa zaidi ya mwaka mmoja, Mei 23, 2026 Mchungaji Peter Msigwa alirejea katika chama chake cha zamani, Chadema na kupokelewa na kukabidhiwa kadi ya uanachama.

 “Pamnoja na kuwa nilikuwa nimeumizwa, nilitakiwa kuangalia mambo kwa picha kubwa. Picha kubwa ni kuwa sauti ya watu wasiokuwa na sauti. Sina maneno mazuri sana, naomba mniwe radhi,” alisema.

Hakuna maisha magumu kama kuishi kwa wakwe (akiwa CCM), nilikuwa ukweni,” amesema Msigwa.

Mchungaji Msigwa aliyehudumu Jimbo la Iringa Mjini kwa miaka 10 akiwa Chadema, amesema katika Biblia Yesu alikuwa na wanafunzi 12 na kati yao wawili waliteleza kama yeye.

Naomba mnisamehe, nilijali zaidi ego (nafsi), sikuangalia picha pana, naomba niahidi mbele yenu, nitakuwa kama simba aliyepoteza watoto wake kuing’oa CCM.”

Heche: Chadema haitishiki

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche akihutubia mkutano huo amesema chama hicho si cha mfukoni, hivyo hakitishwi na vitisho mbalimbali vinavyotolewa dhidi yake.

Heche amesema miongoni mwa vitisho hivyo ni barua za maonyo na notisi za kutakiwa kujieleza zinazotolewa mara kwa mara na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, akidai Chadema imekiuka taratibu mbalimbali.

Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Hech akizungumza na wananchi leo Jumamosi Juni 13, 2026 katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa.

Amesema si Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa pekee inayotoa vitisho kwa chama hicho, bali pia baadhi ya kauli kutoka Jeshi la Polisi na viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), akimtaja Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, aliyedai kuwa Chadema inapanga kufanya vurugu.

Heche amesema Chadema kwa sasa kinaongozwa na Tundu Lissu na kwamba huu si wakati wa kuichezea Tanzania, bali ni wakati wa kuleta mabadiliko.

Ameeleza kuwa mikutano ya hadhara ya chama hicho imezua hofu ndani ya CCM kutokana na mwamko unaoendelea kujengwa kwa wananchi.

“Huu moto tunaowapelekea si wa kitoto, ndiyo maana kifua chake kinataka kupasuka. Yaani wewe Kihongosi polisi wasijue, wewe ndiye ujue? Chadema inapanga fujo wapi? Vitisho hivi vimekuwa vingi mno, hatutakubali,” amesema Heche.

Kauli ya Heche imejibu madai ya Kihongosi aliyoyatoa leo Juini 13, 2026 alipozungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma, kuwa Chadema imeacha kufanya siasa za kawaida na badala yake imegeuka kuwa kundi la wanaharakati wanaohamasisha vurugu na maandamano.

Katika maelezo yake, Kihongosi alidai kuwa Chadema kinafadhiliwa na watu wa nje kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi, akisisitiza kuwa amani inaweza kupotea kwa muda mfupi lakini kuirejesha ni kazi ngumu.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa Chadema, uliofanyika leo Jumamosi Juni 13, 2026 katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa.

“CCM tunazo taarifa za uhakika kuwa wenzetu wa Chadema wamefanya vikao vya siri kwa ajili ya kuhamasisha vurugu na maandamano. Wana ajenda ya kuvuruga amani ya nchi hii,” alidai Kihongosi.

Akijibu madai hayo, Heche alisema Chadema kimekuwa kikikabiliwa na ufuatiliaji mkubwa wa kauli na shughuli zake.

“Kila kauli tunayoizungumza Msajili anaikagua. Tukisema hivi, barua; tukigeuka hivi, barua. Mnataka nini kwa Chadema? Mlidhani chama hiki ni kama vyama vya mfukoni vinavyoendeshwa kwa rimoti? Huu ni wakati mwingine,” alisema Heche.

Katika hatua nyingine, Heche amesema Chadema kitaendelea kupigania kuachiwa huru kwa Lissu na madai ya Katiba Mpya, akieleza masuala hayo ndio mambo ya msingi yatakayosaidia kurejesha haki, usawa na utulivu wa kisiasa nchini.

Amesema chama hicho kinaamini kuwa Tanzania haiwezi kupata maendeleo ya kweli bila kuwepo kwa mifumo inayolinda haki za wananchi na kuhakikisha taasisi za umma zinafanya kazi kwa uhuru na kwa mujibu wa sheria.

“Ili nchi hii itulie na iwe sawa, tunahitaji mambo mawili makubwa; kwanza Free Lissu, yaani Tundu Lissu aachiwe huru na pili katiba mpya itakayosaidia kuendesha nchi kwa haki, amani na maendeleo ya wananchi wote,” amesema Heche.

Heche amesema hali ya kisiasa iliyopo imewafanya baadhi ya wanachama wa Chadema kuishi katika mazingira ambayo hayaakisi usawa wa uraia na haki za msingi.

“Watu waliopo Chadema leo wanaishi kama si Watanzania na hiki si kitu cha afya kwa jamii yetu na kwa mustakabali wa nchi,” amesema Heche.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano wa Chadema, uliofanyika leo Jumamosi Juni 13, 2026 katika Uwanja wa Mwembetogwa mjini Iringa.

Amesema chama hicho hakitanyamaza katika kudai haki za wananchi na kupigania mageuzi ya kisiasa yanayolenga kujenga taifa lenye usawa kwa wote.

Heche amesema hadi sasa zimepita siku 430 tangu Tundu Lissu akamatwe katika kesi ambayo Chadema inaamini haina uhalali.

“Hatuwezi kuacha kuzungumzia jambo hili kwa sababu linagusa haki za msingi za wananchi,” amesema Heche.

Aidha, Heche amesema licha ya vikwazo mbalimbali vilivyowahi kuwekwa dhidi ya mikutano ya chama hicho, wananchi wameendelea kujitokeza kwa wingi kusikiliza sera na hoja za Chadema.

“Walituzuia katika maeneo mengi tusifanye mikutano, lakini sasa mikutano imeanza na watu wanaitikia kwa wingi na hii inaonyesha wananchi wana kiu ya kusikiliza na kushiriki katika masuala ya nchi yao,” amesema Heche.

Agizo la Lissu

Wakati huohuo, chama hicho kimeeleza kwa umma agizo la Lissu kwa viongozi wa chama hicho, akiwataka kuacha kufanya mikutano ya kisiasa mkoani Dar es Salaam na kumwachia jukumu hilo yeye atakapotoka gerezani.

Lissu, ambaye ametimiza mwaka mmoja gerezani tangu alipokamatwa Aprili 9, 2025 mjini Mbinga mkoani Ruvuma na yuko mahabusu akikabiliwa na kesi ya uhaini ambayo haina dhamana.

Maelekezo ya Lissu yamesemwa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, John Mnyika kwenye mkutano wa Chama hicho wilayani Kibaha, Mkoa wa Pwani leo Jumamosi June 13, 2026.

Mnyika amesema kiongozi huyo ametuma salamu hizo maalumu zilizoamsha shangwe kwa wafuasi wa chama hicho.

“Mwenyekiti Tundu Lissu kule gerezani, ametuletea salamu kuwa tunapoendelea na operesheni Katiba Mpya, Free Tundu Lissu twende maeneo mbalimbali ya nchi, lakini Dar es Salaam tuisubirishe kidogo, ili akitoka yeye aje kupiga mkutano wa hadhara Dar es Salaam.

“Kwa sababu hiyo, hiki kijiwe cha Maili Moja acha nisikizindue, ili yeye akitoka aje akizundue,” amesema Mnyika.

Mnyika ameeleza sababu ya kumwachia Lissu uzinduzi wa kijiwe hicho cha Maili Moja kama ni heshima ya kumbukumbu kwake, alivyowahi kuibua mjadala wa wafuasi wa chama hicho mwaka 2020, alipozuiwa kufanya mkutano eneo hilo.

“Mnakumbuka mtiti wa 2020 ikawekwa kambi pale, kwa heshima hiyo kijiwe cha Maili Moja nakiacha hadi akija yeye atakizindua,” amefafanua.

Kumshikilia kunaongeza hasira

Akizingumzia ajenda ya Free Tundu Lissu, Mnyika amesema kuendelea kushikiliwa kwa kiongozi wao huyo kunaongeza hasira za wananchi, jambo ambalo si jema.

Amesema hasira zikizidi hupelekea matukio ya uvunjifu wa amani akikumbushia vurugu Oktoba 29, 2025 ambazo amesema zilichochewa na hasira za wananchi waliokosa majawabu ya madai yao.

“Hasira ina kawaida ya kujaa. Chupa ya hasira ikijaa na ikawa wazi huwa ina kawaida ya kutoka kwa namna yake au kuanguka.

Amesema madai ya Katiba tangu mwaka 1992, migogoro ya kisiasa Zanzibar, mauaji ya watu, migogoro ya uchaguzi na kuwa miongoni mwa mambo yaliyochochea hasira za watu.

“Hasira hizo, zikajidhihirisha Oktoba 29, badala ya kutibu hasira kwa kushughulikia waliosababisha hasira hizo, wanaongeza hasira zaidi kwa kumshikilia Tubdu Lissu,” amesema.

Mnyika naye amesema kuwa ajenda namba moja ya chama hicho ni Katiba Mpya, ikifuatiwa na Free Tundu Lissu, ili kupigania mageuzi ya sheria nchini

Mnyika amesema, wamekubaliana na Lissu kusimamia ajenda zao muhimu.

“Nimezungumza naye Lissu, amesema ajenda yetu iwe kupigania ajenda ambazo zilimfanya akamatwe badala ya kumpigania yeye,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *