
Dodoma. Mbunge wa Ngorongoro, Yannick Ndoinyo amesema ushirikishwaji wa wananchi na kusikilizwa kwa maoni yao, ndiyo njia itakayomaliza changamoto zinazoikabili Ngorongoro, badala ya kutegemea uhamishaji wa watu pekee.
Ndoinyo amesema wananchi wengi wa wilaya hiyo hawataki kuhama kutoka maeneo yao ya asili, licha ya kuunga mkono juhudi za uhifadhi zinazoendelea katika eneo hilo.
Amesisitiza kuwa kupata suluhu ya kudumu kuhusu hatima ya Ngorongoro kunahitaji mazungumzo ya wazi na kuwashirikisha wananchi katika maamuzi yanayohusu maisha yao na mustakabali wa eneo hilo.
Kauli hiyo imekuja wakati Ngorongoro ikiendelea kuwa kitovu cha mjadala wa kitaifa kuhusu namna bora ya kusawazisha masilahi ya uhifadhi na ustawi wa jamii zinazoishi ndani ya eneo la hifadhi.
Hoja za mbunge huyo zinafanana na yale yaliyobainishwa na tume iliyoundwa kuchunguza mchakato wa uhamishaji wa wananchi katika eneo hilo, ambayo ilieleza kuwa baadhi ya wananchi hawakuwa tayari kuhama na kwamba kulikosekana ushirikishwaji wa kutosha wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Ndoinyo alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa wiki hii katika mahojiano maalumu na Mwananchi jijini Dodoma.
Amesema wananchi wengi wa Ngorongoro wasingependa kuyahama maeneo yao, ingawa wanatambua umuhimu wa kulinda rasilimali za Taifa na wako tayari kushiriki iwapo kutakuwa na makubaliano yenye masilahi kwa pande zote.
Anasema tofauti ya mtazamo kati ya Serikali na wananchi iko katika namna ya kutafuta suluhisho, akisisitiza kuwa ushirikishwaji wa wananchi ungesaidia kupata majibu bora zaidi bila kutumia nguvu au gharama kubwa.
Mbunge huyo amesema wananchi wanaunga mkono uhifadhi, lakini wanaamini maoni yao yanapaswa kusikilizwa na kupewa uzito katika maamuzi yanayohusu mustakabali wao na eneo lao na kuwa mapendekezo yaliyotolewa na tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan yafanyiwe kazi.
Anakiri kuwa ongezeko la watu na mifugo ni moja ya changamoto zinazolikabili eneo hilo, lakini anaona zipo njia mbadala za kukabiliana nazo bila kuwahamisha wananchi kutoka maeneo yao ya makazi.
Ndoinyo anasema jimbo hilo lenye tarafa tatu, kata 28 na vijiji 65 bado lina idadi kubwa ya wananchi, akipinga madai yanayotolewa na baadhi ya watu kwamba wakazi wengi tayari wamehamia Msomera mkoani Tanga, kiasi cha kufanya jimbo hilo kubaki na wanyamapori pekee.
Serikali ifanye nini?
Kwa mtazamo wake, suluhisho kubwa la kupunguza malalamiko ya wananchi wa Ngorongoro ni Serikali kuendelea kuwasikiliza na kuwahusisha wananchi katika maamuzi.
“Serikali haina nia mbaya. Kinachohitajika ni kukaa na wananchi, kusikiliza maoni yao na kuyafanyia kazi. Ngorongoro ina vijana wengi wasomi wenye uwezo wa kutoa mawazo ya kitaalamu na ya kimila ambayo yanaweza kusaidia kupata suluhu endelevu,” anasema.
Anashauri kutengwa kwa maeneo maalumu ya malisho kwa wafugaji ili kupunguza changamoto ya uhaba wa maeneo ya kuchungia mifugo.
Anasema licha ya wananchi kuishi ndani ya eneo la hifadhi, si maeneo yote yanaruhusiwa kutumika kwa shughuli za ufugaji, jambo linalochangia changamoto ya upatikanaji wa malisho.
Maisha ndani ya hifadhi
Kuhusu changamoto za kuishi karibu na wanyama wakali, Ndoinyo anakiri zipo na kwamba kumekuwa na matukio ya vifo na majeruhi kwa binadamu pamoja na mifugo.
Hata hivyo, anasema changamoto hizo zinapaswa kutazamwa kwa mtazamo mpana zaidi.
“Ni kweli madhara yanatokea, lakini si tofauti sana na changamoto nyingine za maisha. Barabara yenye ajali nyingi haifungwi, bali tahadhari hutolewa kwa watumiaji wake. Hivyo ndivyo inavyopaswa kuwa hata katika suala hili,” anasema.
Anadai mara nyingi taarifa kuhusu madhara yanayosababishwa na wanyama hukuzwa kupita kiasi, jambo ambalo hujenga taswira kwamba wananchi wanaishi katika maeneo ambayo hawapaswi kuwepo.
Mifugo kutoka nje ya nchi
Akizungumzia madai ya kuwepo kwa mifugo kutoka nchi jirani ndani ya Ngorongoro, Ndoinyo anayakanusha vikali.
“Hilo halipo kabisa. Sisi tunachunga mifugo yetu wenyewe na ufugaji ni sehemu ya maisha na utamaduni wetu. Labda kama jambo hilo liliwahi kutokea zamani, lakini kwa sasa halipo,” anasema.
Mbunge huyo anasema kabla ya kuingia bungeni aliwahi kuwa diwani kwa vipindi viwili kuanzia mwaka 2010 hadi 2020 kabla ya kwenda Marekani kuendelea na elimu.
Anasema hata akiwa katika baraza la madiwani, walikuwa na msimamo wa kuhakikisha mifugo inayofugwa katika eneo hilo ni ya wananchi wa asili na si ya watu kutoka nje.
Hivyo, anasema propaganda za aina hiyo zimechangia kuficha changamoto halisi za maendeleo zinazowakabili wananchi wa Ngorongoro, ikiwemo uchumi dhaifu na miundombinu duni.
Mbunge huyo anasema wakati mwingine wananchi hulazimika kutumia siku mbili kusafiri kufuata huduma mbalimbali jijini Arusha kutokana na hali ya barabara na umbali wa maeneo hayo.
Maisha ya wananchi
Katika mahojiano hayo, Ndoinyo anasema kiu yake ni kuona maisha ya wananchi wa jimbo hilo yanaendana na uhalisia wa rasilimali zilizopo katika eneo hilo.
“Lakini kwa sasa bado kuna changamoto nyingi na hali inayokatisha tamaa,” anasema Ndoinyo.
Mwanasiasa huyo aliyeingia bungeni mwaka 2025 baada ya kushindwa katika uchaguzi wa mwaka 2020, anasema kazi kubwa bado inahitajika ili kuifikisha Ngorongoro katika kiwango cha maendeleo kinachoonekana katika majimbo mengine.
Anasema hata kabla ya kuchaguliwa kuwa mbunge, alitambua uzito wa jukumu la kuwakilisha wananchi wa jimbo hilo ambalo kwa muda mrefu limeonekana kubaki nyuma kimaendeleo.
“Natambua kazi kubwa iliyo mbele yangu. Ninapaswa kuwa kiungo cha kuwaleta pamoja wananchi na Serikali katika meza ya mazungumzo na kuaminiana. Wananchi waone umuhimu wa uhifadhi, lakini wakati huo huo Serikali itambue masilahi ya watu wanaoishi Ngorongoro,” anasema.
Hata hivyo, anasema mjadala wa kuhamishwa kwa baadhi ya wananchi ulikuwa unahatarisha mipango yake ya maendeleo kwa sababu muda mwingi ulitumika kushughulikia suala hilo.
Anasema kwa sasa hali imeanza kutulia kufuatia ripoti ya tume iliyoundwa kuchunguza suala hilo na kuwasilisha mapendekezo kwa Rais.
Mikakati ya maendeleo
Mbunge huyo anasema ana vipaumbele vinne anavyoamini vitasaidia kuleta mabadiliko katika maisha ya wananchi wa Ngorongoro.
Vipaumbele hivyo ni kukuza uchumi wa wananchi, kuondoa hofu na mashaka kati ya Serikali na wananchi, kusukuma ujenzi wa uwanja wa ndege na kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo.
“Mimi ni mtaalamu wa masuala ya uhifadhi na ardhi. Sitamani kuona uhifadhi ukiharibika. Nina wajibu wa kuhakikisha pande zote zinaelewana ili wananchi waendelee kuishi na kufuga, huku Serikali nayo ikinufaika na rasilimali zilizopo bila kuathiri mazingira,” anasema.
Anasema anaendelea kupigania ujenzi wa barabara za lami kutoka Kigongoni hadi Wazo na kutoka Ludewa hadi Serengeti, ili kufungua fursa za kiuchumi katika eneo hilo.
Kufanikisha miradi hiyo, anasema, itakuwa moja ya hatua muhimu katika kuibadilisha Ngorongoro na kuacha alama ya maendeleo kwa wananchi wake.
Alipoulizwa mbinu atakazotumia kufanikisha ajenda hizo, Ndoinyo anasema mafanikio ya mbunge hayategemei tu hoja zinazotolewa bungeni, bali pia uwezo wa kujenga mahusiano na kufanya mazungumzo ya karibu na wadau mbalimbali.
“Kazi ya ubunge inahitaji mbinu na uwezo wa kujenga hoja. Dakika tano au nane za kuchangia bungeni hazitoshi kutatua kila jambo. Mara nyingi tunafanya mazungumzo ya kina na wahusika mbalimbali na kufikia makubaliano. Nina imani wananchi wataanza kuona matokeo mazuri,” anasema.
Anasema kwa sasa umaarufu wa Ngorongoro unatokana zaidi na uhifadhi wa wanyamapori pamoja na utamaduni wa makabila ya Wamasai, Wahadzabe na Wadatoga ambao wameendelea kuhifadhi mila na desturi zao.
Anasema moja ya malengo yake ni kuhakikisha urithi huo wa kitamaduni unaendelea kulindwa na kuendelezwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.