Polisi walifyatua risasi za moto nje kidogo ya kituo cha matibabu ambapo jamaa za Bobi Wine walikuwa wakitibiwa mnamo Desemba 1, 2020 huko Jinja, Uganda. (picha zinazoonyesha ukandamizaji).

Chanzo cha picha, Getty Images

Barani Afrika, majina yao yamebaki yakiandikwa katika kurasa za historia. Kuanzia Idi Amin, Mengistu Haile Mariam, Omar al-Bashir, Hissène Habré hadi Charles Taylor, viongozi hawa waliiacha alama kubwa katika kipindi cha utawala wao kuanzia miaka ya 1970 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Walipoingia madarakani, wengi wao walitawala kwa mkono wa chuma, wakitekeleza sera za ukandamizaji zilizojumuisha mauaji ya kisiasa, kunyongwa au kuuawa kwa umma, vifungo vya kiholela na matumizi ya mateso katika vituo vya mahabusu.

Katika makala haya ya BBC News Africa inaangazia baadhi ya viongozi ambao tawala zao zilihusishwa na kiwango kikubwa cha umwagaji damu, kwa mujibu wa taarifa za mashirika ya haki za binadamu.

1. Idi Amin Dada (Uganda, 1971 hadi 1979)

h

Chanzo cha picha, Getty Images

Maisha ya Idi Amin yaliwahi kuigizwa katika filamu ya The Last King of Scotland, ambapo mwigizaji Forest Whitaker alicheza nafasi ya dikteta huyo wa Uganda.

Idi Amin aliingia madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa Milton Obote tarehe 25 Januari 1971.

Mara baada ya kutwaa mamlaka, alivunja Bunge, kusimamisha shughuli za vyama vya siasa na kuanzisha mfumo wa utawala wa amri za rais.

Vikosi vya usalama vilipatiwa mamlaka makubwa ya kukamata watu bila kibali cha mahakama na kuwazuilia kwa muda usiojulikana hasa wale waliooneka kutaka kupindua mamlaka.

Ingawa awali kupanda kwake madarakani kulipokelewa kwa matumaini na baadhi ya wananchi, hali ilibadilika haraka baada ya utawala wake kuanza kuhusishwa na ukandamizaji mkali.

Miaka ya mwanzo ya utawala wake ilishuhudia kuuawa kwa viongozi kadhaa mashuhuri, akiwemo Benedicto Kiwanuka, aliyekuwa Rais wa Mahakama Kuu ya Uganda. Alitekwa nyara tarehe 21 mwezi Septemba mwaka 1972 akiwa mahakamani na baadaye kuuawa kutokana na msimamo wake wa kutetea uhuru wa mahakama.

Idi Amin alianzisha mauaji ya hadharani kwa watu waliotuhumiwa kutaka kumpindua. Kwa mujibu wa shirika la Amnesty International, kulikuwa na mauaji ya hadharani ya wanaume 15 mnamo Septemba 9, 1977, pamoja na visa vingi vya watu kutoweka na kuuawa vilivyotekelezwa na vikosi vya usalama.

“Tangu mwaka 1971, idadi kubwa sana ya watu wametoweka nchini Uganda baada ya kukamatwa na vikosi vya usalama,” Amnesty International liliandika katika mojawapo ya ripoti zake.

Watu walikamatwa na vitengo mbalimbali vya usalama ambavyo kwa kawaida vilikuwa vinawapeleka waathiriwa katika makao yao makuu, vituo vya polisi au kambini, maeneo ambayo yaligeuzwa kuwa vituo vya mateso.

“Kambi za kijeshi zilizokuwa katika miji yote ya Uganda zilishuhudia mauaji ya wanajeshi na maafisa wa polisi, hasa kutoka makabila ya Acholi na Langi, katika miaka ya 1971, 1972, 1973 na 1977. Wanachama wa makabila mengine kama Lugbara na Teso pia walipatwa na masaibu hayo,” Amnesty International liliandika.

Maafisa wengi wa ngazi za juu, hasa kutoka makabila ya Acholi na Langi, waliuawa katika kipindi hicho. Hali hiyo pia iliwakumba viongozi wa kidini na waumini, akiwemo Janani Luwum, Askofu Mkuu wa Kanisa la Uganda, Rwanda na Burundi.

“Mwezi Oktoba na Novemba 1977, takribani Wakristo 400 katika eneo la Masaka, wengi wao Wakatoliki, wakiwemo makatekista 37, waliuawa au kukamatwa kiholela na wanajeshi.”

Idara ya State Research Bureau, chombo cha ujasusi kilichokuwa chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa rais, ilihusishwa kwa kiasi kikubwa na mauaji hayo.

Ripoti hizo zinataja kuwepo kwa “mateso ya kimfumo na mauaji ya papo kwa papo yaliyotekelezwa katika maeneo ya porini yaliyotengwa, pamoja na nyumba mbalimbali za watu binafsi zilizotumika kwa madhumuni hayo.”

Kwa mujibu wa Amnesty International, watu waliokamatwa na maafisa hao walikabiliwa na hatari ya kuuawa bila kufikishwa mahakamani, kwa kupigwa risasi au kwa mbinu nyingine za kikatili zilizokuwa zimezoeleka nchini Uganda.

Kwa mfano, mfungwa mmoja angeweza kuamriwa, chini ya tishio la bunduki, kuwaua wafungwa wengine kwa kuwapiga kichwani kwa nyundo, shoka au mhimili wa gari.

Katika mbinu nyingine, wafungwa walipangwa mstari mmoja. Wa kwanza alipewa nyundo ili amuue aliyekuwa nyuma yake, ambaye naye aliuawa kwa zamu, hadi wote walipomalizwa na manusura wa mwisho kupigwa risasi.

Kwa miaka mingi, kulikuwa na ripoti nyingi za miili ya wafungwa kupatikana ikiwa imepondwa mafuvu.

Makadirio ya idadi ya watu waliouawa na utawala wa Idi Amin Dada tangu mwaka 1971 yanatofautiana. Makadirio ya chini yanataja watu 50,000, huku mengine yakikadiria zaidi ya watu 300,000 kuuawa au hata zaidi.

Baada ya kuondolewa madarakani mwaka 1979, Idi Amin Dada alikimbilia nchini Saudi Arabia ambako aliishi uhamishoni hadi alipofariki dunia tarehe 16 Agosti 2003, bila kuwahi kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za uhalifu wake.

2. Mengistu Haile Mariam (Ethiopia, 1977 hadi 1991)

H

Chanzo cha picha, (Photo by Françoise De Mulder/Roger Viollet via Getty Images)

Mwaka 2008, mahakama ya Ethiopia ilimpata Mengistu Haile Mariam na hatia ya mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya ubinadamu, na kumhukumu adhabu ya kifo kwa kunyongwa.

Makosa hayo yalihusishwa na kampeni ya ukandamizaji iliyoitwa “Red Terror” iliyotekelezwa kati ya 1977 na 1978.

Kwa mujibu wa mahakama, zaidi ya watu 2,000 waliuawa, wakiwemo maafisa waandamizi wa serikali, mawaziri na wanandugu wa familia ya kifalme. Takriban watu 2,400 waliteswa.

Maelfu ya watu waliotuhumiwa kuwa wapinzani wa kisiasa walikamatwa, kuteswa au kuuawa. Miili ya baadhi yao ilitupwa mitaani kama njia ya kutia hofu kwa umma.

Mashirika ya haki za binadamu yalieleza kuwa kukamatwa kiholela, mateso, kutoweka kwa watu na mauaji yalikuwa jambo la kawaida katika kipindi hicho.

“Katika kipindi cha miaka 17 iliyopita, maelfu ya watu waliotuhumiwa kuwa wapinzani wa serikali wamezuiliwa kwa muda mrefu bila kufunguliwa mashtaka wala kufikishwa mahakamani, wakiwemo wafungwa wengi wa dhamiri,” liliandika shirika la Amnesty International katika ripoti yake.

Shirika hilo linaeleza kuwa wapinzani wa utawala huo, mara nyingi kutoka makabila ya Watigray, Waeritrea na Waoromo, walikumbwa na ukamataji na kuzuiliwa kiholela, mateso, kutoweshwa kwa nguvu pamoja na mauaji.

Mateso yalikuwa jambo la kawaida wakati wa mahojiano ya uchunguzi, kwa wafungwa wa kisiasa na wahalifu wa kawaida. Kwa mujibu wa Amnesty International, maelfu ya wafungwa wa kisiasa walitoweka kutoka maeneo yao ya kizuizini na inaaminika waliuawa kwa siri.

Mashahidi waliiambia mahakama kwamba jamaa waliokwenda kuchukua miili ya wapendwa wao katika chumba cha kuhifadhi maiti walilazimika kulipia risasi zilizotumika kuwaua.

Shahidi mmoja, Gizaw Tefera, alisimulia kuwa wanajeshi waliomuua baba yake walimkata kichwa na kukipeleka sokoni kwa ajili ya mnada. “Hakuna mtu aliyekuwa tayari kununua kichwa cha baba yangu,” alisema mwaka 2000 wakati wa usikilizwaji wa kesi mahakamani.

Mtaalamu wa uchunguzi wa kisayansi kutoka Argentina, Mercedes Doreth, alisema wakati wa kesi hiyo kuwa baadhi ya mabaki ya miili yaliyofukuliwa kutoka makaburi ya halaiki yalionyesha kuwa waathiriwa waliuawa kwa kunyongwa kwa kamba.

“Tulipata kamba za nailoni za kijani zikiwa zimefungwa kwa nguvu shingoni mwao,” alisema Doreth mwaka 2002.

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani ulijumuisha amri za kunyongwa zilizosainiwa pamoja na video za vipindi vya mateso.

Akiwa hayupo wakati wa kesi yake, Mengistu Haile Mariam, ambaye alikimbilia nchini Zimbabwe baada ya kutoroka mwezi Mei 1991, hakuwahi kurejeshwa nchini Ethiopia kukabili mashtaka.

3. Omar al Bashir (Sudan, 1989 hadi 2019)

H

Chanzo cha picha, SEYLLOU/AFP via Getty Images

Utawala wa Omar al-Bashir ulihusishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na mgogoro wa Darfur, ambapo makumi ya maelfu ya watu waliuawa kati ya 2003 na 2008.

Alifika madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1989 na kuiongoza Sudan kwa karibu miongo mitatu.

Al Bashir anatuhumiwa kwa mauaji ya halaiki dhidi ya makabila ya Fur, Masalit na Zaghawa. Pia anakabiliwa na tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu, ikiwa ni pamoja na mauaji, ubakaji, mateso na kuwahamisha watu kwa nguvu.

Baada ya kuondolewa madarakani mwaka 2019, alizuiliwa nchini Sudan huku akikabiliwa na hati kadhaa za kukamatwa zilizotolewa na mahakama ya ICC kwa tuhuma za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

4. Charles Taylor (Liberia, 1997 hadi 2003)

G

Chanzo cha picha, (Photo by Patrick ROBERT/Sygma via Getty Images)

Charles Taylor alijijengea sifa ya kuwa mmoja wa viongozi waasi wenye nguvu zaidi baada ya kuanzisha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Liberia mwaka 1989.

Kuanzia mwaka 1989 hadi 1997, Charles Taylor aliongoza vuguvugu la waasi la National Patriotic Front of Liberia (NPFL), ambalo lilikuwa likitaka kumuondoa madarakani rais wa wakati huo wa Liberia, Samuel Doe.

Kwa mujibu wa ripoti za mashirika yasiyo ya kiserikali, wanajeshi wa kundi hilo walihusishwa na ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu dhidi ya raia, ukiwemo mauaji ya papo kwa papo bila kesi, mauaji ya halaiki, ubakaji wa kimfumo, ukeketaji wa viungo vya mwili, mateso, uandikishaji wa watu kwa nguvu katika vikosi vya waasi, pamoja na matumizi ya watoto kama wanajeshi.

Charles Taylor alijizolea sifa mbaya zaidi kutokana na ukatili uliofanywa na wapiganaji wake wakati wa vita vya nchi jirani ya Sierra Leone.

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Sierra Leone kati ya mwaka 1991 na 2002, aliliunga mkono kundi la waasi la Revolutionary United Front lililoongozwa na Foday Sankoh.

Katika kipindi hicho, waasi wa RUF walituhumiwa kwa mauaji ya raia, ukatili wa kutisha, kukata viungo vya mwili vya waathiriwa, utekaji nyara na matumizi ya watoto katika mapigano, hali iliyochangia kuifanya vita hiyo kuwa miongoni mwa migogoro ya kikatili zaidi katika historia ya Afrika Magharibi.

Baadhi ya wahanga walilazimishwa kuchagua kati ya kukatwa mkono au mguu.

Taylor alikamatwa nchini Nigeria na baadaye kuhamishiwa Uholanzi.

Mwaka 2012 alihukumiwa kifungo cha miaka 50 gerezani baada ya kupatikana na hatia ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

5. Hissène Habré (Chad, 1982 hadi 1990)

Hissène Habré akitoa ishara anapotoka katika kesi ya utambulisho katika mahakama ya Dakar tarehe 3 Juni 2015.

Chanzo cha picha, (Photo by SEYLLOU/AFP via Getty Images)

Hissène Habré alifariki gerezani mjini Dakar, Senegal, mwaka 2021.

Mwaka 2016, mahakama maalumu ya Afrika ilimpata na hatia ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita, mateso, ubakaji na ukatili mwingine wa kijinsia.

Utawala wake uliendeshwa kupitia idara ya kijasusi iliyojulikana kama DDS, ambayo ilihusishwa na ukandamizaji mkubwa dhidi ya wapinzani wa serikali.

Ripoti ya Human Rights Watch ilibaini kuwa maelfu ya watu walikamatwa kiholela, kuuawa au kuteswa chini ya utawala wake.

Miongoni mwa mbinu za mateso zilizotajwa ni “arbatachar”, ambapo mikono na miguu ya mfungwa ilifungwa nyuma ya mgongo kwa namna iliyokatiza mzunguko wa damu na kusababisha ulemavu wa kudumu.

“Baadhi ya wafungwa wengine walifungiwa vichwa vyao chini ya sahani ya chuma na kubanwa kwa nguvu, walipigwa shoti za umeme au waliteswa kwa kuzamishwa majini,” aliandika.

Tume ya uchunguzi iliyoundwa nchini Chad baada ya Hissène Habré kukimbilia nchini Senegal mwaka 1990 ilikadiria kuwa takribani watu 40,000 waliuawa kwa sababu za kisiasa, huku karibu visa 200,000 vya mateso vikirekodiwa katika kipindi chake cha miaka minane madarakani.

Baada ya kuondolewa madarakani mwaka 1990, Hissène Habré aliishi uhamishoni nchini Senegal kwa miaka mingi kabla ya kufikishwa mahakamani na kuhukumiwa mwaka 2016 kwa makosa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita na mateso.

Kesi hiyo ilihesabiwa kuwa hatua muhimu katika juhudi za kuwawajibisha viongozi wa zamani wa Afrika kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *