Dar es Salaam. “Tulikaa zaidi ya miaka minne ndani ya nyumba moja bila kusemezana.”

Hayo ni maelezo ya mmoja wa wanandoa waliofika katika kliniki ya sheria ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam, wakisaka suluhisho la mgogoro uliowafanya waishi chini ya paa moja kama wageni.

Kwa zaidi ya miaka minne, kila mmoja aliendesha maisha yake bila mawasiliano ya kawaida ya kindoa, hali iliyowafanya waonekane zaidi kama wapangaji kuliko mume na mke.

Kisa hicho ni mfano tu wa visa vingi vinavyoibuliwa katika kliniki za msaada wa kisheria nchini, vikionyesha namna migogoro ya ndoa inavyozidi kuhamia kwenye majukwaa ya sheria badala ya familia, viongozi wa dini au wazee wa mila kama ilivyokuwa zamani.

Katika kliniki hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam, tukio hilo liliwashangaza mawakili waliokuwa wakitoa huduma za ushauri na usuluhishi.

Kupitia usuluhishi uliotolewa chini ya wakili wa Serikali, Fatma Pangalugome, wanandoa hao walikaa pamoja, kueleza malalamiko yao na hatimaye kufikia mwafaka wa kurejesha uhusiano wao.

Mgogoro huo ni mmoja kati ya migogoro 49 iliyofikishwa kwenye kliniki hiyo iliyozinduliwa Februari 16, 2026,  kwa ajili ya kusaidia wakazi  kupata huduma za kisheria bila malipo.

Chanzo cha mgogoro huo, kwa mujibu wa Wakili Fatma, kilikuwa ni ukosefu wa mipaka na heshima ndani ya familia, huku watoto wakubwa wakiingia chumbani kwa wazazi bila utaratibu.

“Baba alisema licha ya kutoa fedha za familia na kusaidia miradi yao, mkewe hakutimiza majukumu yake kikamilifu. Hali hiyo ilisababisha kulala chumba kingine na kusitisha baadhi ya majukumu kama ishara ya kutoridhishwa kwake,” alisema Fatma.

Alisema jambo jingine lililochangia kujitenga na mkewe ni manyanyaso yaliyokuwa yakifanywa kwa mtoto wake wa nje ya ndoa.

Hali kama hiyo ilijitokeza pia mkoani Tanga, ambapo wanandoa walikaa kwa zaidi ya miezi 10 bila kuzungumza wala kupeana talaka, kila mmoja akiendelea na maisha yake licha ya kuwa bado wanaishi pamoja.

Wakati huohuo, katika kampeni ya msaada wa kisheria ya Samia iliyofanyika mkoani Dodoma, ilibainika kuwapo kwa wanandoa waliodumu katika mgogoro wa kimya kwa zaidi ya miaka 13.

Mkazi wa Tanga, Jumbe Mbelwa, anasema hakusemezana na mkewe kwa miezi 10 kutokana na kile anachodai kuwa ni usikilizaji wa maneno ya ndugu na dharau kwa mume.

“Ndoa yetu ilikuwa nzuri awali. Kitendo cha kuruhusu ndugu wa mke wangu kuja mara kwa mara nyumbani kilikuwa tatizo kwani wamekuwa wakimueleza anifuatilie akihisi ninaweza kuwa namsaliti,” anasema.

Anasema hali hiyo ilimkera na kila alipojaribu kuzungumza na mkewe hakupata usikivu zaidi ya kuendelea kuchunguza mawasiliano yake, ikiwamo watu anaofanya nao biashara.

Mbelwa anasema kila alipokuwa akiacha simu, mkewe alikuwa akiichukua na kuipekua kuangalia kama kuna mawasiliano mapya, hali iliyofikia hata hatua ya ugomvi wa mara kwa mara kwa sababu ya kushukiwa mambo ambayo hafanyi.

Kwanini kliniki za sheria?

Mkurugenzi msaidizi wa uratibu kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ipyana Mlilo, anasema uelewa mdogo wa masuala ya kisheria ni chanzo kikubwa cha migogoro ya ndoa.

Anasema mara nyingi wanandoa hukosa ufahamu wa haki na wajibu wao, hali inayosababisha uamuzi wa haraka usio  na uzingatiaji wa athari zake kwa familia.

“Migogoro ya ndoa inatakiwa kufuata ngazi mbalimbali za usuluhishi kabla ya kufikishwa mahakamani, ikiwamo familia, viongozi wa dini na mabaraza ya kata,” anasema Mlilo.

Anasema mara nyingi wamekuwa wakitoa ushauri kwa wanandoa kuanzia ngazi za familia na kidini,  kabla ya kuhamia kwenye masuala ya kisheria kutokana na mlolongo wa usuluhishi wake.

Mlilo anasema hatua ya kisheria huwa ni ya mwisho pale ambapo juhudi za ngazi nyingine zinaposhindikana, huku wao wakitoa ushauri na elimu kwa wanandoa ili kuwasaidia kutafakari uamuzi wao.

“Changamoto kubwa ni baadhi ya wanandoa kutojua taratibu za kisheria… hususan kwenye mali na malezi ya watoto, hali inayosababisha migogoro kuendelea na kuathiri ustawi wa familia, hasa watoto,” anasema.

Swali linaloibuka ni kwa nini wanandoa hawa wanashindwa kusuluhisha migogoro yao kupitia familia au viongozi wa dini, lakini hupata suluhisho wanapofika kwenye kliniki za kisheria?

Wakili William Maganga anasema kliniki hizo zinatoa mazingira tofauti yasiyo na upendeleo, yenye faragha na yanayompa kila mmoja nafasi ya kusikilizwa.

“Mara nyingi hawa watu hawahitaji talaka, wanahitaji mtu wa kati wa kuwawezesha kuzungumza. Hivyo kliniki za kisheria zimekuwa jukwaa hilo,” anasema Maganga.

Anasema kingine kilichochangia kliniki za kisheria kufanikiwa ni mabadiliko ya mfumo wa jadi wa usuluhishi uliokuwa ukitumia wazee wa mila, wakuu wa koo na viongozi wa dini.

“Baadhi ya wanandoa wamepoteza imani kwa familia au viongozi wa dini kutokana na hofu ya upendeleo au kufichua siri zao. Hasa kizazi kipya, wanathamini zaidi faragha na uhuru binafsi,” anasema.

Ustawi wa jamii

Uchambuzi wa matukio hayo unaonyesha kuwepo kwa kile wataalamu wanakiita ‘ndoani lakini si ndoani’ hali ambayo wanandoa wanakuwan hawajaachana rasmi, lakini pia hawaishi kama wenza.

Kwa mujibu wa Ofisa wa Ustawi wa Jamii jijini Arusha, Japhet Kavishe, hali hiyo inatokana na sababu mbalimbali zikiwamo hofu ya talaka, utegemezi wa kiuchumi na uwepo wa watoto.

“Wengi wanabaki kwenye ndoa si kwa sababu wanafurahia, bali kwa sababu wanaogopa matokeo ya kuachana. Wengine wanahofia athari kwa watoto au mali walizochuma pamoja,” anasema.

Anasema wamekuwa wakipokea malalamiko ya kutokuwapo kwa baadhi ya huduma kutokana na wanandoa kutosemezana kwa muda mrefu.

Anasema wamekuwa wakiitisha vikao vya usuluhishi ambapo mwafaka mkubwa huwa ni kurejesha mawasiliano kati ya pande zote mbili, kukubali makosa, kusamehe na wakati mwingine kutafuta msaada wa kitaalamu mapema kabla hali haijawa sugu.

Mitandao na mafundisho ya dini

Viongozi wa dini wanasema kuongezeka kwa matumizi ya mitandao ya kijamii, pia kumebadilisha namna wanandoa wanavyopokea ushauri kuhusu ndoa na talaka.

Wanasema hivi sasa baadhi ya wanandoa hufuatilia mahubiri, mihadhara na ushauri kupitia majukwaa ya mtandaoni, hali inayowafanya kupata mitazamo tofauti kuhusu kuvumilia au kuachana na ndoa zao.

Sheikh wa Msikiti wa Kigogo Chawote, Abdallah Ally, wanandoa wengi wenye uwezo wa kifedha wanapofika kwenye mabaraza ya usuluhishi au kwa viongozi wa dini,  hupewa maelekezo kuhusu madhara ya talaka, hususan kwa watoto, mali na heshima ya familia.

Kutokana na kuwa na vitega uchumi au mali za pamoja, wengi wao hutafakari zaidi kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho wa kuachana.

Hata hivyo, kwa baadhi ya wanandoa wenye hali ya kawaida, anasema imekuwa rahisi kufikia uamuzi wa kuachana kutokana na kuona hawana mali nyingi za kugawana wala maslahi makubwa yanayowalazimu kubaki pamoja.

“Wengine wakisikiliza mahubiri au ushauri kwenye mitandao wanajikuta wanaongeza uamuzi wao wa kuachana. Kwa wenye uwezo mkubwa kifedha huwa wanatafakari zaidi, kwa sababu wanaangalia athari za mali na watoto, lakini kwa wenye maisha ya kawaida wengine wanaona hakuna kikubwa cha kuwazuia kuachana,” anasema Shekhe Ally.

Kwa upande wake, Kiongozi wa Kanisa la Ufunuo la Buza, Mchungaji Samweli Mwakipesile, anasema mafundisho ya ndoa kuwa ni agano la maisha yote yamekuwa yakifanya baadhi ya wanandoa kushindwa kuvunja ndoa rasmi hata pale wanapokuwa tayari wameachana kihisia na kimwili.

Anasema baadhi ya wanandoa huamini kuwa kwa kuwa mafundisho ya Kikristo yanaeleza kuwa kifo ndiyo kitawatenganisha, hawawezi kutengana rasmi mbele ya kanisa hata kama tayari hawaishi pamoja tena.

Hali hiyo imekuwa ikisababisha migogoro ya muda mrefu ndani ya familia huku baadhi ya wanandoa wakibaki kwenye ndoa kwa jina tu.

“Wapo wanaume na wanawake wanaoondoka au kuishi pamoja bila kuzungumza, wengine hukimbia nyumba, lakini mbele za Mungu na kanisa bado wanahesabika kuwa ni wanandoa. Hata inapotokea msiba wa mmoja wao, bado wanatambulika hivyo hivyo kwa sababu ndoa yao haikuwahi kuvunjwa rasmi,” anasema Mwakipesile.

Anasema hali hiyo imekuwa ikiwasukuma baadhi ya wanandoa kukimbilia vyombo vya sheria kutafuta ufafanuzi wa haki zao, hasa katika malezi ya watoto, matumizi ya mali na uhalali wa uhusiano mpya wanaoingia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *