Accra, Ghana. Serikali ya Ghana imeingilia kati sakata la kiungo wa timu ya taifa ya nchi hiyo, Thomas Partey baada ya Canada kumzuia kuingia nchini humo kutokana na kesi za madai ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono zinazomkabili nchini Uingereza.
Partey ambaye ni mmoja wa nyota muhimu wa Black Stars, amekosa kibali cha kuingia Canada na hivyo hatakuwepo katika mchezo wa kwanza wa Ghana wa Kombe la Dunia 2026, dhidi ya Panama utakaochezwa jijini Toronto.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 32 anakabiliwa na mashtaka saba ya ubakaji na shtaka moja la unyanyasaji wa kingono yanayohusisha wanawake wanne tofauti, kwa matukio yanayodaiwa kutokea kati ya mwaka 2020 na 2022.
Hata hivyo, Partey amekana mashtaka yote na amewasilisha utetezi wake mahakamani.
Katika taarifa rasmi, serikali ya Ghana imeeleza kutoridhishwa na uamuzi wa mamlaka za Canada, ikisema hatua hiyo ni ya haraka na isiyo na usawa kwa kuwa mchezaji huyo hajapatikana na hatia katika mahakama yoyote hadi sasa.
Kiungo wa zamani wa Arsenal, Thomas Partey wakati alipokuwa akishuka kutoka ndani ya gari kuelekea mahakani kwa ajili ya kusikiliza kesi Aprili 13, 2026. Picha na Mtandao
Serikali hiyo imebainisha kuwa tayari imeanza mazungumzo ya kidiplomasia na viongozi wa Canada kwa lengo la kutafuta suluhisho la haraka litakalomwezesha Partey kuungana na wenzake katika mashindano hayo makubwa ya dunia.
“Tunasisitiza kanuni ya msingi ya sheria kwamba kila mtu anapaswa kuhesabiwa hana hatia mpaka pale mahakama itakapothibitisha vinginevyo,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya serikali ya Ghana.
Aidha, Ghana imeahidi kutumia njia zote za kisheria na kidiplomasia kuhakikisha suala hilo linapatiwa tathmini ya haki kwa kuzingatia ukweli wa kesi husika badala ya tuhuma.
Kwa upande wa Canada, sheria za uhamiaji za nchi hiyo zinaeleza kuwa mtu anayehusishwa na makosa ya jinai au aliyewahi kutiwa hatiani anaweza kunyimwa ruhusa ya kuingia nchini humo kulingana na tathmini ya maafisa wa uhamiaji.
Wakati sakata hilo likiendelea, Partey ameendelea kubaki katika kambi ya Ghana iliyopo Boston, Marekani, akisubiri maombi ya serikali ya nchi yake.
Maafisa wa Ulinzi wa Mipaka wa Marekani wameeleza kuwa walifahamu uwepo wa kesi zinazomkabili nyota huyo lakini kwa kuwa hajatiwa hatiani, aliruhusiwa kuingia nchini humo baada ya kupata visa halali.
Kiungo wa zamani wa Arsenal, Thomas Partey, ambaye kwa sasa anaitumikia Villarreal ya Hispania. Picha na Mtandao
Kabla ya kuanza kwa Kombe la Dunia, kocha wa Ghana, Carlos Queiroz, alisisitiza kuwa hakuwa na tatizo lolote kumjumuisha Partey katika kikosi chake, akieleza kuwa suala hilo bado liko mikononi mwa mahakama.
Partey aliitumikia Arsenal kabla ya kuondoka mwishoni mwa msimu wa 2024-25 na baadaye kujiunga na Villarreal mwezi Agosti mwaka jana.
Mbali na mchezo dhidi ya Panama, Ghana pia inatarajiwa kucheza dhidi ya England Juni 23 na Croatia Juni 27 nchini Marekani, mechi ambazo Partey anaweza kushiriki ikiwa ataendelea kubaki nchini humo.
Hata hivyo, endapo Ghana itamaliza nafasi ya pili katika Kundi L na kufuzu hatua ya mtoano, timu hiyo inaweza kurejea Canada kwa mechi za hatua ya 32 bora, jambo ambalo linaweza kuifanya tena suala la Partey kuwa ajenda kubwa katika mashindano hayo.