
Gazeti la Washington Post, katika ripoti yake kuhusu hati ya makubaliano kati ya Iran na Marekani, limekejeli hatua ya Rais Donald Trump wa Marekani ya kusherehekea kurejea Washington kwenye hali ya kabla ya Februari 28, hatua ambayo baadhi ya wataalamu wanaamini ni kurudi nyuma kwa maana halisi ya neno hilo mkabala wa Iran.
Maelewano kati ya Iran na Marekani yamefikiwa wakati ambapo Trump anajaribu kukomesha vita vya gharama kubwa, na licha ya majigambo yake katika siku za mwanzo za vita alivyoanzisha kwa shabaha ya kuangamiza kabisa nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu, sasa anapigania kufungua tena Lango-Bahari la Hormuz ambalo lilikuwa wazi kabla ya kuanza vita hivyo.
Trump alitangaza mwisho wa vita vyake dhidi ya Iran jana Jumapili akisema: “Meli za dunia, sasa zinapaswa kuwasha injini. Acha mafuta yatiririke!”
Kwa msingi huo, gazeti la Washington Post limeandika: Trump anasherehekea kurudi kwenye hali ya kabla ya Februari 28, siku moja kabla ya mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya Iran.
Ripoti hiyo inasema: Kutokana na mapambano ya Iran katika miezi ya hivi karibuni, kumeibuka mgawanyiko mkubwa kati ya Rais wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kiasi kwamba Trump jana alimlaani mbele ya waandishi wa habari wakati wa sherehe ya kutimiza miaka 80 ya kuzaliwa kwake.
Sehemu nyingine ya ripoti ya Washington Post inasema: Kinyume na majigambo yake ya kabla ya vita, Rais wa Marekani hazungumzii tena suala la kuondoa madarakani utawala wa Iran, amejikita katika kufanya mazungumzo na Tehran na anajiondoa katika hatua yoyote ya kijeshi ambayo inaweza kuhatarisha amani, sawa na hali iliyotokea Jumapili alipomkosoa Netanyahu kwa kushambulia kitongoji cha Dahiya nchini Lebanon.
Gazeti la Washington Post limezungumzia pia upinzani wa baadhi ya waungaji mkono wa Trump dhidi ya makubaliano ya Iran, akiwemo Mark Levin, mtangazaji mashuhuri na mchambuzi wa kihafidhina wa Marekani, na vilevile seneta Lindsey Graham ambao wametoa wito wa kuwekwa wazi maelezo ya makubaliano hayo na kuwasilishwa kwenye Kongresi ya nchi hiyo.