Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza haja ya kuimarishwa usitishaji mapigano huko Gaza na kufikiwa makubaliano endelevu ya kusitisha mapigano, akibainisha kuwa vikosi vya jeshi la Israel vimewaua Wapalestina wapatao 1,000 tangu usitishaji mapigano Oktoba mwaka jana, pamoja na kuimarisha vizingiti vya kuzuia misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza, jambo ambalo amesema limezidisha mgogoro wa binadamu katika sekta hiyo.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametoa maoni hayo leo Jumatatu wakati wa ufunguzi wa kikao cha 62 cha Baraza la Haki za Binadamu huko Geneva.

Katika Ukingo wa Magharibi, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kwamba kasi ya kuhamishwa watu kwenye makazi yao, uharibifu wa jamii na unyang’anyi wa ardhi imeongezeka, akieleza kuwa makumi ya watu wameuawa, maelfu wamejeruhiwa na mamia wamekamatwa, huku shughuli za ujenzi wa vikongoji vya walowezi wa kizayuni zikiendelea.

Ameongeza kuwa baadhi ya taarifa zilizotolewa na maafisa wa Israel ni pamoja na wito wa kuwafukuza Wapalestina au kuzuia kuanzishwa taifa huru la Palestina, akielezea jambo hili kuwa ni kinyume cha sheria. Amesisitiza haja ya kuzidishwa mashinikizo ya kimataifa ili kusimamisha mapigano hiyo na kuwawajibisha wale wanaohusika na ukiukwaji huo wa sheria.

Volker Türk pia amezungumzia kuongezeka kwa mapigano kati ya Hizbullah na Israel, mauaji ya raia na vilevile kuhamishwa watu wengi nchini Lebanon, akielezea wasiwasi wake kuhusu mashambulizi yanayolenga miundombinu na maeneo ya makazi. Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kusitishwa mara moja vitendo vya uhasama, kuondoka vikosi vya jeshi la Israel kutoka kwenye ardhi ya Lebanon, na uchunguzi huru kuhusu ukiukaji wote wa sheria uliofanywa na Israel.

Katika upande mwingine, Turk amezungumzia hali ya mambo nchini Sudan, na kuongezeka mgogoro wa nchi hiyo, utumiaji ya ndege zisizo na rubani, na kusajiliwa mauaji ya zaidi ya raia elfu moja katika miezi ya kwanza ya 2026, pamoja na visa vya unyanyasaji wa kingono.

Kwa ujumla, Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu hali mbaya ya haki za binadamu duniani kote, akitaka kuimarishwa sheria za kimataifa na uwajibikaji kwa wale wanaohusika na ukiukwaji wa haki hizo katika maeneo mbalimbali yenye migogoro.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *