Kiungo mkabaji wa Tanzania Prisons, Gustapha Saimon Lunkombi amesema kwamba Ligi Kuu Tanzania Bara inazidi kuwa bora na yenye ushindani mkubwa kutokana na kila timu kuwa na wachezaji bora wenye viwango vya juu.

Nyota huyo ambaye amewahi kuzitumikia klabu kadhaa hapa nchini zikiwemo Yanga na Dodoma Jiji alisema kwa sasa anahitaji kupambana kuhakikisha timu yake ya Tanzania Prisons inabakia Ligi Kuu.

“Kadri ligi inavyozidi kusogea mwisho, inazidi kuwa bora na yenye ushindani na msimu huu ushindani upo juu sana.

“Matumaini yangu kwa sasa ni kuhakikisha timu yangu inabaki sehemu salama ndani ya Ligi Kuu.“

Hata hivyo, timu ya Tanzania Prisons ipo katika nafasi hatari ya kushuka daraja msimu huu iwapo itashindwa kufanya vizuri katika michezo yake iliyosalia.

Kabla ya mechi ya jana dhidi ya Dodoma Jiji, Tanzania Prisons ilikuwa katika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 20.

Pointi 20 ilizokusanya hadi sasa hazitoshi kuinusuru Prisons kubakia katika Ligi Kuu kwani inahitaji pointi zaidi ili kuzipita Namungo na Mbeya City ambazo zipo nafasi ya 13 na 14.

Kutokana na hali ya timu jinsi ilivyo, itawalazimu wachezaji kupambana kadri ya uwezo wao kuhakikisha timu inasalia katika Ligi Kuu.

Kiungo mkabaji wa Tanzania Prisons, Gustapha Saimon Lunkombi wakati alipokuwa katika moja ya mechi za Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar

Changamoto zinazomkwaza

Gustapha ambaye alipitia katika kituo cha kukuzia vipaji kilichopo Magomeni Mikumi, Dar es Salaam cha Kisa Sports Centre, hakuacha kumtaja kocha Mohammed Chiwanga ambaye ndiye alikuwa na mchango mkubwa sana katika safari yake ya soka.

Katika kila safari huwa changamoto hazikosi, Gustapha alieleza changamoto anazokuwa akipitia yeye kama mchezaji.

“Kuhusu changamoto nadhani kwa upande wangu ni pale ambapo timu yangu inapokuwa imepata matokeo mabaya na hata inapotokea nimeshindwa kucheza kwa kiwango changu hizo ndio huwa changamoto kubwa kwangu,” alisema Gustapha.

Kutokana na kupitia changamoto hizo, mchezaji huyo alitoa wito kwa vijana wanaochipukia au wenye ndoto za kuja kuwa wana soka hapo baadaye akiwasisitiza kufanya mazoezi kwa bidii pamoja na nidhamu.

“Ushauri wangu kwa wachezaji wadogo ni kwamba wajitahidi kufanya mazoezi kwa bidii na kuwasikiliza makocha ambao wanawasimamia. Kwa sababu msingi wa mafanikio ya mchezaji ni mazoezini na hakuna kingine,”alishauri Gustapha.

Mafanikio yake

Hata hivyo, kuhusu mafanikio yake ambayo ameyapata kupitia soka alisema kuwa ni mengi na makubwa lakini hakutaka kuyaweka wazi.

“Kuhusu mafanikio ni mengi tu na ni makubwa nimepata kupitia mpira naomba iwe siri yangu hiyo,” alisisitiza mchezaji huyo.

Kiungo mkabaji wa Tanzania Prisons, Gustapha Saimon Lunkombi (kulia) wakati akipiga mpira katika moja ya mechi za Kirafiki

Imani kwa wazawa

Gustapha anaamini wachezaji wazawa wana viwango vya juu na ndio maana wapo idadi kubwa wanaocheza katika klabu kubwa nchini.

“Mimi kwa upande wangu siamini kwamba wachezaji wazawa wanashindwa kutamba ndani ya Simba na Yanga. Kwa sababu wapo wengi wanaofanya vizurii ndani ya klabu hivyo,” alieleza Gustapha.

Kiungo huyo hadi sasa ameichezea Prisons katika mechi saba za Ligi Kuu ya NBC.

Historia tamu

Miaka ya 2021 nyota huyo aling’ara alipokuwa na kikosi cha Gwambina kutokea Misungwi kule Mwanza.

Gustapha alisifika zaidi kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani ukichagizwa na akili na uwezo alionao mchezoni.

Gustapha pia aliwahi kuichezea timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20 mwaka 2019 na kiwango alichokionyesha kilimfanya kocha wa Yanga wa kipindi hicho Mwinyi Zahera kumpandisha nyota huyo kutoka kikosi cha vijana hadi kikosi cha wakubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *