Dar es Salaam. Hassan Yusuph (20) na Warioba Masenza (23) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 1,045

Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo leo Jumatatu Juni 15, 2026 na kusomewa shtaka lao na wakili wa Serikali, Winniwa Kasala, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Anna Magutu.

Wakili Kasala amedai Desemba 17, 2025 katika eneo la Mwenge, Mtaa wa Mlalakuwa Wilaya ya Kinondoni Dar es salaam, washtakiwa walikutwa na dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa gramu 1,045.

New Content Item (1)

Washtakiwa wanaodaiwa kusafirisha bangi zenye uzito wa gramu 1,045, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kusomewa shtaka lao.

Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka lao, walikana kutenda kosa hilo.

Upande wa Jamhuri wamedai upelelezi umekamilika hivyo waliomba tarehe nyingine kwa ajili ya kupata muda wa kukamilisha hoja za awali na taarifa nyingine. Pia alidai shtaka wanalokabiliwa nalo lina dhamana.

Hakimu Magutu alitoa masharti ya dhamana ambayo, kila mshtakiwa anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye kitambulisho cha Nida na mmoja kati ya yao anatakiwa awe mfanyakazi kutoka katika taasisi inayotambulika kisheria.

Washtakiwa wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na kesi hiyo imeahirishwa hadi Julai Mosi, 2026 itakapotajwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *