
Nairobi. Rais wa Kenya, William Ruto, amesema kuwa serikali haitavumilia vitendo vya vurugu, uharibifu wa mali na machafuko wakati baadhi ya vijana wa nchi hiyo wakitangaza kufanya maandamano Juni 25 wiki ijayo.
Mpango huo wa baadhi ya vijana wa Kenya ni maadhimisho ya kumbukumbu ya maandamano yaliyofanyika Juni 25, 2024 nchini humo ambapo maelfu ya vijana maarufu ‘Gen Z’ walifanya maandamano ya kupinga Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024 (Finance Bill 2024)
Wakati huo waandamanaji waliingia ndani ya viunga vya Bunge jijini Nairobi baada ya wabunge kupitisha muswada huo waliodai una utata.
Akizungumza leo Ijumaa Juni 19,2026 katika mkutano wa kitaifa wa utendaji na uzalishaji uliofanyika Ikulu ya Nairobi, Rais Ruto amesema Kenya itaendelea kulinda haki za wananchi za kuandamana, lakini akasisitiza uhuru huo haupaswi kutumiwa kuhatarisha utulivu, uchumi na maendeleo ya nchi.
“Kenya ni taifa linaloamini kwa dhati katika utaratibu, sisi ni taifa lililostaarabika, jamii iliyopangika na tunaamini katika utawala wa sheria,” amesema Ruto.
Rais huyo ameeleza kuwa kila mwananchi ana haki ya kuwasilisha malalamiko yake au kuandamana kwa mujibu wa sheria, huku Serikali ikiwa na wajibu wa kulinda haki hizo.
“Haki ya kuandamana na kuwasilisha malalamiko lazima ilindwe, hata hivyo, jambo ambalo halitakubalika ni watu kuhamasishwa kuharibu mali, kusababisha vurugu au machafuko,” amesema.
Kauli ya Ruto inakuja wakati hali ya kisiasa nchini humo ikiendelea kuwa ya tahadhari kutokana na maandalizi ya maadhimisho ya maandamano ya Juni 25, huku vyombo vya usalama vikitarajiwa kuimarisha ulinzi katika Jiji la Nairobi na maeneo mengine ya mijini.
Rais huyo amesisitiza umuhimu wa kulinda shughuli za kiuchumi na kijamii, akisema sekta muhimu kama elimu, kilimo na biashara hazipaswi kuathiriwa na maandamano.
“Lazima tulinde haki ya watoto wetu kwenda shule na kujifunza, wakulima wanapaswa kuendelea na shughuli za uzalishaji wa chakula ili kuhakikisha taifa halikabiliwi na njaa, pia wafanyabiashara wanapaswa kuendelea na shughuli zao za kiuchumi,” amesema.
Ameongeza kuwa wafanyakazi wote wanapaswa kupewa mazingira salama ya kwenda kazini ili kuongeza uzalishaji wa taifa na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Katika hotuba yake, Ruto ametoa wito wa umoja wa kitaifa na kuhimiza wananchi kuzingatia zaidi ajenda ya maendeleo badala ya migawanyiko ya kisiasa.
Amesema Kenya ina rasilimali, nguvu kazi na uwezo mkubwa wa kiuchumi ambao unapaswa kutumika kikamilifu ili kuharakisha maendeleo ya nchi.
“Kwa muda mrefu tumekubaliana na hali ya kufanya mambo kwa kiwango cha kawaida na kuathiri maendeleo ya taifa letu. Hakuna sababu ya msingi kwa Kenya kubaki nyuma wakati nchi kama Singapore, Korea Kusini na Malaysia zimefikia hadhi ya mataifa yaliyoendelea,” amesema.
Wakati huohuo, Ubalozi wa Marekani nchini Kenya umetoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake ukionya uwezekano wa kutokea maandamano katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo kuelekea maadhimisho ya Juni 25.
Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi Juni 18,2026, ubalozi huo ulieleza maandamano yanaweza kutokea wakati wowote, ingawa uwezekano mkubwa unatarajiwa kuongezeka kadri tarehe ya maadhimisho inavyokaribia.
Ubalozi huo ulionya maandamano hayo yatasababisha msongamano mkubwa wa magari, kufungwa kwa baadhi ya barabara na usumbufu wa usafiri katika maeneo mbalimbali, hususan katikati ya Jiji la Nairobi na miji mingine mikubwa nchini Kenya.
Habari hii imeandikwa kwa msaada wa mtandao wa Ikulu ya Kenya (YouTube).