Dar es Salaam. Wakati vyombo vya habari vikihimizwa kuongeza juhudi za kufichua matukio ya ukiukaji wa maadili miongoni mwa viongozi wa umma, wadau wa habari wameeleza kuwa kuwekwa wazi kwa mali za viongozi hao ni hatua muhimu ya kuimarisha uwajibikaji, uwazi na imani ya wananchi kwa taasisi za umma.

Wamesema hatua hiyo itasaidia kuondoa mkanganyiko wa uelewa katika jamii na kuweka msingi imara wa kudhibiti mgongano wa masilahi na vitendo vya ufisadi.

Aidha, hatua hiyo imeelezwa itavifanya vyombo vya habari kuwa na uwezo wa kufikia taarifa za mali za viongozi na kuziweka bayana.

Wito huo unetolewa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile katika kikao kazi kilichoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma wakikutana na Jukwaa la Wahariri na waandishi wa habari leo Juni 19, 2026 jijini Dar es Salaam.

“Sheria nadhani iongezewe, isiishie kwenye kuripoti, kuchunguzwa na mamlaka ambapo jamii itabaki na maswali. Viongozi hawa kama wanajua hawana cha kuficha sheria iruhusu vyombo vya habari vipate uwezo wa kuripoti kujua kiongozi fulani anamiliki kitu fulani.

“Tukiwa na taarifa sahihi itaondoa mkanganyiko kwa jamii kudhani fulani anamiliki mali fulani, lakini tungekuwa na sheria inayoweka wazi mtu anachomiliki kinawekwa kwenye mtandao ingeondoa mkanganyiko,” amesema.

“Tukiendelea hivi watu wataendelea kusingizia mali fulani ni za kiongozi Fulani, kwa sababu hatuna taarifa,” ameongeza.

Katika kikao kazi hicho cha leo Ijumaa Juni 19, 2026,  Katibu Usimamizi wa Maadili kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Kassim Mkwawa amesema chunguzi zinaendelea kufanyika ili kubaini uvunjfu wa maadili.

“Kwa kipindi cha miaka minne kuna zaidi ya viongozi kumi ambao kesi zao zimefanyiwa kazi,” amebainisha huku akisema hali ya maadili nchini ni nzuri.

“Kuna kazi inayofanyika na mitazamo ya watu. Serikali kwa kushirikiana na sekretarieti imeendelea kusimamia uadilifu na viongozi wengi ni waadilifu,” amesema.

Mchango wa vyombo vya habari

Katika kikao kazi hicho, Waziri Kipacha, katibu ukuzaji Maadili katika ofisi hiyo ameeleza kuwa vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kushughulikia na kudhibiti mgongano wa masilahi.

Miongoni mwa majukumu yake amesema ni kufanya uchunguzi na kufichua vitendo vya mgongano wa masilahi kwa kufuatilia taarifa za maofisa wa Serikali, wanasiasa na watunga sera wenye masilahi ya kifedha yasiyowekwa wazi, wanaoonyesha upendeleo au wanaotumia ushawishi usiofaa katika maamuzi ya umma.

Pia, vyombo vya habari vinaweza kutoa jukwaa salama kwa watoa taarifa na wafichuzi wa nyaraka zinazohusu biashara zenye utata au mipango ya kifisadi, na hivyo kusaidia kuhimiza hatua za kinidhamu au kisheria dhidi ya watumishi wa umma wasio waadilifu.

Aidha, vina jukumu la kuwaelimisha wananchi kuhusu athari za mgongano wa masilahi kwa kuandaa kampeni za uhamasishaji, kuandika makala na kuendesha vipindi vinavyoeleza jinsi mgongano wa masilahi wa kimfumo unavyoweza kudhoofisha utoaji wa huduma za umma, kuathiri ushindani wa soko na kuchochea vitendo vya ufisadi.

Kauli ya Mwigulu

Mjadala huo umekuja siku chache baada ya Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba kusema Serikali itafanya maboresho ya sheria na mifumo ya uwajibikaji katika utumishi wa umma ili kuwabaini na kuwachukulia hatua watumishi wanaotumia mianya ya kiutendaji kujinufaisha huku wakikwepa mifumo ya ufuatiliaji iliyopo.

Dk Mwigulu alisema hatua hiyo inalenga kurekebisha dosari zilizopo katika mifumo ya sasa ya uwajibikaji ambayo imekuwa ikiwalenga zaidi baadhi ya viongozi huku ikiacha maeneo mengine yenye hatari kubwa ya upotevu wa rasilimali za umma.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Iringa Juni 6, 2026, Dk Mwigulu alisema Serikali haijaridhishwa na namna baadhi ya taasisi za usimamizi wa maadili zinavyotekeleza majukumu yake, akitaja kuwa nguvu kubwa imeelekezwa katika kufuatilia viongozi kujaza fomu za maadili na kutaja mali zao.

“Tuna sekretarieti yetu ya maadili, na nilishawaelekeza. Kwa kiwango kikubwa wanashughulika na kumulika wanasiasa wajaze fomu za maadili, wataje mali walizo nazo. hatupingi wajaze, lakini…

“Kuna watu wengine wamekaa pazuri, wametegesha rada zao wanavuna hawaonekani, halafu kuna wengine ambao wako kwenye ukame, ndiko tochi zimeelekezwa, ndiko mitego ilipo. Sasa haya na yenyewe tumesema lazima tuyasimamishe,” amesema Dk Mwigulu.

Kutokana na hali hiyo, alisema Serikali imeanza kupitia upya mifumo ya uwajibikaji kupitia Sekretarieti ya Maadili na taasisi nyingine za usimamizi ili kuhakikisha maeneo yote yenye hatari ya upotevu wa fedha za umma yanawekwa chini ya uangalizi sawa na kuondoa mianya ya upigaji ndani ya Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *