
Mazungumzo ya kidiplomasia kati ya Iran na Marekani nchini Uswisi, yaliyokusudiwa kuimarisha Hati ya Makubaliano (MoU) iliyosainiwa hivi karibuni, yameahirishwa.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bw. Esmaeil Baghaei, amethibitisha uamuzi huo, huku akionyesha kutoridhishwa na hali ya Israel kuendeleza mashambulizi nchini Lebanon, jambo ambalo ni uvunjifu wa wazi wa makubaliano hayo mapya.
Mazungumzo hayo, yaliyokuwa yakitarajiwa kufanyika Ijumaa, yalitokana baada ya ‘Makubaliano ya Islamabad’, mkataba wa vipengele 14 uliosainiwa na pande zote mbili mapema wiki hii. Mkataba huo unalenga kuweka msingi wa kumaliza uhasama katika nyanja zote, ikiwemo Lebanon, kufungua Lango Bahari la Hormuz kwa shughuli za kibiashara, na kuanza mchakato wa majadiliano kuhusu masuala nyeti ndani ya kipindi cha siku 60.
Akizungumza na wanahabari siku ya Ijumaa, Bw. Baghaei alifafanua ramani ya mchakato wa hatua za mazungumzo hayo, akisisitiza kuwa “mashauriano ya kina” bado yanaendelea kupitia wapatanishi.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa maandishi ya mkataba huo (MoU), kuanza kwa mazungumzo ya mwisho kunategemea utekelezaji wa dhati wa vifungu vya 1, 4, 5, 10, na 11. Hivyo, kuahirishwa kwa mazungumzo hayo kunatokana na ukweli kuwa malengo ya awali yameshaanza kutekelezwa kupitia njia nyingine mbadala.
‘Makubaliano ya Islamabad’ yaliyosainiwa na marais wa nchi zote mbili Alhamisi iliyopita, ni matokeo ya miezi kadhaa ya juhudi kubwa za upatanishi zilizoongozwa na Pakistan, kwa ushirikiano wa nchi nyingine za kanda hasa Qatar.
Hata hivyo, Israel, ambayo imesalia nje ya mchakato huo wa amani, imejitenga na makubaliano hayo na inaendelea na operesheni zake za kijeshi katika maeneo ya makazi kusini na mashariki mwa Lebanon.
Licha ya tangazo la kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na harakati ya Hizbullah, lililotarajiwa kuanza saa nne usiku siku ya Ijumaa, ripoti za mashambulizi mapya ya anga ya Israel ziliendelea kusikika muda mfupi baada ya makubaliano hayo kutakiwa kuanza. Mashambulizi hayo ya kikatili yamesababisha vifo vya watu zaidi ya 30, wakiwemo wanawake na watoto. Kwa upande mwingine, vikosi vya Hizbullah vimeendelea na mapambano ambapo jana vimeagamiza wanajeshi 4 wa Israel na kujeruhi wengine zaidi ya 10 katika mapigano makali yaliyoendelea kusini mwa Lebanon.