TUNAWATAKA! Ndio kauli ya mashabiki wa Simba kwa sasa baada ya kikosi hicho kutinga fainali ya Kombe la CRDB kwa kuifunga Coastal Union mabao 4-0, katika mechi ya nusu fainali iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Mashabiki wa kikosi hicho walikumbushia fainali ya Julai 25, 2021 na Simba iliifunga Yanga bao 1-0 na kubeba ndoo.

Katika mechi hiyo nyota wa kikosi hicho Libasse Gueye aliifungia Simba bao la kwanza la dakika ya 19, baada ya kupokea pasi nzuri ya kiungo, Neo Maema na kupiga shuti lililomshinda kipa wa Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, Wilbol Maseke.

Dakika ya 55, Simba ikapata bao la pili lililofungwa na beki wa kushoto, Nickson Kibabage aliyemaliza mpira uliookolewa na kipa wa Coastal Union, Wilbol Maseke aliyekuwa anaokoa shuti lililopigwa na Gueye.

Wakati Coastal Union ikipambana kusawazisha mabao hayo, dakika ya 75 Simba ilipata bao la tatu lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Rushine De Reuck baada ya beki wa kikosi hicho, Anthony Mligo kufanyiwa madhambi akiwa eneo la hatari.

Dakika ya 79, Clatous Chama akaifungia Simba bao la nne lililotokana na mpira aliotengewa na mshambuliaji wa kikosi hicho, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ na kuihakikishia timu hiyo ushindi unaoipeleka katika fainali ya Kombe la CRDB.

Fainali hiyo kwa Simba ni ya kwanza katika Michuano ya Kombe la CRDB baada ya miaka minne, miezi 10 na siku 26, tangu mara ya mwisho ilipocheza Julai 25, 2021 na kuifunga Yanga kwa bao 1-0, kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini, Kigoma.  Kwa sasa matumaini ya kikosi hicho ya kutwaa taji hilo ililolikosa kwa misimu minne mfululizo na kwenda kwa watani zao Yanga huenda ikatimia.

Tangu mechi hiyo hadi Juni 20, 2026, Simba imetumia siku 1791 kufika fainali baada ya kusota kwa muda mrefu na kuwashuhudiwa watani zao Yanga ikitamba kwa kuchukua ubingwa huo kwa misimu minne mfululizo.

Safari ya Simba msimu huu katika Kombe la CRDB, ilianza hatua ya 64 kwa kuifunga Greenland FC ya Kagera mabao 3-0, kisha hatua ya 32 ikaichapa B19 FC 2-0 na 16 bora ikaifunga Dodoma Jiji 3-1 na robo fainali ikaitoa TRA United kwa mabao 4-0.

Simba ambao ni mabingwa wa Kombe la CRDB mara nne huku mara ya mwisho ikichukua msimu wa 2020-2021, inasubiria mshindi wa leo wa mechi ya pili ya nusu fainali kati ya Yanga dhidi ya Azam FC, itakayopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *