MATOKEO ya kupoteza mchezo dhidi ya Simba, yameonekana kuwavuruga Mbeya City katika hesabu za kukwepa kushuka daraja, huku kocha mkuu wa timu hiyo Salum Mayanga, akitaja kitakachowabeba.

Mbeya City ikiwa nyumbani jana ilikutana na kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Simba na kuwaacha nafasi yao ya 14 kwa pointi 25, ambapo kwa sasa wamebakiza michezo mitatu iliyoshikilia hatma yao.

Timu hiyo iliyorejea Ligi Kuu msimu huu haijawa na matokeo mazuri, ambapo baada ya kumalizana na Simba itacheza mechi mbili ugenini dhidi ya Dodoma Jiji, Pamba Jiji kisha kumalizia Sokoine Mbeya dhidi ya TRA United.

Katika mechi hizo, City itahitaji kushinda zote ili kufikisha pointi 34, ambazo kwa hesabu zinaweza kuinusuru na aibu ya kushuka daraja kuungana na KMC ambao tayari wameshaaga Ligi Kuu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga amesema kwa sasa timu imekuwa na muunganiko mzuri na ubora wa mchezaji mmoja mmoja unaweza kuibeba City katika michezo iliyobaki na kukwepa kushuka daraja.

Amesema benchi la ufundi linaendelea kuboresha na kusahihisha makosa yaliyoonekana haswa eneo la beki ili kuondokana na mwendelezo wa kuruhusu bao kila mchezo wakati huohuo safu ya ushambuliaji kuongezewa makali.

“Kwa mechi zilizobaki tunaenda kupigana kufa na kupona kusaka pointi tisa, nashukuru vijana wamekuwa na muunganiko mzuri na kila mmoja anaonesha uwezo na juhudi binafsi, ari na morali ni kubwa kikosini.

“Benchi la ufundi linaendelea na wajibu wake kusahihisha makosa madogo madogo yanayoonekana, lakini tunaridhishwa na kiwango wanachoonesha uwanjani, naamini tutabaki salama Ligi Kuu,” amesema Mayanga.

Straika wa timu hiyo, Eliud Ambokile amesema bado wanaendelea kupambania nafasi yao kwa mechi zilizobaki kuhakikisha wanapata ushindi na matokeo waliyonayo ni ngumu kukata tamaa.

“Niwaombe mashabiki wasitukatie tamaa bado mechi zipo na sisi wachezaji tunayo ari na morali, tunaamini hizi michezo iliyobaki tukishinda tunakuwa salama na ndio kampeni yetu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *