
Dar es Salaam. Watumiaji wa WhatsApp sasa wanaweza kusoma ujumbe wa sauti ‘voice note’ waliotumiwa badala ya kuusikiliza baada ya kampuni hiyo kuendelea kuboresha huduma zake kwa kuanzisha kipengele cha kutafsiri ujumbe wa sauti kuwa maandishi.
Kipengele hicho kinachoitwa Voice Message Transcripts kinabadilisha ujumbe wa sauti kuwa maandishi yanayoweza kusomwa moja kwa moja chini yake.
Hatua hiyo inalenga kuwasaidia watumiaji wanaoshindwa kusikiliza ujumbe katika mazingira yenye kelele au wakati ambao hawawezi kutumia sauti.
Ili uweze kuitumia huduma hiyo kwa mujibu wa WhatsApp lazima aiwashe kupitia kwenye settings. Baada ya kuwashwa, mpokeaji wa ujumbe huo wa sauti ataweza kuona maandishi yaliyotafsiriwa, huku mtumaji akiwa hawezi kuyaona.
WhatsApp imeeleza tafsiri hizo hutengenezwa moja kwa moja ndani ya kifaa cha mtumiaji na si kwenye seva za kampuni, jambo linalosaidia kulinda usiri wa mawasiliano kupitia teknolojia ya end-to-end encryption.
Kwa sasa, huduma hiyo inapatikana kwa lugha nne pekee ambazo ni Kiingereza, Kireno, Kihispania na Kirusi.
Jinsi ya kuwasha
Ili kutumia huduma hiyo, mtumiaji anatakiwa kwenda kwenye sehemu ya settings, kisha chats na kuwasha kipengele cha Voice Message Transcripts. Baada ya hapo atachagua lugha inayotumika zaidi kwenye ujumbe wa sauti anaopokea.
Baada ya kuwezesha huduma hiyo, mtumiaji anaweza kubonyeza vidoti vitatu vilivyopo upande wa juu kulia, kisha kuchagua chaguo la Transcribe ili kuona maandishi ya ujumbe huo.
Mbali na maboresho hayo, WhatsApp imeendelea kusisitiza matumizi ya ujumbe wa sauti kama njia ya haraka ya mawasiliano kati ya watu binafsi na makundi.
Kwa mujibu wa kampuni hiyo, ujumbe wa sauti umeendelea kuwa moja ya njia maarufu za mawasiliano kwa sababu unarahisisha kutuma taarifa za haraka bila kulazimika kuandika maandishi marefu.
Kuanzishwa kwa huduma ya kutafsiri ujumbe wa sauti kunatazamwa kama hatua nyingine ya WhatsApp katika kutumia teknolojia kuboresha upatikanaji wa taarifa na kurahisisha mawasiliano kwa watumiaji wake duniani.