Dar es Salaam. Wataalamu wa afya wamezitaka nchi za Afrika kuongeza juhudi za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) kutokana na idadi ya wagonjwa na vifo vinavyotokana na magonjwa hayo yanaongezeka.

Wataalamu hao wamesema magonjwa yasiyoambukiza, shinikizo la damu, kisukari, saratani na magonjwa ya moyo yanazidi kuibuka kuwa janga la afya kwa watu barani Afrika kutokana na kuchangia vifo vingi.

Wakinukuu takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), wamesema mwaka 2000 magonjwa yasiyoambukiza yalikuwa yakichangia vifo kwa asilimia 24 kwa Afrika lakini sasa ni asilimia 37 na hatua za haraka zisipochukuliwa hali itakuwa mbaya zaidi 2030.

Akizungumza leo Juni 23, 2026 katika Mkutano wa tatu wa Kimataifa wa PEN-Plus jijini Dar es Salaam, Kiongozi wa Kitengo cha Magonjwa yasiyoambukiza na Afya ya Akili wa WHO Kanda ya Afrika, Profesa Kofi Mensah Nyarko, amesema magonjwa hayo yanazidi kuhatarisha mifumo ya afya barani humo.

Washiriki mbalimbali wa mkutano wa tatu wa Kimataifa wa PEN Plus uliofanyika Dar es Salaam.

“Nusu ya watu wenye shinikizo la damu hawafahamu hali zao za kiafya na hali hiyo inaonekana kwa wagonjwa wengi wa kisukari, watu hufika hospitalini baada ya kupata madhara makubwa kama kiharusi, matatizo ya figo au magonjwa ya moyo,” amesema.

Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ukosefu wa uchunguzi wa afya wa mara kwa mara pamoja na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ni miongoni mwa sababu zinazochelewesha utambuzi na matibabu ya mapema.

Profesa Nyarko amesema ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza linachochewa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mtindo wa maisha yanayotokana na ukuaji wa miji, matumizi ya vyakula visivyo na lishe bora, matumizi ya tumbaku, unywaji wa pombe kupita kiasi pamoja na kutofanya mazoezi ya kutosha.

“Mitindo yetu ya maisha imebadilika sana katika miaka ya karibuni, watu wanafanya mazoezi kwa kiwango kidogo, wanatumia vyakula visivyo bora kiafya na wanaishi katika mazingira yasiyowasaidia kufanya uchaguzi sahihi wa kiafya,” amesema.

Profesa huyo amesisitiza umuhimu wa Serikali za Afrika kuweka sera madhubuti zaidi za kudhibiti vihatarishi vya magonjwa hayo.

Ametaja changamoto zinazotatiza kukabiliana na magonjwa hayo, kama ukosefu wa miundombinu rafiki kwa watembea kwa miguu na waendesha baiskeli, utekelezaji hafifu wa sheria za tumbaku na pombe pamoja na uhaba wa maeneo salama ya mapumziko na mazoezi.

Profesa Nyarko ametoa wito kwa Serikali za Afrika kuongeza fedha za ndani kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza, akionya utegemezi mkubwa wa fedha za wafadhili unadhoofisha juhudi za kufikia huduma za afya kwa watu wote na kupunguza vifo vinavyotokea kabla ya wakati.

Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akifungua mkutano huo Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Profesa wa tiba Hospitali ya Brigham ya nchini Marekani, Gene Burkhman amesema changamoto ya upungufu wa fedha katika sekta ya afya inaendelea kuhatarisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa mamilioni ya Waafrika.

“Nchi nyingi bado zinategemea ufadhili ili kuwa na uwezo wa ndani wa kugharamia huduma za msingi za afya, wananchi wanatarajia kupata huduma bora za matibabu, hivyo tunapaswa kutafuta njia endelevu za kuhakikisha huduma hizo zinapatikana,” amesema.

Akizungumzia mkakati wa PEN-Plus, Profesa Burkhman amesema umeanza kuonyesha matokeo chanya kwa kuokoa maisha ya wagonjwa huku ikiimarisha mifumo ya utoaji huduma za afya.

“Huduma za PEN-Plus zinaokoa maisha ya vijana wengi kwa sasa, lakini pia zinachangia kuboresha kwa ujumla huduma za afya katika ngazi ya msingi na hospitali za rufaa,” amesema.

Amesema upanuzi wa programu hiyo unaweza kuokoa mamia ya maelfu ya maisha katika kipindi cha miaka 10 ijayo, hususan kwa watoto na vijana ambao ndio kundi kubwa la wanufaika wa huduma hizo.

Akizungumzia umuhimu wa uwekezaji katika mpango huo, Profesa huyo amesema PEN-Plus kuwa ni miongoni mwa uwekezaji wenye tija katika sekta ya afya.

Alisema uchambuzi wa kiuchumi unaonyesha kuwa faida zinazoweza kupatikana kutokana na upanuzi wa programu hiyo zinaweza kuzidi gharama za utekelezaji kwa zaidi ya mara nne.

Fahamu hili

Dhima ya mkutano huo ni kuharakisha Mafanikio ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ya kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza Afrika ifikapo 2030, tathmini ya utekelezaji wa PEN-Plus, changamoto na mwelekeo wa baadaye.

Mkutano umekuja baada ya wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika kuridhia utekelezaji wa mkakati wa PEN-Plus, unaolenga kuimarisha utoaji wa huduma jumuishi kwa wagonjwa wenye magonjwa sugu na magumu yasiyoambukiza katika hospitali za rufaa za ngazi ya kwanza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *